Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti kubwa ya Serikali yetu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Timu yake yote kwa bajeti nzuri ambayo ipo chini ya Rais wetu, bajeti inayojibu matakwa ya wanyonge wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitachangania mambo kama matatu au manne, lakini kubwa sana ni kilio kikubwa cha wananchi wangu wa Mkalama. Katika bajeti hii yameongelewa mambo mengi lakini mojawapo ni la barabara. Naishukuru Wizara imekuja na mpango mpya wa ujenzi wa barabara kwa mtindo wa EPC+F, mtindo huu ni mzuri kwa sababu mkandarasi anajenga barabara kwa fedha zake, Serikali inaendelea kumlipa taratibu wakati wananchi wakitumia barabara. Kwa mtindo huu zimetajwa barabara kadhaa lakini mojawapo ni Barabara ya kutoka Meatu, Mbulu na ikaelekea Daraja la Sibiti kwenda Lalago mpaka Maswa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la barabara hii kuambaambaa pembeni mwa Mkalama kwenda kufuata Daraja la Sibiti ni kufuata daraja hili ili kuvuka Mto Sibiti, lakini kimsingi kabisa daraja hili lilijengwa kwa nia ya kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida na ndiko liliko daraja hili. Kwa hiyo, kuambaambaa kwa barabara hii ni kulifuata daraja. Sasa inasikitisha sana kwa wananchi wangu wa Mkalama kuiona barabara ikiambaambaa pembeni mwa wilaya kufuata daraja ambalo wamelilia kwa miaka mingi mpaka limekamilika, leo linavusha barabara zingine kuunganisha Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Arusha wakati wenyewe wa Singida wakitazama kwa mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi si muumini wa kutaka changu kwa kukandamiza wengine, nimwombe Mheshimiwa Waziri kaka yangu, pacha wangu, tunachangia jimbo, wilaya moja baba yetu mmoja Iramba, Waziri yuko Magharibi mimi nipo Mashariki. Tumeacha jina la Iramba Mashariki kulinda historia kwa mawazo ya Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri Barabara hii ya Lalago inayotoka Meatu kwenda Lalago mpaka Sibiti iwepo, ni nzuri sana, inamega kidogo katika jimbo langu, lakini barabara hii ikifika Sibiti inaacha kipande kidogo cha kilometa kama 120 kutoka Iguguno mpaka Sibiti. Katika hizi kilometa 120 kuna kilometa 20 tayari zinajengwa kama matolezi ya daraja, kwa hiyo, zinabaki kama kilometa 105 ukiunganisha kilometa hizi 105 na zile kilometa 389 zinakuwa kilometa 494. Kwa sababu mpango wenyewe ni EPC+F ambao mkandarasi anajenga kwa fedha zake kama ataongezea kipande hiki atakuwa hajaathiri bajeti yake Mheshimiwa Waziri, kwa sababu anajenga Serikali inaendelea kulipa polepole. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri barabara hii isomeke kwamba inatoka Karatu inapita Mbulu inakwenda Sibiti inakutana na matawi mawili; tawi moja linakata kwenda Iguguno kwa kupitia katika jimbo langu na hii inaelekea Meatu. Kwa hiyo, inakuwa kilometa 494. Akiikabidhi hii kwa EPC+F maana yake atakuwa hajaathiri bajeti yake. Nimwombe sana kaka yangu hii inasabisha sasa hata wapita njia wameanza kudandia barabara hii kama political mileage yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana sana Waziri utakapokuja ku-windup uje uongeze kipande hiki hakitaathiri bajeti yako na mimi mdogo wako utaendelea kunifanya niendelee. Hivi sasa huko jimboni ni gumzo tupu kuhusu mimi na wewe ambao ni mapacha. Nikuombe sana Waziri, nipo chini ya miguu yako, ingekuwa kanuni hazijazuia hapa ningeanza kugalagala lakini kanuni imezuia. Kwa hiyo nikuombe sana Waziri utakapokuja ku-windup ujumlishe kipande hiki na kuwa… (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Francis wakati mwingine maombi yanakuwa hayasikiki vizuri kwa sababu unaongea na yeye wewe ongea na mimi, mimi ndiyo ananisikiliza yeye.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naomba ukikazia hii barabara mimi kijana wako angalau nirudi awamu ya pili hapa nitashukuru sana. Baada ya kilio changu hicho sasa niende kwenye mambo ya kitaifa.

Mheshimiwa Spika, hapa tunalia ili tupate kodi na mimi nataka niende kwenye suala zima la kodi. Sheria ya Kodi ya mwaka 2015 kifungu cha 35 kinawatambua walipakodi wadogo wanaopata mauzo kuanzia milioni nne mpaka milioni mia moja. Katika kiwango hiki cha walipakodi hawa sheria imetenga wigo wa madaraja kama manne tu ya walipakodi, kwa maana ya kwamba wanaopata mauzo chini ya milioni nne wanapata kitambulisho kile cha mlipakodi ambaye hasumbuliwi, lakini kuanzia milioni nne mpaka milioni saba wanalipa shilingi laki moja kwenye ule wigo. Kuanzia mauzo ya milioni saba mpaka kumi na moja wanalipa laki mbili na nusu na kuanzia kumi na moja mpaka kumi na nne wanalipa laki nne nusu, madaraja yanaishia hapo lakini tukumbuke wigo unatambua mpaka milioni mia moja. Kwa hiyo, kuanzia milioni kumi na nne kwenda juu yule afisa inabidi sasa achukue kile kiwango cha mauzo, halafu anakipiga asilimia 3.5 anajumlisha na laki nne na nusu. Hapa ndipo wafanyabiashara wengi wanapoanza kulalamika kwamba wanaonewa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kinachochukuliwa ni mauzo, sasa mtu anaweza kuwa na mauzo ya milioni hamsini, lakini katika yale mauzo ya milioni hamsini kiasi kikubwa ni mtaji wake, faida pale ni ndogo sana, lakini sasa inapigwa pale asilimia tatu inajumuishwa na laki nne na nusu anaambiwa alipe kodi ambayo anaona anaonewa sana. Kwa hiyo, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri kaka yangu alete hii sheria kwanza nikiwatambua wafanyabiashara katika wigo mpana huo wa milioni nne mpaka mia moja, hata haya madaraja sasa yasiwe manne, yaongezeke kwa maana ya tofauti hata ya laki moja moja kuanzia laki moja, laki mbili, laki tatu mpaka huko juu ili yule Afisa wa Kodi anapokuja akiangalia mauzo, mtu ameuza milioni 50 anajua category yake ni hii hapa, wala haina mabishano wala haina malalamiko. Kwa hiyo, niombe sheria hii iletwe tuiangalie upya, tuongeze madaraja ili tuondoe huu wigo wa kukadiriana kwa asilimia 3.5 halafu mtu ni mauzo na wala si faida inawaumiza watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la EFD machine; EFD machine ni chombo kinachosaidia TRA kukusanya kodi lakini mpaka sasa EFD machine zinaagizwa na wafanyabiashara binafsi na wanapokuja hapa wanawauzia wafanyabiashara wenzao sasa hao wafanyabiashara kwanza hawana ofisi wilayani ofisi, zao zinaishia mkoani na hata hizi EFD machine zinapoharibika inabidi wairudishe kwa wakala yuleyule akatengenezewe kwa malipo. Sasa wale wafanyabiashara waliopo vijijini inabidi ahangaike kusafiri mpaka mkoani aende akatengenezewe au kuituma inakaa wiki mbili sasa katika kipindi hiki kwanza Serikali inakosa mapato kwa sababu katika kipindi hiki wakati hii EFD inatengenezwa huko wilayani ina maana Serikali inaendelea kukosa kodi na hata hao wafanyabiashara mawakala wanaweza waka-collude na wafanyabiashara kwamba chelewesha chelewesha hiyo mashine huko hata wiki mbili huku yeye anaendelea kuuza na Serikali inakosa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inakuja inamrudishia, inakata mtu kodi kwa sababu alinunua EFD machine, anakatwa kodi kupunguziwa kodi yake, sasa aliyeuza ni mfanyabiashara, halafu Serikali inakuja inampunguzia kodi mwingine kwa kufidia. Kwa hiyo, ina maana yule mfanyabiashara wakala amelipiwa na Serikali EFD, kwa nini TRA wasiagize EFD machines wao wenyewe? Waanzishe vitengo kwenye mikoa kule na kwenye wilaya kiwepo kitengo maalum cha EFD ambacho kitakuwa kinahudumiwa na Serikali ikibidi kutugawia bure kama ni kuuza basi itakatwa kwenye zile session nne za kulipa kodi katika mwaka, lakini ikae mikononi mwa Serikali, TRA wenyewe wamiliki EFD machine. Huu mkataba wa kuwaachia wafanyabiasha wengine wawatoze wafanyabiashara wenzao unaumiza na unaiumiza Serikali pia Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka niguse kidogo kwenye Bima ya Taifa NIC, hili Shirika la Bima. Shirika hili ni la kwetu limeanzishwa na baba wa Taifa shirika hili lililegalega sana leo zimeanzishwa bima nyingi naomba Serikali sasa iipe mtaji shirika hili ili liweze kujiendesha lishindane na mashirika mengine ya bima na wateja kama Wakala wa Serikali, halmashauri zote zinakata bima ziende zikakate kwenye shirika hili ili kulipa mtaji liweze kushindana, tupate gawio tuongeze kodi Serikalini. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)