Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hoja tatu zilizoko Mezani. Pamoja na kukupongeza kwa kazi nzuri ya kuliongoza Bunge na kuaminiwa na dunia, umeiheshimisha sana nchi yetu. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyofanya ya Kidiplomasia ambayo kwa kweli ndiyo imejenga msingi wa Tanzanaia kuendelea kuaminiwa Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazipongeza ripoti zilizowasilishwa Mezani za Kamati zetu, ripoti zote tatu. Wamefanya kazi nzuri. Najua walikuwa wanakesha, wanahangaika kuhakikisha ripoti zinafika hapa. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na ofisi yake. Wanatufanyia kazi nzuri sana. Kwa siku tatu nimeona uzalendo wa Wabunge hapa, jinsi wanavyopiga kelele, jinsi wanavyohangaika kuhakikisha kwamba, nchi yetu inatendewa haki kwenye kusimamia rasilimali za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu ni ushahidi kwamba Chama cha Mapinduzi kinalea vizuri, kwa sababu Wabunge wengi ni wa CCM. Ripoti zi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali zimekuwepo kwa muda na mimi nimepata bahati ya kuzipitia sana. Nikiwa Katibu Mwenezi, tulikuwa na utaratibu zilikuwa zinaletwa pia CCM, tunazipitia. Nimekuwa Mbunge hapa mwaka 2015 na sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja kubwa kwenye hizi ripoti, toka zimeanza kuletwa na toka zimeanza kufanyiwa kazi kwanza, kuna kazi kubwa sana ambayo imefanyika ya kuboresha mambo kwa kuzitumia hizi ripoti. Ndiyo maana ukienda kuangaliwa takwimu zinaonesha kwamba, kule yako matatizo yaliyokuwa yanatokea ambayo leo hayatokei. Ukiangalia ripoti baada ya ripoti yako mambo mengi sana yamebadilika. Hati safi zimeongezeka. Baadhi ya query ambazo zilikuwa zinatokea nyuma, nyingi zimerekebishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi Waziri nasimamia TEHAMA.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Moja ya uamuzi wa kwenda kushushughulikia makusanyo ya Serikali kwa kuweka TEHAMA, yametokana na ripoti za CAG katika mkakati wa Serikali wa kuziba myanya ya kupotea kwa mapato ya Serikali.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: …Nilichokuwa nataka kusema ni kwamba, ripoti hizi zina manufaa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nape, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia.

TAARIFA

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mzungumzaji anayeeleza vizuri. Kwa mujibu wa CAG anasema, “Hizo hati zimebadilika kwa sababu wezi wamejua namna nzuri ya kuiba au kutumia risiti kuwasilisha vielelezo.” Kwa mujibu wa CAG wanawasilisha vielelezo hata baada ya kufanya wizi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nape Nnauye, unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.


SPIKA: Haya, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo. Mheshimiwa Nape subiri kidogo, inaonekana kuna Kanuni imevunjwa hapa.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nimesoma ripoti tatu, zina kurasa 889. Mheshimiwa amesema hapo kwamba, CAG amesema kwamba, hati safi zimepatikana baada ya wizi kuanza. Naomba kiti chako kielekeze kama anaweza akatuonesha hiyo sehemu kwenye CAG Report. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kitila Mkumbo, kwa sababu hapa ni jambo la Kanuni kuvunjwa, kwa hiyo Mbunge anasema uongo? Ili tujue tunajielekeza kwenye Kanuni gani, nitoe utaratibu.

WAZIRI WA MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ni uongo kwa sababu hicho kitu kwenye ripoti hakipo. Atuthibitishie na napata Kanuni sasa hivi nitai-cite Kanuni hapa. Naitafuta.

SPIKA: Hakuna neno. Waheshimiwa Wabunge tutaenda tutaenda. Hakuna neno. (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kwa Mujibu wa Kanuni ya 71 ya …

SPIKA: Hakuna neno. Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri amesema amesimama hapo kwa mujibu wa Kanuni ya 71 ambayo inazungumza kuhusu mambo yasiyoruhusiwa Bungeni. Kwa sababu ametaja neno uongo, nadhani kuna Kanuni inayohusu hapo. Kanuni ya 70 ndiyo inahusu uongo na hakuna neno. Nia tu nataka kutengeneza. Hakuna shida, tunataka kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, hakuna shida mtu akitaja 71 wakati ni 70. (Makofi/Kicheko)

Waheshimiwa tusikilizane, nimesimama.

Kanuni ya 70 inazungumza kuhusu kutokusema uongo na inaruhusu Mheshimiwa Mbunge kusimama mahali pake na kusema Kuhusu Utaratibu. Fasili ya tatu inasema Mbunge huyo baada ya kuruhusiwa ataeleza hayo maelezo ambayo yanaeleza uwongo unatokea wapi. Kwa ujumla ukiisoma Kanuni hii inataka yule aliyesema kwamba Mbunge mwingine anasema uongo ndiye athibitishe, huo uongo wa huyo Mbunge. (Makofi)

Sasa kwa muktadha huo, Mheshimiwa Kitila Mkumbo, alivyosimama hapo ameeleza kwamba katika taarifa zilizopo yeye hajaliona hilo jambo ambalo Mbunge amelisema; kwa maana ya kwamba wale wezi wamejifunza utaratibu mzuri wa kutoa taarifa na kwa hivyo wanapata hati safi. Katika zile halmashauri ambazo zimepata hati safi, zipo ngapi Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC? Ni hapa tu, unaruhusiwa kusimama na mimi nikiwa nimesimama. (Kicheko)

MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA LAAC: Mheshimiwa Spika, kumi na tatu zimepata hati zenye shaka na 170 ndiyo zimepata hati safi.

SPIKA: 170 zimepata hati?
MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, hati safi. Zenye shaka ni 13, moja chafu.

SPIKA: twende kwenye safi 170. Kwa maelezo na kwa michango tuliyoanza nayo Alhamisi, jana na leo, kwa namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge, wameeleza halmashauri zao zilivyo na changamoto; hizi hati 170 ni hati safi; na huu unaoitwa wizi, ubadhirifu umetokea kwenye hizo halmashauri. (Makofi)

Hizi hati safi zimetolewa kwa muktadha upi; ni kwa maana ya kwamba zinakaguliwa kwa utaratibu ule wa kawaida na kwa utaratibu ule wa kawaida wamefuata taratibu za upelekaji wa taarifa kwa CAG. Kama hivyo ndivyo kwa takwimu hizi, pengine maneno sasa kwa sababu taarifa muda ni mfupi, kwa takwimu hizi zilizopo katika taarifa hii ya kamati na taarifa ya CAG ni dhahiri hawa wabadhirifu wamejifunza namna nzuri ya kutoa taarifa. (Makofi)

Kwa sababu kama hivyo sivyo, mimi nitachukua mfano mmoja tu na unaotokana na michango ya hapa ndani. Mfano mmoja tu, ukurasa wa 106 wa taarifa ya Kamati ya LAAC, halmashauri namba 16, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina hati inayoridhisha. Hapa tumemsikia Mheshimiwa Mbunge wa Bunda, akieleza taarifa ya CAG ilivyoitaja Bunda kwenye mambo mengi ambayo hayaendi sawa sawa. Wametajwa kwenye kuzima POS na m kwenye mambo mengine mengi tu ambayo ameyaorodhesha hapa. Kwa hiyo mazingira hayo Mheshimiwa Kitila Mkumbo, inaniwia vigumu kusema Mheshimwa Mbunge kasema uwongo kwa sababu muktadha wa taarifa hii unaashiria hayo. (Makofi)

Waheshimiwa wabunge, sasa tunaendelea. Tuliishia ambapo Mheshimiwa Nape alikuwa anachangia, akapewa taarifa na Mheshimiwa Anatropia, katika kutoa zile taarifa ikaonekana kuna kanuni inavunjwa. Kwa hiyo hapa tulikuwa tunashuhurikia ile kanuni iliyovunjwa na kuhusu uwongo. Sasa tunarejea kwenye jambo lile la msingi ambalo ni kumuuliza Mheshimiwa Nape, kwa sababu ile hoja ya uwongo tumeshaimaliza kazi yake. Mheshimiwa Nape, unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Anatropia? (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme Waheshimiwa Wabunge, jambo tunaloliongea hapa linahusu maisha ya watu. Mimi ningewaomba sana, na hasa Waheshimiwa Wabunge wa chama change; nataka kuwaomba sana na kwa unyenyekevu mkubwa sana, kwamba tusiingize ushabiki kwenye jambo kubwa la maisha ya watu, nataka tutafute suluhisho. Mimi nimesema watu wanazungumza kwa uzalendo mkubwa sana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikia mwongozo wako, tunayo ripoti ya CAG, unless we are doubting kazi ya CAG. Ametupatia kwa numbers and Waheshimiwa wabunge, numbers speak clear. Maneno yanaweza kuongea kwa sauti kubwa sana, lakini numbers zinaongea very clear. Hoja yangu ilikuwa rahisi na ndiyo maana sipokei taarifa ya Mheshimiwa Mbunge na mimi namheshimu sana dada yangu. Hoja yangu ipo very clear kwamba taarifa hizi, zimekuwa zikitumika na Serikali kuboresha mambo ya usimamizi wa shughuli za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nikatoa mfano; hapa tumezungumza habari ya POS, habari yakukusanya makusanyo kwa TEHAMA, tulifikaje huko? Yalianzia kwenye ripoti za CAG kuonyesha kwamba kunakuvuja kwa mapato ya Serikali. Tukasema katika kushughulikia tuweke mifumo ishughulikie huo wizi, ishughulikie huko kuvuja kwa mapato. Sasa ripoti ipo mezani, ipo very clear unless we are doubting integrity na uwezo wa CAG kuripoti kazi zake ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hilo ndiyo hoja then hoja yangu haipo…

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, lakini kama tunamuona huyu CAG, namba zipo wazi CAG ametueleza ukweli…

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, upo mezani na ndiyo tunaoujadili. (Makofi)

SPIKA: Nani alikuwa anasema taaarifa?

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Naambiwa Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, alisimama kwanza.

TAARIFA

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nimesimama kumpa taarifa kaka yangu, kiongozi wangu, mtu mahiri sana, Mheshimiwa Waziri, kwamba katika mjadala huu hakuna ushabiki. Katika mjadala huu tunaoendelea nao tumeweka maslahi ya Taifa mbele, na tunajua kwamba tunashughulika na maisha ya watu, lakini vile vile tunashughulika kukomesha wizi na ubadhirifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili Bunge limejinasibisha kama chombo cha wananchi kushughulika na jambo hili. Kwa hiyo hatuna upande ilimladi mtu yeyote anashughulika na hili sisi tupo pamoja naye. (Makofi)

SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Nape Nnauye, unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, Kilumbe ni kaka yangu. Pia mimi nilikuwa kiongozi wake. Taarifa hii inamatatizo; (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: sawa. Mimi nina haki kama wabunge wengine. Mheshimiwa Spika, taarifa hii inamatatizo hapa, hivi kweli…

MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, hivi kweli sisi Waheshimiwa wabunge, nimesikia maneno hapa jana kuna Mheshimiwa Mbunge, anasema nchi inakuwa. Extent ya nchi kufa, miradi yote inaendelea hakuna mradi uliyosimama. Kuna fedha zipo majimboni kwetu mara 10, mara 15, mara 20, nchi inakufa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ndiyo maneno tunayomwambia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa nchi inakufa? (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nape.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, aah! Jamani tusifike huko, mimi nasema tujadilini wizi, tutafuteni solutioni. Tusiweke ushabiki. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nape.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Nape. Waheshimiwa wabunge, Mheshimiwa Nape kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Halima Mdee.

TAARIFA

MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, naomba ni nukuu ili taarifa yangu ichukuliwe kwa kunukuliwa kwake “Uchambuzi wa jumla wa kamati umebaini kuwa, idadi ya halmashauri zilizopata hati zinazoridhisha zimepungua kutoka 176 iliyotolewa katika mwaka wa fedha 2021 hadi halmashauri 170. Hati zenye shaka, idadi imeongezeka kutoka halmashauri nane mwaka 2020 mpaka halmashauri 13”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hati zinazoridhisha, zina-drop. Hati zenye shaka zinaongezeka, halafu tunasema mambo ni mazuri. (Makofi)

SPAKA: Sawa, ahsante sana.

MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba aseme ya kwake katika context yake, asiseme kwamba mambo ni mazuri wakati tumeambiwa hapo mambo ni mabaya. Tujadili mambo kwa ubaya wake… (Makofi)

SPAKA: Ahsante sana, umeleweka Mheshimiwa…

MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, tutafute suluhu.

SPAKA: Mheshimiwa Halima. Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, unaipokea taarifa hiyo?

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nilipoanza kuzungumza hii hoja ya utumiaji wa ripoti za CAG sikujikita kwenye mwaka mmoja. Mheshimiwa Halima, anatoa takwimu za mwaka mmoja. Na nimeanza nimesema nina bahati nimeziona taarifa nyingi sana nikiwa Katibu Mwenezi miaka sita, taarifa zote nimeziona. Nikiwa hapa Mbunge, tangu mwaka 2015 taarifa zote nimeziona. Ukichukua cumulatively ushauria ambao umekuwa unatolewa na CAG na Bunge, umekuwa unafanyiwa kazi ndi maana kuna-improvement, ndiyo hoja yangu niliyokuwa naisema hapa. (Makofi)

SPIKA: Sawa, ahsante Mheshimiwa…

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, na mimi sisemi kwamba mambo ni mazuri kabisa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Sekunde 30 malizia mchango.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kuna matatizo na Waheshimiwa wabunge wana haki ya kuwa wakali kwenye matatizo hayo. Hoja yangu matatizo hayo hayajatupeleka kwenye extent ya nchi kufa, siyo sawa. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa…

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, matatizo yapo ndiyo kwamba eti…

SPIKA: Muda wako umekwisha, ahsante sana.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, leo tunafika mahali kwa hali ilivyo kazi iliyofanyika na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnasema nchi inakufa serious?
SPIKA: Mheshimiwa Nape, muda wako umekwisha, ahsante sana. (Makofi)