Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia taarifa ambazo zimewasilishwa na Kamati zetu za Kudumu za Bunge kuhusiana na Ripoti ya CAG.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutumia nafasi hii, kabla sijachangia naomba kuwapa pole wananchi wa Jimbo langu, kaya 30 ambao wametaifishiwa mifugo yao 900 na TANAPA wiki hii. Inafadhaisha, yanayotokea sasa hivi hapa, inaonesha kuna watu hawatekelezi majukumu yao vizuri. Kwa sababu, kwa suala hili la hawa wananchi kutaifishiwa mifugo ninaamini kwamba walipelekwa mahakamani wakasema hawana mwenyewe na wala hawana wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kiuhalisia hili suala lilikuwa linajulikana. Kwa hiyo, tutoe tahadhari kwamba Serikali yetu isije ikawa ni sehemu ya kuwafanya wananchi wawe maskini. Kwa sababu, kutaifisha mifugo 900 kaya 30 maana yake wale wananchi wameshakuwa fukara. Sijui tutawaingiza kwenye mfumo wa TASAF au tutafanyaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa ninatafakari kuhusiana na Ripoti ya CAG…

SPIKA: Mheshimiwa Oleshangai ngoja hili Bunge tulielekeze vizuri kwenye kufanya maamuzi. Jambo hili unalolizungumza sasa ni sehemu ya Taarifa ya CAG au ni la kwako kama Mbunge kwa sababu linawagusa wananchi?

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, ni la kwangu kama Mbunge kwa sababu linawagusa wananchi wangu.

SPIKA: Sawa, sasa ngoja tuliweke vizuri. Kwa sasa, kwa sababu umesimama kuchangia hoja iliyoko mezani, ikiwa kuna jambo ambalo unataka kulifikisha ili Serikali ilifanyie kazi, inabidi utumie kanuni nyingine ili Taarifa zetu za Bunge zikae vizuri. Kwa sababu, kwenye hoja hii, hoja ni ya Kamati. Kwa hiyo, hata uhitimishaji watakuja kuhitimisha Wenyeviti ambao hawana uwezo wa kulizungumzia hilo. Ili likae vizuri, utakapomaliza mchango wako unaohusu Taarifa ya CAG baadaye tukishamaliza hayo tafuta kanuni ambayo itakufanya uliseme hilo jambo la wananchi wako.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru na ninaomba kuendelea kuchangia Ripoti ya CAG. Nilikuwa natafakari kuhusiana na yanayotokea. Kwenye taarifa zetu kuhusiana na Ripoti ya CAG. CAG amepewa majukumu, ukijaribu kusoma ni kwamba anaitwa ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Ninaamini kwamba CAG amekuwa akitekeleza jukumu moja la ukaguzi lakini udhibiti imekuwa labda sio sehemu ya kazi zake.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye Mfuko wa NHIF tumekuwa tukilalamika kwamba mfuko hauwezi kusaidia kuhudumia wananchi ambao wanaenda hospitali kwa ajili ya kutibiwa, cha kushangaza ni kwamba, kuna fedha ambazo watumishi wa NHIF wamekopeshana zaidi ya shilingi bilioni 41. Hizi fedha wamekopeshana wakati sheria inawaruhusu kukopeshana kutumia mfuko wa kuzungusha au revolving funds, lakini wao wamekuwa wakikopeshana fedha ambazo zinatokana na michango ya wanachama wa NHIF.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ninataka kulichangia kuhusiana na NHIF, Waziri wa Afya kila siku hapa amekuwa akisema mfuko wa NHIF unakufa. Lazima ufe, kwa sababu, Serikali yenyewe inadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 228 na hamtaki kulipa, Serikali haitaki kulipa fedha hizo kwa mfuko wa NHIF kwa ajili ya kuwahudumia wanachama wake na leo hii tumeondoa ile Toto Afya Card lakini Serikali ingeweza kulipa fedha nyingine ambazo zingeweza kuwahudumia watoto wa maskini ambao hawapati huduma.

Mheshimiwa Spika, suala lingine. Kuna ununuzi wa vifaa ambavyo vilifanyika kupitia bohari ya dawa. Kuna Kampuni ya Alhandasia ambayo walipewa kandarasi ya kununua vifaa aina 75 kwa shilingi bilioni 3 lakini mpaka kufikia tarehe 30 Oktoba, 2021 kampuni hiyo imeonekana kwamba ni kampuni hewa. Ukiwauliza watu wa bohari ya dawa wanasema tuliwatafuta online tukalipa fedha online na fedha zikapotea na yule mtu ajulikani alipo.

Mheshimiwa Spika, tunashangaa. Ni mtumishi gani wa Serikali ambaye unaweza ukalipa fedha online halafu ukasema huyo mtu hayupo na namba ya account baada ya kulipa ikatoweka. Are we serious? Kwa sababu, leo unalipa fedha halafu unasema baada ya kulipa, halafu mtu anatoweka. Anajitokeza mtu mwingine anaitwa EPICO anasema mimi nitaleta hivyo vifaa pamoja na zile za Alhandasia. Maana yake inawezekana kuna ushirika fulani ambao unatengenezwa halafu baadaye tunasema hatumjui mtu, kumbe huyo EPICO ndiyo huyo huyo tena amebadilika jina alikuwa anaitwa Alhandasia sasa hivi anaitwa EPICO. Kwa nini sasa yeye akubali kubeba gharama za yule mtu ambaye ametoweka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini kila mtu akiweza kutimiza wajibu wake tunaweza ku-control haya matatizo yanayotokea. Hivi kweli mtu anasema alitoweka, wewe ulimlipaje mtu kama haumjui. Bahati mbaya au nzuri walimwandikia Balozi wa Misri, Balozi wetu. Akawaambia huyu mtu sisi hatumfahamu, baadaye wao wakaamua kulipa. Halafu hawa watu bado wanatembea mitaani. Huku tunakimbizana na machinga kuwanyanganya shilingi elfu 20 wakati huku tunapoteza shilingi bilioni 5. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadaye huyu mwingine anaitwa EPICO anajitokeza anasema ataleta hivyo vifaa aongezewe shilingi bilioni 10 ili alete zile za shilingi bilioni 3 lakini sharti lake alipwe shilingi bilioni 10. Imagine!

Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba, tuna tatizo ambalo tusipoamua kulitibu kama nchi tutaendelea kuwaumiza Watanzania. Leo tukifikiria shilingi bilioni 3 tutajenga vituo vya afya vingapi? Lakini zimepotea. Nimeangalia ripoti… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa dakika moja malizia. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la halmashauri zetu, halmashauri zetu kuna tatizo moja kubwa la ukusanyaji wa mapato. Niishauri TAMISEMI, kule chini ukijaribu kuangalia ukusanyaji wa mapato kuna POS machine lakini zinapoletwa kwenye Taarifa ya CAG, kuna POS machine ambazo hazifanyi kazi moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, Mheshimwa Waziri itabidi uwaagize Wakurugenzi, zote zipitiwe zile ambazo hazifanyi kazi tuondoe hizo quarries. Mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, unakuta kuna POS Machine, tumewapa wale watu wa mitaani waingize au wakusannye ushuru. Badala ya kuandika shilingi elfu nane unakuta ameandika shilingi milioni 8. Halafu ndiyo hizo CAG anaenda kusema ni fedha ambazo hazijakusanywa. Kuna POS errors ambazo watu wanaingiza fedha. Mfano, mbuzi mmoja ni shilingi 2500 lakini unakuta kwenye POS Machine mtu anaandika vibaya, anaandika elfu 25 kufuta hawezi mpaka atoke mtu makao makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwenye halmashauri zetu kuna vitu vingine ambavyo vinahitaji hekima pamoja na ku-act haraka ili tuweze kuondoa hizi querries ambazo hazina maana. Kwenye halmashauri zetu, unakuta mtu anataka aandike shilingi elfu 80 anaandika shilingi laki 8. Hawezi kurekebisha mpaka atoke mtu makao makuu. Hiyo kama Serikali tunahitajika kuchukua hatua pamoja na kuwatafuta wataalamu wa kukusanya mapato wengine kule chini.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru. (Makofi)