Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza naanza kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza mambo ambayo tuliyapendekeza kwenye Mpango uliopita. Pia, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kuwasilisha Mpango wao nasi tuweze kuongeza mawazo yetu waone kama vile yanafaa kwa ajili ya kusaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea katika maeneno mawili. Chanzo cha mapato, ni namna gani ambavyo tunaweza tukatumia mawazo haya yakatusaida kama Taifa kwa ajili ya kuongeza mapato. Jambo la kwanza, najaribu kuangalia yale maeneo ambayo kutoka kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi hususani kwenye upande wa vijana, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inasema: “kutengeneza ajira zisizopungua milioni nane katika Sekta Rasmi na isiyokuwa rasmi kwa vijana.” Chanzo kimoja ambacho nitaongelea ndani ya nchi yetu ni pamoja na huduma za forodha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Huduma nyingi za kiforodha mfano Tunduma, Namanga, Holili, Kasumulu na maeneo mengine ambapo kuna Vituo vya Forodha, kumeonesha kuvutia sana wananchi wengi kwenda kufanya biashara maeneo hayo. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwamba 2021 ulikuja pale, ukatembelea kwenye lile eneo, tunaomba tupate Kituo cha Forodha. Licha tu ya kwamba itasaidia wana-Momba lakini vituo vingi vya Forodha vimeonekana kuwa chachu ya mapato kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tu mfano wa Tunduma, angalia mapato ambayo yanapatikana pale. Pia kwenye hivi vituo vya Forodha, licha tu ya kupata mapato, hata katika hali ya ulinzi, tunaongeza ulinzi kwenye nchi yetu kwa sababu tunakuwa tunaendelea kuikagua vizuri ile mipaka na kuzuia hata mambo ya magendo. Nakuomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, uone tena, ukae na timu yako ya TRA mpitie lile eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea hapo hapo kwenye Kituo cha Forodha Tunduma, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Hivi mnaonaje kwenda kuyapunguza yale magari yote ambayo yamejaza msongamano pale Tunduma na kusababisha jam zisizokuwa za lazima? Kwa nini baadhi ya magari yasivutwe kwenda mpaka kule kwa Kakozi? Si ni matumizi mabaya ya barabara? Barabara iko wazi tu, nyeupe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa tunasubiri huo mfumo wa njia nne, basi tunaweza tukayavuta yale magari tukapunguza jam Tunduma ili watu wakaendelea kuvusha magari yao vizuri bila kuathiri shughuli nyingine. Mji mdogo lakini unaweza ukatumia zaidi ya nusu saa kwa ajili ya kupita kilometa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuongelea chanzo cha mapato ambacho kinaweza kikasaidia vijana, ni kwenye eneo la teknolojia. Wakati nasoma hotuba ya Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwenye ukarasa wake wa 51 pamoja na ukurasa wa 117 kwenye kipengele cha 3.3.2.2.1, nikajaribu kuangalia namna ambavyo yeye ameielezea teknolojia. Katika ulimwengu tulionao, matajiri duniani, kwa mfano nikiongelea nchi ya USA wana mabilionea 735. China wana mabilionea 607 na nchi nyingine huko duniani. Hata hivyo, matajiri wengi hawa wanatokana na utajiri ambao unatokana na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili nimeandaa andiko fupi kwa kuangalia mwaka 2021 ambao toka nimeanza kuchangia mambo ya teknolojia mwaka 2022, naomba Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo apate pamoja na wewe mwenyewe upitie uone. Nimekuja na orodha ya matajiri duniani kama kumi hivi ambapo utaona utajiri wao wote mabilionea hawa unatokana na mambo ya teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwasome kidogo. Tajiri wa kwanza duniani mwaka huu wa 2023 ni Elon Musk ambaye ana utajiri wa dola za Kimarekani bilioni 240 ambao unatokana na kufanya biashara za teknolojia. Ana Kampuni ya SpaceX pamoja na Tesla. Tajiri wa pili ni Bernard Arnault lakini yeye anafanya mambo ya fashion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tajiri wa tatu ni, Jeff Bezos ambaye yeye utajiri wake ni dola za kimarekani bilioni 154, ambaye ndiye mmiliki wa Taasisi ya Amazon, anafanya biashara za mtandaoni, tajiri wa nne ni Larry Ellison ambaye utajiri wake ni dola za kimarekani bilioni 146 naye ni mmiliki wa Kampuni ya Oracle Cooperation ni mambo ya teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tajiri wa tano kwa mwaka huu wa 2023 …

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sichalwe pamoja na kuwajua hao matajiri, ungelisaidia Bunge utajiri wao walioupata kwenye teknolojia na walitumia mbinu zipi ili work the talks ambapo sasa hao matajiri hawasaidii kitu kama huelezi wamefanya nini ili Waziri aweze kuelewa, sawa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Halafu sasa hao matajiri waache, tutaambizana baadaye jioni.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nataka kusema nini hapa; orodha ya matajiri wote ambao tunawaona duniani hawa wote wametokana na kuwekeza kwenye teknolojia. Kwenye teknolojia ipi? Mapinduzi manne viwanda (forth industrial revolution) kwenye mambo ya blockchain technology, kwenye mambo ya digital currencies na kwenye mambo ya artificial intelligence. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja ya Serikali yetu kutafuta mazingira mazuri na wezeshi ya kuruhusu vijana wa kitanzania kuonesha uwezo wao wa kiteknolojia ili na wao tuweze kupata matajiri wengi kama hawa duniani. Miundombinu yetu mingi iliyopo hapa Tanzania, hai-support vijana wengi kwenye kujielekeza katika teknolojia. Pia hakuna mazingira wezeshi ambayo Serikali imewawekea vijana ili waweze kuonesha uwezo wao na ubunifu wao ili tuweze kupata akina Elon Musk wengi kama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia watu wote hawa pamoja na kunikataza ndio hivyo hivyo. Mtu kama Mark Zuckerberg pamoja na mawazo yake ya ubunifu lakini unaona kabisa Serikali yao imewatengenezea mazingira ambayo wana-support ubunifu. Yeye ndie ambaye ndio mmiliki wa Mtandao wa Facebook, Instagram, WhatsApp, angalia mazingira gani ambayo wanapata, angalia ni mapokeo gani ambayo Serikali ina-support teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 tulipochangia sana kwenye mambo ya blockchain technology Mheshimiwa Rais ameshawahi kutoka hadharani na kuonesha ni namna gani ambavyo wataalam wanapaswa ku-support.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi kutaka kujua kwa nini nchi yetu wakati mwingine, inatukwamisha kwenye ku-support mambo ya teknolojia, angalia mpaka sasa hivi tulishachangia sana hapa bungeni kuhusiana na kuruhusu Mfumo PayPal ili tuweze kulipa malipo ya PayPal kwenda nje ya nchi, lakini unaweza kukuta watanzania wengi ambao wanafanya biashara ili waweze kulipa kwa njia ya PayPal wao wanaruhusiwa kulipa lakini wao hawaruhisiwi kulipwa. Kwa mazingira kama hayo yanaonesha dhahiri kabisa kwamba nchi yetu bado haijatu-support hususan vijana kwenye mambo ya teknolojia. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mazigira wezeshi ya ku- support teknolojia yawezeshwe ili tuweze kupata matajiri wengi kama hawa duniani, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Sasa hayo ndio ilitakiwa uyaseme, sio kutaja majina ya matajiri.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa ni kuwa-motivate Mawaziri pamoja na wewe mwenyewe.