Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali nzima kwa kazi nzuri ambayo wanaendela kufanya. Namshukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Geita Mjini na wananchi wa Mkoa wa Geita, kama wiki moja au mbili zilizopita tulikuwa na mkutano mkubwa wa wachimbaji Dodoma, ambapo kwa sehemu kubwa wachimbaji walitoka Mkoa wa Geita. Tunashukuru kwa kukabidhi vifaa vya teknolojia ya madini, tunamshukuru sana na wananchi wanasema sasa wameingia kazini rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha kwa taarifa yao nzuri ambayo nimeipitia. Kama ambavyo malengo au shabaha ya mpango wenyewe imezungumza ni kuongeza thamani kwenye mazao tunayouza nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuishauri Serikali, tunayo Sheria kwenye madini ambayo imeweka ulazima wa kuongeza thamani madini ya dhahabu kabla ya kuyauza nje. Kwa kufanya hivyo, Serikali ilitoa leseni za kujenga gold refinery na zimejengwa gold refinery nyingi lakini bado nashangaa ni kwa nini bado kuna kusita sita kwenye kutumia sheria hiyo kuhakikisha kwamba dhahabu yote inayouzwa nje imekuwa refined.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kuna sababu kubwa ya kulazimisha hivyo? Kwanza; tunapeleka dhahabu nje ambayo tayari itakuwa branded kama dhahabu yetu; Pili, tunaiongezea thamani na pia tunazifanya hizi refinery ambazo zimejengwa kwa gharama kubwa kufanya kazi iliyokusudiwa. Kwa hiyo, lengo hapa ni tusimamie hii sheria tuliyoiweka, tuweke malengo ya kuongeza thamani ya madini haya, tuhakikishe kwamba soko tunalolipata huko nje linatambua kwamba dhahabu hii inatoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapoondoka Tanzania raw gold kwenda nje kama South Africa au Uarabuni wanapoifanyia refinery wanai-brand wao kule kwa hiyo matokeo yake inapoteza uasili lakini sisi tunapoteza thamani yetu kwenye eneo hilo. Naishukuru sana Serikali pia kwa mchakato ambao imetoa ahadi kwamba inauanzisha ambao sasa inajipanga kufanya high resolution airborne geophysical survey ambayo itatusaidia kuijua vizuri nchi hii na kuangalia maeneo mahsusi ambayo yana madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pamoja na mbwembwe zote tulizonazo eneo ambalo limefanyiwa utafiti ni kama asilimia 16. Tukiongeza, tukijielekeza kwenye kukamilisha utafiti kwenye eneo hili makato yanayotokana na madini sehemu kubwa yata-double yatakuwa mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali katika maeneo ya wachimbaji kuna vituo vya mfano vimewekwa viko vitatu. Kimoja kiko Rubete, kingine Rwamgasa ambapo wamejenga CIP. CIP hizi zingejengwa hata 30 au 50 Tanzania ili ziwasaidie wachimbaji wadogo kumaliza dhahabu kwenye mchanga. Sasa hivi teknolojia inayotumika inaacha dhahabu nyingi sana kwenye mchanga kwa sababu wanatumia plant na hizo plant ni lazima uje urudie kuchukua ule mchanga kuuingiza kwenye plant.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali kwa kuwa dhahabu inatuingizia fedha nyingi za kigeni na kwa kuwa, tayari tumegundua asilimia 40 ya dhahabu Tanzania inatokana na wachimbaji wadogo wadogo, isione aibu kuwekeza, tuwekeze ili tuweze kupata pesa nyingi zaidi kutoka kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, mwaka huu pia nilichangia, kwenye mchango wangu nilizungumzia habari ya kuongeza pesa za mauzo ya nje kutoka kwenye mazao. Sasa hivi tunapata pesa nyingi sana kutoka kwenye avocado na hii ilikuja yenyewe tukapata pesa nyingi. Tanzania kuna maeneo yanajipambanua kwa kulima migomba, kuna maeneo yanajipambanua kwa kulima nanasi. Nilizungumza duniani kuna export ya nanasi inayokadiriwa kufikia dola bilioni 30. Nanasi tulizonazo Tanzania ni kama vile madawa ya kienyeji kwa sababu huwezi kuzi-export. Nilisema tukiboresha eneo hili peke yake, Costa Rica wanapata dola bilioni moja kwa kuuza nanasi, Philippines wanapata dola bilioni 300 kwa kuuza nanasi, Nigeria wanapata zaidi ya dola milioni 100 kwa kuuza nanasi. Sisi hatuuzi nanasi lakini wakulima wa nanasi wapo, tunachotakiwa hapa ni kupata mbegu sahihi ambayo tunaweza kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kuwa wakulima wa nanasi wapo na tuna BBT inaendelea ni kuwapelekea teknolojia, kuwapelekea mbegu bora na kuwatafutia soko kama tulivyotafuta soko la avocado tukaanza kuuza nje tukapata mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nataka kuzungumzia, kwanza naipongeza Serikali kwa kuonesha itapeleka trilioni 15.3 kwenye maendeleo sawa sawa na asilimia 33 nakupongeza sana. Juzi wakati tunajadili taarifa ya CAG ulitokea mjadala wa zaidi ya shilingi trilioni 200 ambazo zimeonekana zimekwenda nje kinyume cha utaratibu. Mawaziri wote wawili wa Fedha na wa Mipango walikuwa wanapinga na mimi nakubaliana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye repoti utakutana na hizo dola bilioni 140 kama pato la nchi lakini kwa mfumo ulivyo duniani Mheshimiwa Waziri wa Mipango ukiangalia kwenye list financial flows duniani pesa ambayo inavuja ni nyingi kuliko pesa inayokusanywa. Pesa tunayoizungumzia hapa ni pesa ambayo haikupita kwenye vitabu vyako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili hii pesa shillingi trilioni 15.3 ambayo ni sawa na asilimia 33 iweze kufanya kazi yake vizuri lazima tujue kwamba corruption ime- imejizalisha, wamebadili mbinu. Corruption sasa hivi inakuwa exported, inakuwa exported kutokea kwenye contract na kutokea kwenye kazi ambazo watu wanazitengeneza leo

MWENYEKITI: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Kanyasu.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuwe na mpango madhubuti wa ku-deal na aina mpya ya rushwa ambayo inaweza, pesa zote hizi zisitusaidie kuona tunachokifanya kutokana na ukweli kwamba kuna watu tayari watakuwa wamejiandaa namna ya kuichukua. Nakushukuru sana. (Makofi)