Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa muda wa kuchangia hoja ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Spika, naomba kwenye Bunge hili tumtangaze Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu kuwa Spika wa viwango vinavyozingatia kanuni, sheria na utaratibu wa kuliendesha Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaiongoza nchi yetu kwa ufanisi mkubwa. Nataka niseme bila kuficha, nimekuwa Mbunge hapa mwaka wa 12, nimesikia bajeti nyingi hapa, lakini bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameitendea haki kwa kuisoma, kuihusianisha kabisa na Mkuu wa Nchi, kwamba yeye ametumwa tu kuja kufanya, lakini mwenye kazi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naweza kusema bila kuficha, ni bajeti pekee ambayo imemtaja Mheshimiwa Rais kwa wingi sana kuliko bajeti zote zilizosomwa na Mawaziri hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya mambo tuyazungumze katika ukubwa na upana. Hapa tunazungumzia Mfuko Mkuu wa Serikali, tunazungumzia namna gani tutaishauri Serikali kwanza kukusanya mapato yaingie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali halafu baadaye namna ambavyo tutanufaika nayo kwenye Majimbo na Watanzania namna gani watafaidi baada ya kuwa yamekusanywa.

Mheshimiwa Spika, sasa tunapozungumzia vyanzo vya mapato, tuwe wakweli, tunahitaji kuishauri Serikali kukusanya kodi kwa uhakika, lakini vilevile kuwa na nidhamu ya kutunza fedha zinapoingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ili kesho na keshokutwa zije zirudi tena kuwasaidia wananchi.

Mheshimiwa Spika, niseme, viongozi wengi sana wa Afrika kumbe wakati mwingine huwa wanabadilishwa na watu. Nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Samia tunayemsifu leo kuwa mpole na mtulivu, sina hakika tukiendelea na tabia hii kama itafika 2030 akiwa hivyo. Tunaweza tukajikuta sisi wenyewe tumembadilisha. Rais anaweza kuwa mpole, mtulivu anayefuata sheria lakini vitendo vya baadhi yetu vikambadili akawa mkali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania tumeshuhudia watu wakihama baadhi ya maeneo. Tumeshuhudia ndugu zangu Wasukuma, wafugaji wakihamishwa kutoka bonde la maji pale kuelekea Mtwara, wote tulikuwepo na ni watu wazima; watu walikufa katika safari ile na mifugo ilikufa. Mtu alimnunulia mwanaye raba mpya za kutembelea, lakini baada ya kufika Tunduru zilikuwa zimechanika, zimechakaa na miguu imetoboka, anatembea kijana kutoka Mbeya kwenda Tunduru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Rais anahamisha watu kwa mabasi, ng’ombe wanapanda malori, bado tusiseme jamani tuna Rais mwenye huruma na anayependa watu? Haiwezekani. Rais hili jambo amefanya ni la kibinaadam la kiutu sana. Hakuna katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watu walioweza kuhama kwa raha kama watu wanaohamishwa kutoka Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi tukubaliane, hapa kwenye jengo la Bunge ikilipuka volcano, kuna Mbunge anabaki hapa? Ikitokea hatari hapa wote tunatoka; huwezi sheria ilisema hapa ndiyo jengo la Bunge, hakuna! Siku moja king’ora kililia tu hapa, Waziri Mkuu alikuwa ndio wa kwanza kutoka hapa anakimbia. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukubaliane kwamba tunataka mapato yaongezeke kwenye mfuko wa nchi. Haya mapato mengine yanatoka kwenye utalii, mengine yanatoka kwenye kilimo. Kwa hiyo, ni lazima tukubali tunapotaka kuboresha utalii, tunaboresha mapato yaongeze kwenye mfuko wa Taifa. Kumbe Rais anaongoza Taifa hili kutoka wapi hizo fedha? Tunapotaka maendeleo, huku tunasema Rais asikope, huku tunasema watalii wasije, sasa huyu Rais ataongoza Taifa kutoka wapi? Fedha atazitoa wapi?

Mheshimiwa Spika, fedha nyingine ni za utalii, lazima watalii waje kwenye nchi yetu. Tumeona pale Wabunge wengi sana wametembelea China. Umeona kwenye great wall pale, Mchina hataki mtu asogee pale! Bahati mbaya sana nchi hatuwezi kuiongeza ukubwa. Nchi yetu ndiyo hii hii tumepewa, upande huu tunapakana na Msumbiji, huku Kenya, huwezi kuiongeza ukubwa. Kwa hiyo, lazima rasilimali tuliyonayo, hiyo hiyo itutoshe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upendeleo mwingine uliotoka hata nyumbani kwako pale unapoishi, mimi nimefika, wewe unakaa sehemu ina heka moja ile! Ila watu waliohamishwa Ngorongoro wamepewa heka tatu, wakati wewe unakaa pale padogo kabisa! Watu wamepewa heka tatu. Ardhi ya heka tatu siyo ndogo mabwana. Kwa hiyo, tumsaidie Mheshimiwa Rais kwenye baadhi ya mambo, tumsaidie kuwashauri wale ambao hawaelewi, jamani eeh, maeneo haya ni hatarishi. Hapa tunataka kuimarisha utalii, watu waondoke kwa hiyari, sisi tusiwe vikwazo. Tunaoelewa tusiwe vikwazo, tuwaelimishe watu wetu namna gani ya kuweza kukubali ili Serikali iongeze mapato. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo yamezungumzwa hapa na Wabunge wameyazungumza kwa ufasaha sana kuhusu kuipongeza Serikali. Mimi naipongeza sana Serikali.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtaturu.

T A A R I F A

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba migodi yote ambayo unaiona inachimbwa madini nchi hii ni maeneo ambayo walikuwa wanaishi watu. Leo walipopewa leseni zikatolewa na Serikali, watu wale walihamishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 5 na Na. 6 ya mwaka 1999. Kwa hiyo, hata kinachofanyika Ngorongoro ni kufuatana na Sheria hiyo ya Ardhi ambayo inasema kwa mujibu wa Sheria. Kwa hiyo, naomba nimwongezee taarifa hiyo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde, unaipokea taarifa hiyo.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, huwa mtu hawezi kupokea kabla hujaka hapo, lazima achangie kwanza halafu ndio umpe taarifa. Maana sasa utakuwa unampa taarifa yule aliyekaa kule, utakuwa haumpi mwenye muda wake.

Ahsante sana, Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Halafu mimi leo nilikuwa nimejiandaa kuhutubia nchi, kwa hiyo, akina Mheshimiwa Tabasam hebu watulie kidogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa hapa suala la Wamachinga. Naishauri Serikali, tufanye utafiti. Hivi tunashindwa kufanya utafiti Wamachinga wetu wa Tanzania wanataka nini? Hebu tujipe muda wa kwenda kufanya utafiti, kuongea nao, Wamachinga wanachotaka pengine siyo kile ambacho sisi tunafanya. Wamachinga wanataka kukaa maeneo yenye mlundikano mwingi wa watu ili waweze kuuza biashara zao. Machinga hawahitaji jengo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wamachinga unaweza kuwajengea jengo nzuri na bado lisiwasaidie. Wanataka kukaa maeneo yenye watu wengi ili waweze kufanya biashara. Wamachinga hawahitaji vitu vingi ambavyo sisi tunafikiria.

Mheshimiwa Spika, lingine limezungumzwa hapa juu ya asilimia 10. Nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakaposimama anisaidie kidogo. Hivi alipokuwa anasema kipindi kile cha Mpango kwamba lengo la Serikali ni kuzalisha mabilionea wengi, ndiyo kwa hii asilimia tano au kuna mpango mwingine unakuja? Maana unapataje mabilionea wengi kwa utaratibu huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, tuone ni namna gani tutahamasisha kilimo. Ndugu zangu Wizara ya Kilimo imefanya kazi kubwa sana, watu wanalima sana, lakini Benki yetu ya Kilimo ni ngumu kukopa. Wakulima hawawezi kukopa. Hebu siku moja waite watu wa Benki ya Kilimo waje waeleze, utashangaa hawana mkulima hata mmoja wamemkopesha. Tulipeka wakulima wa zabibu 15 kutoka Mvumi wakawapokea, wakawapa maelezo mengi, lakini mwisho wa siku hawakupata hata senti tano. Kukopa kwenye Benki ya Kilimo ni ngumu, haiwezekani. Fedha wanazo, wanataja mabilioni lakini hakuna wanayemkopesha hata mtu mmoja. Hii Benki ni ya namna gani? Yaani bora mtu akakope CRDB atakopa alime lakini Benki ya Kilimo tuitake kila mwaka ituletee orodha ya majina ya wakulima waliokopa. Benki ina masharti magumu, haiwezi kumkopesha mtu wala kumsaidia mtu, lakini inaitwa Benki ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna Taasisi zina majina mazuri lakini hazimsaidii mtu, mtu wa chini imekuwa ngumu kukopa. Kwa hiyo, naomba sana Benki ya Kilimo tujipange vizuri, ushirika uimarishwe ili wakulima wawe na masoko. Tuwe na bei elekezi kwenye kila zao. Zabibu tuweke bei elekezi, korosho tuweke bei elekezi, tukija kwenye ufuta tuweke bei elekezi, tukija kwenye alizeti tuweke bei elekezi ili wakulima wetu wasipunjwe na kudhulimiwa.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka, ameelekeza vizuri namna nzuri ya kubana matumizi kwa wazazi wanaopeleka watoto wao kwenye Kidato cha Tano na cha Sita ili msamaha wa ada uliotolewa na Rais uweze kuwafaa watoto wetu. Vinginevyo mwakani tutaiomba Serikali irudishe ada, lakini iondoe michango, maana tunaona kwenye michango sasa ndiyo kuna tatizo kubwa kuliko kwenye ada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)