Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu muweza wa yote kwa kunipa nafasi ya kusimama jioni hii ndani ya Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi ambayo amelitendea Jimbo langu la Buchosa. Wananchi wa Buchosa wote kwa ujumla wao wanamshukuru Mheshimiwa Rais wao kwa barabara, maji, vituo vya afya na mambo mengi na kwa kweli tunasubiri utekelezaji kulipa fadhila zetu mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa leo nizungumze kile ambacho mimi naamini kwamba ni ukweli wangu. Nafahamu katika nchi yenye watu milioni 60 hatuwezi kufanana Mawazo yetu wakati wote. Tunatofautiana Mawazo, huyu atakuwa na Mawazo haya, mwingine na Mawazo yale. Kwa hiyo, nimepewa nafasi hii niweze kusema kile ambacho mimi naamini kitaweza kulisaidia Taifa langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkononi mwangu hapa nimeshika kitabu, kitabu hiki kinaitwa The Checklist Manifesto, How to Get Things Right. Kitabu hiki nilikisoma baada ya kuona kwamba sifanikiwi kwenye mambo mengi. Nilikuwa nikifanya mambo mengi lakini sipigi hatua na wala nikienda nasimama, nikienda nasimama nikalazimika kutafuta kitabu hiki nikakisoma. Baada ya kusoma kitabu hiki kimebadilisha kabisa maisha yangu na ninaamini kwamba kama nchi ya Tanzania ilivyo na ninawashauri Waheshimiwa Wabunge tutafute kitabu hiki tuweze kukisoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kama nchi inahitaji checklist manifesto, orodha ya mambo ambayo tunataka kuyafanya, wazee wetu mwaka 1961 walikuwa na Checklist Manifesto baada ya uhuru wakasema tunayo madini mengi ardhini lakini tunayatunza yatachimbwa na watoto wetu. Checklist Manifesto, wameyatunza madini yale tumekuja kuyachimba sisi. Kwa hiyo, leo tunapokaa hapa kukaa kuzungumza tunajadiliana checklist manifesto ya nchi yetu. Tunataka kufanya nini ndani ya miaka mitano, tunataka kufanya nini ndani ya miaka 20 checklist manifesto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila checklist manifesto hatuwezi ku-achieve kitu chochote. Binafsi sina mashaka yoyote na Mheshimiwa rafiki yangu Profesa Mkumbo kwa uwezo wake na kwa uzalendo wake, lakini lazima tupange nini tunataka tukifanye ndani ya muda gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa nikiamini ya kwamba tunayo kazi kubwa ya kubadilisha Taifa letu, lakini hatuwezi kubadilisha Taifa hili kwa wakati mmoja kwa mambo yote. Ningependa tujiulize leo tunataka Tanzania ya namna gani? Tunataka Tanzania yenye nini baada ya miaka 50 au miaka sitini ijayo? Hilo ndilo jambo la kujiuliza leo na tunaanza kufanya kazi moja baada ya nyingine kwenye checklist yetu tuna-tick kitu kimoja kimoja hatimaye tutimize vitu vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika checklist manifesto yetu sisi kama Watanzania tunataka kufanya nini ambacho watoto wetu watakaokuja watakuja kutusifia nacho, kwamba wazazi wetu walitangulia walifanya mambo haya ambayo yamekuwa na faida kwetu. Kwa hiyo, tumekutana hapa kujadili Mpango na Mpango nimeusona una mambo saba Mheshimiwa Mkumbo ameyaorodhesha pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza sisi kama Watanzania, sisi kama Wabunge, sisi kama watu waliotumwa tunataka ku-achieve kitu gani, tunataka tukumbukwe kwa jambo gani kama Bunge la Kumi na Mbili, tunataka Rais wetu wa Awamu hii ya Sita akumbukwe kwa kipi? Lazima tuwe na vipaumbele, hatuwezi kuyamaliza matatizo yote kwa wakati mmoja lazima tu-set priorities, kipi katika list yetu yote ile tunataka tuanze na kipi kifuate nini? Hilo ni jambo ambalo nimelikosa wakati nasoma Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji tukubaliane tunataka tuanze na barabara, tunataka tuanze na maji, tunataka tuanze na umeme ili mwisho wa siku tumalize kimoja baada ya kingine. Tukifanya hivyo tutamaliza mwisho wa siku itajulikana kwamba Rais wa Awamu ya Sita alishughulika na healthcare, Rais wa Awamu ya Saba alishughulika na barabara, Rais wa Awamu ya Nane alishughulika na maisha ya watu, hiyo ndiyo checklist manifesto, nimefanya hivyo maishani mwangu na maisha yangu yamebadilika. Tunayo sababu ya kuwa na checklist manifesto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimeusoma Mpango huu na nimeuelewa ya kwamba tunatakiwa tupange kipaumbele ninachokitafuta tunaanza na nini, kinafuata nini, tunakuja nini na tunamalizia na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo nataka kuliongelea hapa leo ni suala zima la mapato, ukurasa wa 21 pameandikwa tutaongeza mapato katika Mpango huu. Ninao ushauri wa kutoa, jambo pekee litakaloongeza mapato katika nchi ni kuboresha sekta zetu. Sekta zetu zimeshindwa kuchangia vya kutosha kwenye Pato la Taifa. Nchi hii ni Tajiri sana na wote tunafahamu lakini sekta zetu zimeshindwa kabisa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi huwa natoa mfano wa Venezuela nikiongea, Venezuela ni nchi tajiri sana ya mafuta namba moja Duniani inafuatiwa na Saudi Arabia lakini Venezuela ni nchi maskini kuliko Tanzania kwa sababu wameshindwa kutumia utajiri wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utajiri tuliopewa na Mungu tuutumie kuingiza fedha kwenye kapu la Taifa. Tukiingiza fedha kwenye kapu la Taifa nataka kukuhakikisha ya kwamba fedha zitakuwa nyingi na mwisho tutakuja kufikiri hata kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wetu. Tuwapunguzie VAT tukipinguza VAT lazima tutaongeza compliance ya wafanyabiashara waweze kulipa kodi kwa wingi, tukifanya hivyo tutakuwa tumesaidia sana nchi yetu, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwawezesha wazawa kiuchumi tuwawezesheni watu wetu washikilie uchumi wa nchi yao, nimeshaongea sana jambo hili mara nyingi, tuwapeni fursa Watanzania washiriki kwenye kukuza sekta binafsi tuwape mitaji, tuwape fursa mwisho wa siku wakipata fedha Watanzania wataitumia hapahapa nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee jambo la mwisho, National Innovation Fund, nimeshazungumza sana hapa, kwamba tuna vijana wengi wabunifu kwenye Taifa letu hawana mitaji, kama tuna Mfuko wa Kilimo, tuna Mfuko wa Filamu, tunayo Mifuko kadhaa tumeanzisha, tunashindwaje kuanzisha National Innovation Fund? Tuwasaidie wabunifu wetu wanatoka Chuo Kikuu hawana mitaji, watengeneze products.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina vijana wengi sana wabuni. Kuna mtu ametengeneza mashine za kusaga, mtu wa Darasa la Saba. Leo hii huko Iringa hawanunui mashine za Kichina wananua mashine za mtu huyo. Asaidiwe. National Innovation Fund itakopa fedha kutoka Global Innovation Fund. Global Innovation Fund, ni mfuko wa dunia ambao matajiri wakubwa kama akina Bill Gates wanapeleka fedha pale. Fedha hizi siyo mkopo, unaandika tu barua, unapeleka maombi, unapewa grant, na unawapa watu wako bila riba yoyote. Naamini tukianzisha National Innovation Fund, tutawasaidia sana vijana wetu wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Profesa Mkumbo, tumekuamini, tumekupatia jukumu la kutuendeshea mipango ya ychi yetu. Nataka nikwambie kaka, fanya jambo hili kwa uaminifu wako wote, kwa akili zako zote. Kwa sababu tumekupa responsibility na authority, mwisho wa siku tutaku-hold accountable. Tukifeli kama Taifa tutakushika mkono wewe. Bahati nzuri uliwashawahi kuwemo ndani halafu ukatoka, tumekurudisha tena, ukituharibia tutakutoa tena. Tukikutoa safari hii hatukurudishi tena. Kwa hiyo, nataka nikwambie Mheshimiwa Prof. Mkumbo, fanya kazi yako kwa akili zako zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa ushauri, Waziri aunde kitu kinachoitwa National Economic Planning Think Tank. Wako watu kwenye Taifa hili wana akili nyingi japo hawana certificate wala degree, wala Ph.D. Wachague hao watu wakuzunguke wawe wanakupa ushauri. Ninaamini kabisa ya kwamba ukifanya hivyo utapata mawazo mazuri sana kutoka kwa watu na utafanikiwa kwenye kazi yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni wizi. Sikuchangia kwenye Ripoti ya CAG, niliamua niache kwa sababu mara ya mwisho niliongea sana kuhusu wizi, lakini ngoja niligusie tena leo. Tunakusanya fedha lakini zinaibiwa. Kwenye Taifa hili ni kama kuna pepo wa wizi anazunguka. Kila mtu anataka aibe, lazima mpango huu unioneshe ya kwamba wizi utadhibitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa ni pen. Kwa watu wengi hii ni kalamu, lakini wasomi mtanisamehe, simaanishi wasomi wote. Kwa wasomi wengi hii siyo kalamu, hii SMG, hii AK-47

MBUNGE FULANI: Eeeh!

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Wanatumia hii kuiba fedha zetu. Ni lazima tuwathibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu utamke kwamba watu watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria tulizonazo. Tuna sheria tano tumetunga ndani ya Bunge hili; Sheria ya Fedha, Sheria ya TAKUKURU, Sheria ya Manunuzi, Sheria ya Watakatishaji Fedha, Sheria ya Uhujumu Uchumi na bado kuna Sheria ya Jinai. Tutumie sheria hizi kuwadhibiti watu wanaotuibia,

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikilize. Nataka nimwambie jambo, kuna bomu linakuja mbele. Ndani ya Wizara yake kuna Kitengo kinaitwa TSA kama sikosei, watu hawa wanaiba fedha, wanazituma kwenye halmashauri, halafu zinatoka kwenye halmashauri zinarudi kwao. Naomba kaka yangu ninakupenda, nenda kawadhibiti Watu wa TSA watakuingiza kwenye matatizo. Wanatuma pesa kwenye halmashauri… (Makofi)

MWENYEKITI: Kengele ya pili, ahsante.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)