Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii, lakini kabla ya yote naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku ya leo ambapo tunazungumzia mambo makubwa ya Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati kabisa, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ustawi na maendeleo ya nchi hii na pia hasa katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo tunaweza tukajisahau nini kinaendelea. Unapomwona Rais wa IPU ni matunda ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye ambaye amefanya kwa sasa tuwe na Rais huyo. Kwa hiyo, hiyo ni kazi kubwa, lakini pia ushawishi mkubwa alionao kwenye mataifa ya nje na jinsi ambavyo watu wanavyomheshimu yeye na kuliheshimu Taifa hili. Kwa kweli tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipowashukuru hawa Mawaziri wawili Dkt. Mwigulu Nchemba na Profesa Kitila Mkumbo. Wamefanya kazi kubwa na wametuletea Mpango mzuri sana ambao kwayo utaleta mambo makubwa na maendeleo makubwa kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hawa Mawaziri wawili tu, naomba nikiri wazi kwamba, nimekaa hapa kwa hii miaka mitatu, nimefuatilia Mawaziri wetu wanavyofanya kazi. Naomba niwashukuru hawa Mawaziri. Wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Hawa Mawaziri hawalali usingizi. Kuna watu nimewahi kuongea nao wananiambia wengine wanalala wanapigiwa simu mpaka usiku kwa ajili ya kunusuru Taifa hili ili liweze kuendelea. Waheshimiwa Mawaziri, watembee kifua mbele na wao ndiyo Askari wa Mwamvuli wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Pia, mambo yote yanayotendeka pamoja na watendaji wenu ninyi ndiyo mnaoyafanya. Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wote na mambo yote tunayoyazungumza hapa leo na hata tangu tumeanza, lengo letu kubwa ni ustawi wa jamii zetu na ustawi wa wananchi walioko kule chini. Vile vile, tunapoyafanya haya tunafanya mambo makubwa. Mheshimiwa Rais amejitolea moyo wake wote kwa dhati kuhakikisha mambo mengi yanakwenda kule chini na sasa tunatembea kifua mbele. Kila tunachokiomba kwa Mheshimiwa Rais kwa kweli kinafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo madogo sana ambayo ningeomba tushauriane vizuri sana tena kwa maneno ya staha sana na ndugu zetu wanaoshiriki katika mipango hii. Mambo hayo ni yale ambayo yanawahusu wananchi hasa kwenye sehemu zile ambazo niseme zinaleta kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kero ndogo ndogo ambazo kwa kweli wakati mwingine siyo za lazima. Kwa mfano, kule kwangu kuna malalamiko ya Wastaafu hasa wanajeshi. Wanaambiwa waende kuhakikisha taarifa zao, watoke vijijini kwa nauli zao waende Mbeya kilomita 118 na unapanda milima, kwenda na kurudi bila kula ni zaidi ya shilingi 25,000. Sasa hao watu walilitumikia Taifa, walipigana vita na tayari wamekwishazeeka. Hili la kuhakiki badala ya kuweka centers kwenye wilaya, wanawaambia waende mikoani ndiko wakahakiki taarifa zao. Ndiyo nasema hivi ni vitu ambavyo huwa vinahitaji kurekebishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la TASAF; TASAF imekuja kuwakomboa watu maskini, lakini kuna malalamiko makubwa sana huko kwamba, wanaopewa siyo wale ambao walistahili na mfumo unaotumika ni mfumo wa kisomi. Sasa, wale wazee wetu walioko huko chini ukiwaletea mfumo wa kisomi unakuwa ni shida. Maswali wanayoulizwa na majibu yanayoingia kwenye Computer ili computer ichague, hayaendani na uhalisia. Mtu mwingine hata umri wake haujui, hata kwamba anapata shilingi ngapi kwa siku hajui. Sasa, unapomwingiza kwenye computer ndiyo achague kwa kweli inakuwa ni ngumu. Ningeomba ifanyike kama ilivyokuwa ikifanyika zamani. Wananchi wenyewe ndiyo watoe majina ya hao watu. Pia wakitoa kusiwe na haja ya mfumo kuchambua tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Serikali kulipa madeni ya wakandarasi lakini na haya madeni madogo madogo yanayohusu wananchi. Kwa mfano, kuna sehemu zinapitishwa barabara, mpaka mnakwenda mnagombana na wananchi kwa kitu ambacho hakina maana ambapo tayari tulikuwa tumekwishapanga barabara ipite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano mmoja kwenye barabara ya Ibanda – Itungi port. Tunaishukuru sana Serikali inajenga barabara ile lakini tangu wananchi wake wamefanyiwa assessment mpaka leo hawajalipwa fedha zao na barabara inaendelea kujengwa. Kwa hiyo, vitu kama hivi huwa vinawaudhi sana wananchi, ningeomba Serikali inapopanga mipango, ipange na mipango ambayo itakuwa inaondoa hizo kero ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kero kubwa kubwa pia. Leo tunapozungumza kulikuwa kuna kero za wananchi kupigwa, wananchi kufanywa nini na TANAPA. Mimi ni shahidi, nilibahatika kuwa kwenye timu ya kamapeni kule Mbarali. Wakati wa ufungaji wa kampeni kule Mbarali pamoja na kata nane nilizozunguka, nilipangiwa Kata ya Madibila kwenye Vijiji vya Ifuchilo na Ukwavila. Hata hivyo tulipowambia Mheshimiwa Rais na Makamu kupitia Chama Cha Mapinduzi wamesema, wananchi sasa wataendelea kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walinivuta vijana wachache walikuwa kama mia moja hivi pembeni hivi baada ya mkutano, wakaniambia Mheshimiwa Mbunge tumekubaliana na wewe, sisi kura kwa CCM tutatoa lakini suala la kwamba tuende tukalime, hatuwezi kwenda kule tumepoteza ndugu zetu, tumepoteza vifaa vyetu vya kulimia, labda aje yeye mwenyewe aje atupeleke kule, otherwise tunapigwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine nataka nisistize, wataalam wetu hebu wachague moja kuishauri Serikali kwa weledi, wenzetu walioko Ulaya wamekuwa na ubunifu mkubwa sana kwa sababu ya matatizo. Leo sisi tuna matatizo kwa mfano kule Mbarali, kuna tatizo la ardhi, kuna matatizo ya maeneo oevu, mimi naona hakuna haja ya kuanza kupigana kikubwa ni kwamba, Serikali wataalam washauri ni jinsi gani tunaweza tukatokana na hilo wakiwashirikisha wananchi. Kuna mambo mengine yanafanyika bila kushirikisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni nchi ambayo ni ya umoja hebu tuende tuwe tunawashirikisha wananchi katika mambo mengine ambayo yanafanyika. Kwa hiyo mimi naomba wataalam wetu waishauri vizuri Serikali kule chini Mbarali watu wanasema achana na kitu chochote kile sisi ni ardhi. Kwa hiyo watu wabuni ni jinsi gani tutatumia ardhi pamoja na kuhifadhi mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kule Kyela kuna suala la cocoa, kuna matatizo pamoja na Serikali yetu na Mkuu wetu wa Mkoa kujitahidi kwa dhati ya moyo wake kuhakikisha anaondoa matatizo yanayotokea, lakini imekua ni ngumu kwa sababu ya nature ya zao lenyewe lilivyo. Kwa hiyo mimi ningeomba kuna vitu vingine ambavyo hakuna haja ya kuingizia kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani, kwa sababu lile zao ni zao ambalo haliwezi kumnufaisha mkulima, kwanza ni zao la wazee, ni zao ambalo watu wanalima kwenye nyumba zao. Kwa hiyo inakuwa ni ngumu sana kulifanya liingie kwenye stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ili tuendelee tunahitaji sana nishati, kuna miradi mingi ambayo inahitajika ili kuweka nishati vizuri. Tusitegemee Bwawa la Mwalimu Nyerere tu, kule kwetu Mbeya kuna mradi wa River Songwe Basin mara nyingi hauongelewi lakini ni mradi ambao unakuja na Megawatt 90 za umeme ukikamilika. Mimi ningeomba sasa iwe ni wakati sahihi Serikali kuanza kuutekeleza huo mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kiwila Coal Mine kuna megawati 200 ambazo zingefanyiwa kazi saa hizi tungekuwa tunapata umeme na tayari tusingekuwa kwenye matatizo haya ambayo Kyela kila siku ni giza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine nitachangia kwa maandishi lakini kuna Kiwanda cha Urafiki ni aibu tena ni kwa Mheshimiwa Kitila Mkumbo kule.

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa kengele ya pili.

MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Urafiki pale imekuwa ni sehemu ya kupangisha badala ya kutengeneza nguo ambazo tulinuia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono, hoja ahsante sana kwa nafasi.