Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mahali hapa muda na wakati kama huu, lakini kipekee pia nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Neema zake kubwa kubwa alizozineemesha katika Taifa letu. Kama neema hii mpya iliyoingia wanasema, “the state of at neema” ya kupata Rais wa Bunge la Dunia. Ni neema kubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Bunge la Dunia kwa mimi kuwa sehemu ya uzoefu nilioupata bila yeye kutaka kwenda tusingepata uzoefu ambao tumeupata. Nashukuru sana kwa nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuipongeza sana Serikali kwa jitihada kubwa za kuhakikisha maendeleo ya Taifa letu yanasonga mbele. Kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji. Katika mchango wangu nakwenda moja kwa moja katika hitimisho na vile vile nitarudi nyuma ya hotuba iliyotolewa na Waziri waWizara hii ya Mipango na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kwa hitimisho zuri kabisa ambalo kwa hakika limeonesha dhamira ya Wizara hii kuwa think tank ya Taifa hili, ameeleza vizuri kabisa kwamba tunapaswa kuweka mipango na kuipa vipaumbele na kama Taifa kuridhia kwa pamoja namna gani tutaviendea vipaumbele hivyo ambavyo tumekubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndio maana halisi ya kuwa na Wizara ya Mipango kama think tank ya Taifa hili. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri. Nimekwenda zaidi ulivyosisitiza kwamba, mipango hii ni mipango ya maendeleo ya Taifa letu na sio mipango ya Serikali, maana yake ni kwamba umelenga kabisa kuhakikisha Taifa hili linasonga mbele kimaendeleo na sio kuwa na mipango ambayo haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Kamati yetu ya Miundombinu tulikuwa na kikao pamoja na Kamati ya Wizara ya Fedha. Suala lililoniumiza kwa uchungu na nilisema kwa uchungu kabisa ni kuwepo na miradi mingi ya maendeleo ambayo fedha zake haziendi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya fedha alielezea vizuri sababu ya kwamba miradi hiyo inakuwepo na nani hataki miradi, kila mtu anataka miradio. Sasa ifike wakati tuangalie vipaumbele vya Taifa letu ili tuweze kusonga mbele na bila kupanga mipango ya Serikali bali tupange mipango ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba katika hoja hiyo nzuri aliyoitoa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, mimi naiunga mkono asilimia mia moja, lakini ili mipango ile itekelezeke ni lazima kuwepo na ufuatiliaji na tathmini ya mipango hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo ambacho sikubaliani nacho ni Wizara hii ya Mipango kujifanyia ufuatiliaji na tathmini, naona hii haiko sawa. Mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ni lazima ifanywe na Wizara nyingine ambayo itaweza kuangalia vizuri utekelezaji wa mipango ile, lakini italeta contradiction na kutakuwa na conflict of interest au actions kwa maana mimi nimepanga mwenyewe halafu mimi nijitathmini mwenyewe, hatutaweza kwenda sawa. Ni lazima jambo hili liangaliwe kwa namna nzuri ambayo litaweza kuwekwa na lilete tija kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG amesema wazi fedha nyingi ambazo zinapotea katika Taifa letu, na tulikuwa tunaamini mifumo kwamba itatusaidia kupunguza mianya ile, lakini mifumo nayo inachezewa. Kama mifumo inachezewa basi ni lazima tuje na ufuatiliaji wa mara kwa mara na tathmini za mara kwa mara za miradi ya maendeleo. Kuna mambo mbalimbali ambayo katika Taifa letu tumeyaona ni maendeleo, kwa hiyo naomba kama Taifa ni kwa nini tunaogopa kuingia katika ufuatiliaji na tathmini? Ni nani anayeogopa kivuli chake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona tumetoa mifano mingi kwenye Afrika yetu hii. South Africa wanayo, Uganda wanayo…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Engineer Ulenge kwa sababu ni kati ya Wabunge ambao ninaweza kuwaita ni ma-champion wa monitoring and evaluation na amekuwa akitusaidia ushauri wa mara kwa mara. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kutokana na mawazo yake na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge wengine na hasa utendagi kazi mzuri wa mtangulizi wangu Mheshimiwa Simbachawene, kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali imeamua kuanzisha Directorate mpya ya monitoring and evaluation na iko ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Sheria ya mipango tuliyopitisha tumempa nafasi Waziri wa Mipango yeye kuiangalia ile miradi mikubwa ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kazi ya kufanya monitoring na evaluation kwa utendaji kazi na shughuli zote za Serikali kwa mujibu wa Directorate mpya imebaki kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na tunaomba Waheshimiwa Wabunge, muendelee kutushauri na tukiweza kujaaliwa mwakani tutakuja na ripoti mpya ya ufuatiliaji na tathmini ambayo itaangalia utendaji kazi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mbunge…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Engineer, taarifa hiyo.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokea taarifa hiyo na ninafahamu kwamba Serikali imechukua hatua. Ni kweli kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, hiyo Directorate ya monitoring and evaluation ipo. Shida yake ni nini? Iko chini ya Mkurugenzi wa Mipango, uongo au ukweli? Nafikiri hii ndio contradiction ambayo mimi naizungumzia, kwa hiyo, nashukuru kwa taarifa ya Mheshimiwa Chief Whip, kwamba Serikali mtalianglia vizuri, mimi nimeridhika na hilo na ninaamini Serikali yetu ni sikivu na inapokea maoni yetu ipasavyo.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uzingatie muda wangu tafadhari.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nataka nimpe dada yangu taarifa kwamba sheria iliyopitishwa na Bunge hapa iliyoanzisha Tume ya Mipango na kwa mujibu wa sheria hii, Bunge hili liliipa nguvu hiyo Tume ambayo ndio ya Taifa ifanye tathmini ya sera zingine zote za wizara zote ili tuweze kujua kama tunakwenda kwa mujibu wa sera ya Taifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya, Mheshimiwa Eng. Ulenge.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, napokea taarifa hiyo. Naifahamu hiyo Tume na ndani ya hiyo Tume kwenye hiyo sheria, inaonesha pia inafanya monitoring and evaluation, ndio kitu ambacho mimi naona ni contradiction. Niliiona ile sheria, kwa hiyo mimi naomba Serikali wataliangalia vizuri, wakiona inafaa, wakichukua na maono ya uzoefu wa nchi nyingine za Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu uuzingatie umepotea muda mwingi tafadhari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wetu ambao umewasilishwa na Waziri mwenye dhamana umeweka mkazo katika kuimarisha uzalishaiji katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Mimi naomba nizungumzie sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha imekopesha boti kwa wavuvi na sisi Mkoa wa Tanga tumepata boti kumi na nne zenye thamani ya bilioni 1.2. tunaishukuru sana Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenye dhamana ameeleza vizuri kwamba malengo au msisitizo ni kuhakikisha thamani inaongezwa katika mazao yatakayouzwa nje ya nchi, sasa sisi tumepata boti, alhamdulillah tunashukuru, lakini je, boti zikishazalisha zaidi tunaongezaje thamani kama ukanda wote wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kilomita takribani 1400 kutoka Tanga mpaka Lindi hakuna viwanda vya kuchakata Samaki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini viwanda visijengwe ukanda wa Bahari ya Hindi, ili kuweza kuongeza thamani katika mazao ya uvuvi ili yaweze kusafirishwa nje ya nchi? Ni lini Serikali watajenga viwanda ukanda wa Bahari ya Hindi ili tuweze kuongeza thamani ya Samaki wanaozalishwa kwenye Bahari ya hindi waweze kwenda nje ya nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani tani laki saba na thelathini elfu zinazalishwa huko. Kwa nini hatuoni maana ya kuhakikisha uchumi wa blue tunaupa thamani ya kutosha kwa kujenga viwanda katika ukanda wa Bahari ya Hindi? Hili linashindikana vipi? Mbona Ziwa Victoria tumeweza? Ni wapi pa kubwa ukanda wa Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, mbona kule imewezekana? Tunaiomba Serikali katika mipango yake na hili walipe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia Bandari. Tunaipongeza Serikali, tumeona mikataba imekwishaingiwa ya kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam. Sasa, wote tumekubali. Pia, nchi nyingi ambazo zimeendelea mfano Singapore na south Korea ni kutokana na rasilimali bahari. Sasa Serikali iweke macho yake pia kwenye bandari za pembezoni. Ni lazima tuchechemue uchumi katika yale maeneo ambayo yana Bandari. Ni kweli fedha zimepelekwa takribani bilioni 500 katika Bandari ya Tanga na kweli kina kimeongezwa. Hata hivyo, bila kuchechemua uchumi wa maeneo yale meli kubwa haziwezi kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima yale yote yanayopatikana katika maeneo yale kama Mtwara – Liganga na Mchuchuma, Tanga, yote ambayo yanaweza kufanyika Mkoani Tanga ili kuchechemua uchumi wa Tanga ili meli kubwa ziweze kwenda Serikali ipange kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, Serikali imeweka mpango kwenye Bandari ya Mwambani, nafikiri sasa ni wakati sahihi. Sheria ya PPP imekwishakamilika, Bandari ya Mwambani ipatiwe mwekezaji na uchumi uchechemuliwe katika Bandari ya Tanga ili tuweze kunufaika na rasilimali bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, ukiangalia Nchi ya China ina bahari katika maeneo mbalimbali lakini siyo mizigo yote inapita Guangzhou, siyo mizigo yote inapita Shanghai. Lazima kama Taifa tuamue kupanga mizigo ipi ipite wapi. Pia kwa nature ya Tanga ilivyokaa na ukizingatia Mradi wa Bomba la Mafuta unaokwenda, Tanga iwe dedicated kwa ajili ya mafuta na hilo linawezekana. Kwa nini hatutaki kufanya hivi? Hakuna Taifa ambalo litaendelea bila bahari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata pale Bagamoyo walipofikiria kuanzisha upya Bandari ya Bagamoyo, wanafikiria pamoja na viwanda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, haiendi peke yake. Kwa hiyo, naiomba pia waangalie namna ya kuchechemua uchumi wa maeneo yenye bandari ili tuweze kunufaika na bandari zetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)