Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kutoa mchango wangu kwenye Wizara hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa, niungane na wenzangu kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia na kukubali ushauri wa Bunge wa kutenganisha Wizara hizi na hatimaye kutuundia Wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji. Kipekee kabisa nichukue nafasi kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nimshukuru kwa kutupa mtu ambaye ni sahihi, tukiamini kabisa kwamba lengo na dhumuni la Wabunge tulikuwa tukilizungumza kuhusiana na Mipango kapewa mtu ambaye ni sahihi na sasa imani yetu ni kwamba Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo atatuvusha kwenye hili. Akiamini kabisa kwamba Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji inapaswa kuwa ndiyo dira, mwelekeo na catalyst ya kutuonesha wapi tunatakiwa kwenda kama nchi na isiwe mipango ya mwaka mmoja peke yake naamini kwamba itakuwa ni mipango endelevu ya miaka nenda rudi, yote hiyo ni kutuonesha kwamba kama Taifa tunapaswa kuelekea wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, wewe ni msomi nafikiri kwa sababu wewe ni Professor, unajua, hakuna mipango mizuri ambayo inaweza ikafanyika, kwa uchache tu kwanza, bila kuzingatia research. Pili, bila kuoanisha na kutazama sera (policy) mbalimbali zinazoshabihiana kwenye Wizara na Sekta husika, hili ndilo inawezekana ikawa ufaulu mkubwa sana wa Wizara hii kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mchango wangu utajikita hapa. Kwanza, ambalo ningetamani nikushauri ni kwamba pamoja na kwamba unaweza ukawa na mipango mizuri uliyotuwasilishia leo hapa lakini mipango yako ningekushauri Mheshimiwa Waziri iende ikatazame sera mbalimbali za kisekta hasa sekta za uzalishaji, ambazo kimsingi zitashabihiana na kuku-boost kwenye Mpango wa Taifa 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera mbalimbali ambazo zimepitwa na wakati haziwezi kusaidia Mpango wa Taifa linalokusudia kwenda miaka mitato, kumi kwenda mbele. Mfano, kuna Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995, sera hii kwa namna ambavyo ameizungumza Mheshimiwa Waziri, kwenye wasilisho lake sera hii inagusa maeneo mengi. Migogoro inayozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge, ambayo iko TANAPA, TAMISEMI na Wizara ya Ardhi inagusa wananchi wanyonge ambao ni wananchi maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna yoyote kama Taifa likiwa lina mipango mizuri inayogusa wananchi maskini bila kutazama namna ya kutatua ile migogoro hatuwezi kupata ile furaha tunayoitamani kutoka kwa wananchi wetu tunaowawakilisha. Kwa hiyo, ningetamani sana Mheshimiwa Waziri, kama nilivyosema kwa sababu Wizara yako ni catalyst iende ikatazame namna ya kufanya maboresho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kwenda na mipango ya miaka mitano mbele tunakwenda kuzungumzia 2030, huku una sera ya mwaka 1995 yaani miaka 18 iliyopita kwa population ambayo ilikuwa haifiki milioni 20 tuitumie kupanga mipango ya nchi ya kwenda zaidi ya mika 10 mbele. Kwa hiyo, ningetamani Mheshimiwa Waziri, uende ukakae na utoe ushauri kabisa kwenye Wizara za Kisekta hizi ambazo kimsingi ndizo zinapaswa zikusaidie wewe kuhakikisha mipango inakwenda kwenye Wizara hii, wafanye maboresho ya sera ambazo zimepitwa na wakati, ikiwemo na hii Sera ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, Mheshimiwa Waziri kwanza utapunguza urasimu kwa maana ya kwamba utaboresha Sekta ya Uwekezaji ambayo iko chini ya Wizara yako. Pili, utakwenda kupunguza migogoro ya miingiliano kati ya Wizara zote tatu ambazo kimsingi ndiyo wananchi wanyonge wanakotoka. Niliwahi kusema hapa GN ya eneo moja inaweza likatolewa na Wizara tatu tofauti, yaani TAMISEMI, inatoa GN ya kuanzisha kijiji, Wizara ya Ardhi inatoa GN ya kutengeneza mipaka lakini vilevile ukienda kwenye upande wa maliasili nao wana GN yao ya maeneo ya hifadhi. Kwa hiyo, kule kunakuwa na kelele nyingi Mheshimiwa Waziri, kwanza kelele za wananchi maskini wanaozungumza haziwekwi, lakini wewe pia Wizara yako kwa maana ya uwekezaji hauwezi kuwa na tija kama maeneo haya yatakuwa hayajafanyiwa kazi. Kwa hiyo nikuombe sana ulione hili namna ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia mipango sehemu ya ardhi iliyopimwa ni zaidi ya asilimia 25 peke yake, lakini mipango unayoizungumza inakwenda kupangwa kwenye eneo hilo hilo la ardhi, kwa hiyo, ni lazima uone namna ambayo unaweza kupanga eneo hili likapimwa kwa maana ya nchi nzima ili mipango yako iende sambamba na kuweza kuleta faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Waziri ambalo ningekushauri, Bunge lililopita tulipitisha hapa Itifaki ya Huduma za Kibiashara za Nchi za Kusini mwa Afrika, ningeomba uone namna ya Itifaki hii kama Waziri wa Uwekezaji na Waziri na Mipango kutoa elimu kwa wananchi wazawa, wawekezaji wa nchi hii ili waone namna ya kuchangamkia hii fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili Mheshimiwa Waziri, ujiandae namna ambavyo Nchi wanachama ambazo zimekubaliana kufanya shughuli za kibiashara kwenye nchi hizi, namna zitakavyowekeza Tanzania na namna wananchi watakavyoweza kunufaika kama Tanzania. Mara nyingi tumekuwa tukipitisha Itifaki hizi lakini tunakosa mtu halisi wa kusimamia na kutafsiri nini ambachoo Bunge limekusudia. Kwa hiyo, ningekuomba Mheshimiwa Waziri, uone namna ya kulifanya hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu Mheshimiwa Waziri, mipango yako yote ningetamani Mipango ya Taifa lazima iendane na Mipango ya Wizara, Mipango ya Taasisi na Mipango ya Halmashauri. Hatuwezi kuwa na Mpango wa Taifa halafu huku chini kwa maana ya Taasisi, Halmashauri nazo zina mpango tofauti na mpango ambao unaendana na wewe. Kwa hiyo, kama Halmashauri zinaandaa mpango maana yake ni lazima zioane na ule Mpango wa Taifa, hatuwezi kuwa na mpango mdogo Halmashauri ambao kwako wewe hausimamii na hauna namna ya kuusimamia, maana yake tutakuwa tuna mipango mingi tu, kwamba huku Taasisi zina mipango yao lakini sisi tuna mpango mkubwa wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho Mheshimiwa Waziri, ninaomba kwa kuwa tayari tunakwenda kuinua uchumi ninayo barabara yangu ambayo nimeizungumza sana, siyo barabara yangu ni barabara ya Mkoa wa Mara, kimsingi barabara ile inatuunganisha kati ya Kenya na Tanzania. Barabara ile inapita katika Jimbo langu, nimezungumza leo nilipokuwa nauliza swali nilikuomba Mheshimiwa Waziri, barabara hizi ambazo ni kiungo cha uchumi kati ya nchi na nchi, kati ya Mkoa na Mkoa na Wilaya na Wilaya zipewe kipaumbele katika uwekezaji wa mpango ili angalau tuone namna ambavyo zinaweza kuinua uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi barabara za ndani zipo lakini barabara kubwa zinazounganisha kati ya nchi na nchi, Mheshimiwa Waziri uone namna ambavyo mnaziwekea fedha kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko hapo ziwekewe fedha ili angalau ziweze kuinua uchumi kutoka maeneo jirani na uchumi wa wananchi wote kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)