Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe pongezi kubwa sana kwa Serikali kwa Mheshimiwa Rais kwa kusikiliza maoni ya Wabunge na kutoa maamuzi magumu kwenye KADCO ambayo imetesa miaka yote ya Ubunge wangu miaka Nane tunajadili KADCO, hongera sana Serikali na tunajipongeza kama Wabunge.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kumteua Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Mipango, mimi nakuamini sana Mheshimiwa Kitila Mkumbo kwa research wewe ni bingwa kabisa. Mheshimiwa Rais amefanya vizuri amewakabidhi fedha na akawakabidhi na mipango, ninyi wote mnatoka Iramba, ndoho mayo mkiharibu tutauana, nina imani mtafanya vizuri na wapiga kura wenu tunawategemea na kule kwa shemeji zangu wanajua sasa mambo yanaenda vizuri kwa sababu mmekabidhiwa wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Kitila Mkumbo kwa mpango mzuri lakini lazima tukushauri, kupanga siyo makaratasi, mara nyingi tumekuwa na mipango lakini mipango inakuwa haitekelezeki. Najaribu kuona vitu ambavyo baadae tutakuja kukusulubu humu kukuuliza, nakupa tu mfano mdogo. Kwa mfano, unasema tunajenga vituo vya gesi kwa ajili ya ku-refuel magari, lakini najiuliza wenzangu labda mnaweza mkanisaidia tunayo magari haya yanayotumia gesi Tanzania, kwenye takwimu tuna magari sijui 3000 na kitu, ni sawa. Lakini kweli mnaona jinsi ambavyo yale magari yanavyobadilishwa kutoka mfumo wa mafuta kwenda kwenye mfumo wa gesi, yaani inakushawishi nini mpaka ukaanze kujenga vituo kwa design ile ya magari yaliyoko Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu ametupa bahati ya kuwa na maliasili, maliasili kama tumegundua tuna gesi ambayo inaweza kutumika kwenye magari, kwa nini Waziri wa Mipango, usingeleta mpango hapa tukachukua wataalam tukawapeleka kusoma huko Japan, halafu wakaja na teknolojia ndiyo tukaanza kuliko kukurupuka. Nakupa mfano, ukipanda kwenye gari ambalo limebadilishwa mfumo wa mafuta kwenda kwenye gesi limewekewa drum huko kwenye buti na Wajapani walivyotengeneza gari lile buti ni kwa ajili ya kuweka mabegi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najiuliza nyinyi wenzetu Mawaziri kidogo hadhi yenu ni kubwa mnavyoanza hii teknolojia ya gesi, mimi nilikuwa nashauri muanze na gari za Serikali za Mawaziri tuwawekee yale ma-drum ya gesi kule nyuma, halafu usafiri na hilo gari hupati hata usingizi! Naona kabisa tunaenda kupoteza hela kwenye vitu ambavyo haviwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu nchi zilizoendelea wanaotumia gesi wanatoa oda ya magari yao kwamba yanakuja special kwa ajili ya gesi, lakini angalia hata hayo malori ya Dangote mkikutana nayo watu wanachomelea ma-drum yanawekwa nyuma ya cabin, yaani kwanza gari lenyewe linakuja limeshapoteza na uzito ile capacity yake, kwa hiyo, mimi naona kabisa tunaenda kufeli tutaanza lakini hawa watumiaji wenyewe kwa sababu sisi wengine tunajifunza kutoka kwa Serikali, kwamba Serikali inapoona gari fulani ni zuri, kwa mafano V8, tukiona mmekuwa nazo nyingi Serikalini na sisi tunakimbilia kwa sababu Serikali imeshaona ni gari zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri gari la Waziri wa Fedha, kwa sababu wewe ni Mchumi na Waziri wa Mipango, kwa sababu wewe unatupangia tukufungie gesi kwenye buti lile drum liwe mfano kwa sababu wewe utabana matumizi, kuliko kwenda kuweka rehani maisha ya Watanzania kwa kuweka teknolojia za kijiweni halafu Serikali inaingia gharama kwenda kupitisha bajeti ya kujenga vituo, naona kama hatuendi sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza hapa Mbunge wa Ngorongoro, amezungumza suala la ng’ombe, ndugu zangu mimi huwa nazungumza kila siku ng’ombe huwa hawaongei lakini wana machozi, sisi tuliokuzwa na ng’ombe tunafahamu, Waziri rafiki yangu sana Mheshimiwa Kairuki, hili suala ukisimama hivi unavyosimama, mimi niliwahi kulia humu nikamlilia Mheshimiwa Magembe aliekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, hakumaliza siku tatu akala kichwa, akaja na mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba busara kwenye suala la watu maskini, hivi tunahitaji shule gani kuona kwamba watu wetu wanaonewa? Nimemsikiliza kaka yangu AG, anasema ukomo, Mahakama ina ukomo, Mahakama ya Mkoa, hivi mtu wa Darasa la Saba anayefuga ng’ombe unamuambia hicho kiingereza alichozungumza hapo cha ukomo wa Mahakama, nani anaelewa hayo mambo? Huku akienda anaambiwa tunafanya uchunguzi, kumbe ninyi mnashughulika na kuuza ng’ombe! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu jiulize yaani hukumu imetoka Tarehe 31, halafu mnauza ng’ombe Tarehe 01. Maana yake dalali alikuwepo siku hiyohiyo wala ile hukumu haikuwa na alternative lipa faini, yaani ni vitu ambavyo, kwa kweli unafika mahali unajiuliza pengine hii nchi ni ya matajiri tu maskini hatutakiwi kuwa Tanzania! Haiwezekani...

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Waitara achana na taarifa kwanza …

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, kuna taarifa kwa Mheshimiwa Waitara, kwa ufupi kabisa.

TAARIFA

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Musukuma, namuongezea kwamba TANAPA hao ndiyo walikamata ng’ombe, TANAPA walipeleka Mahakamani, TANAPA ndiyo walipewa hukumu kwamba wameshinda, TANAPA wamepiga ng’ombe mnada na ng’ombe mmoja amenunuliwa chini ya shilingi laki moja kila ng’ombe mmoja. (Makofi)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, hakuna taarifa juu ya taarifa. Mheshimiwa Musukuma taarifa ya Mheshimiwa Waitara, unaipokea.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea na ninaomba Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu ndiyo kasi inaingia namba tatu hebu pumzikeni kwanza, wekeni pause hizo taarifa kuna wanaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahitaji kuwa na elimu ya namna gani kugundua kwamba hii ni dili kuanzia huko TANAPA, na watu wetu wanakuwa maskini. Halafu unapanga mpango huo mpango ukawafaidishe wakina nani? Mnataka watu wote sasa muwalishe na TASAF, hii kitu hakiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri achana na mambo ya kusema nisome sheria, tunajua wewe ni Mwanasheria mzuri lakini ukisimamisha Wabunge humu ndani wanaokaa jirani na mapori siyo mtu wa kwanza leo, wakikosa hela wanaenda kuswaga ng’ombe wanaziingiza kwa bunduki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jiulize hukumu imetoka tarehe 31 haina hata notice kwamba mlipe faini au ziuzwe, zimeuzwa kesho siku hiyo hiyo zimepakiwa zimeenda Dar es Salaam, unahitaji kuwa na degree kujua hiyo mipango? haiwezekani! Ni lazima Mheshimiwa Waziri, toka kwenye boksi hapo ukienda hivi, wafugaji sisi huwa tuna kitu chetu tukitoa machozi Mungu atatusikia huko aliko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Kaka yangu Waziri wa Mipango, niambie unahitaji kuwa na shule gani kwamba watu tunafeli, angalia Dar es Salaam, mna mwendo kasi, kuna DART na kuna UDART. DART anamiliki lami, ile barabara ambayo haifi miaka 100, halafu anamiliki mifumo ambayo inaweza kusimamiwa na TAMISEMI na mtu mmoja tu, unaweka Mkurugenzi, unaweka Chief, unaweka ma-V8 na makorokoro mengi kwenye kitu ambacho hakizalishi. Mwisho wa siku kila mtu anasubiri mshahara tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo mmeua kwa ajili ya kupiga, magari yenyewe yameisha, sasa kama kuna mtu mmemkodisha barabara kwa nini huyu msimamizi DART, fukuza wote pale, weka hapo mtu mmoja tu, kwa nini tunasimamia POS nchi nzima unashindwaje kusimamia Mfumo wa U-DART? Hicho ni kitu ambacho mnatengeneza mipango mizuri halafu mashirika yetu hayaendelei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushauri pamoja na Waziri wa Mipango, fukuza wote pale, unaenda unachukua wazee wastaafu umedumbukiza ma-V8 mpya kwenye kitu ambacho hakizalishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza suala la bangi. Leo nazungumza mara yangu ya tatu, mnaona kama naongea vitu vya ajabu, nami sishabikii bangi ya kuvuta. Huwa nawaangalia Polisi wanafyeka kule na ma-TV, lakini hiki ni chanzo. Angalieni Canada, Colombia, Pakistan, dunia nzima inapiga kelele na madawa ya kulevya wao ndiyo chanzo cha mapato. Sasa tunafyeka kwa ajili gani, tungedhibiti watumiaji, nchi jirani wanatumia, sasa kwa nini tunazuia, unaenda unafyeka unaonyesha na kwenye TV, unafaidika kitu gani wakati hilohilo zao ndilo linaweza kukuingizia kipato kutoka nchi ya Jirani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza kidogo suala la CAG. Uliona mchakato wa CAG ulivyokuwa, nashauri ili tuende vizuri tunapofika kipindi cha kuhoji wale Wakuu wa Taasisi, kwa sababu huu ni Muhimili unajitegemea siyo wa kihuni, tuna Serikali, tunayo Mahakama na tunalo Bunge. Ninashauri ukiondoa wale Viongozi Wakuu wa Serikali wanne wa juu, hawa wengine bila kuangalia nyota au ngao za mabegani, hakuna kuja humu na ma-bodyguard, watu wanaogopa kuwahoji, kwani nani ataingia na bunduki huku ndani? Tunakuja tumekaguliwa mpaka mlangoni pa kuingia, sasa mtu anaitwa kuja kuhojiwa, mfano ana ngao mbili hapa mabegani, anakuja na walinzi nane mnanyanyuliwa mpaka na kwenye viti utamhoji vipi huyo mtu? Mimi nashauri wakifika pale protocol zao ziishie kule, maana hata sisi tukiwa watuhumiwa kwenye taasisi zao hatuendagi na mbwembwe tunaenda mmoja, waje humu watu wawahoji bila kuwa na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Kanda ya Ziwa na nimeshangaa sana Waziri wa Mipango, umenisahau. Hivi ninyi watu wa Kanda ya Ziwa labda huwa mnatuona kama sisi ni Waganda au namna gani? Uwanja unaoingiza pesa Tanzania ukitoa Uwanja wa Dar es Salaam, Uwanja wa pili ni Uwanja wa Mwanza, kigugumizi ni cha nini kutuwekea International Airport Mwanza, mnieleze. Halafu mnakuja na mpango, nawaangali na Wabunge wenzangu wa Kanda ya Ziwa mnapiga makofi, sisi tunakuja kusindikiza kila siku humu ndani? Uwanja wa Ndege wa Mwanza unajiuza, una wateja tuna nchi jirani zinategemea pale. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajenga reli …

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Brother, tuliza basi.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, muda wako umeisha naomba umalizie.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba namalizia huyu ameingilia muda wangu, kama unataka tuelewane ukinichenga hapa Mheshimiwa Waziri wa Mipango, mwaka huu ni mwisho kutudanganya mlisingizia uwanja umekataliwa na Ilemela, mmerudishiwa na hela bilioni 4.5, tunaomba kwenye bajeti inayokuja tuone hapa unakuja na hela, ukija na swaga tutazinguana. Nakushukuru. (Makofi)