Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwa siku ya leo pamoja na kuwa sauti yangu haipo vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali kwa sababu ya kupokea maoni ya Wabunge na maoni ya wadau; na kurejesha Tume ya Mipango lakini kuja pia na hii Wizara ambayo inaongozwa na Profesa Kitila Mkumbo ambaye wakati naanza Chuo Kikuu cha Dar es salaam alikuwa Rais wangu wa DARUSO na mimi nikawa Mbunge kwenye Bunge la Wanafunzi. Tulikuwa tunachuana sana pale USRC nadhani unakumbuka Makamu wako wa Rais akiwa Dkt. Francis. Kwa hiyo, nakufahamu kwa utendaji toka siku zile tukiwa pale Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa na Mheshimiwa Kibajaji, Mheshimiwa Lusinde tulikuwa tunaenda Iringa, Mafinga kwenye shughuli pale Bwawani kwa Mchungaji Mahimbi na wachungaji wale walisema wao kama viongozi wa dini wapo na Serikali na mojawapo ya kazi wanayoifanya ni kuombea Serikali lakini pia kumuombea Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tupo na watu wanatuombea katika nchi hii sisi kama viongozi kwa hiyo ni wajibu wetu kutenda yaliyo mema kwa manufaa ya nchi hii. Siku ile ninapoongozana na Mheshimiwa Lusinde, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu akaniambia naona mmejichagua, sikumwelewa. Baadaye akaniambia si naona mnaenda wote simba huko Mafinga mmechagua, wewe simba Mheshimiwa Kibajaji nae simba. Sasa mimi baadaye nikakaa nikaona alah! Kumbe Waziri wa Mipango naye yanga, Waziri wa Fedha naye yanga, of course mmeteuliwa lakini imetokea nyinyi nyote yanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni simba inaeleweka niwaombe kabisa fanyeni kama yale ambayo wanafanya Max Nzegeli na Pacome katika utendaji wa kazi ndani ya Serikali, nadhani mtakuwa mmenielewa vizuri najua wana simba wenzangu hawawezi kunikubali katika hilo lakini kuna hatua tukifika lazima tukubali ili tujipaange kwa hiyo, tumekubali yote tunajipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili. Kuna mtu juzi alikuwa ananiambia naona Wabunge Bunge hili mmechachamaa nikamwambia kwa nini? Akasema ingekuwa wakati wote mko hivi hivi, nikamwambia hapana inategemeana na agenda ya wakati huo. Kwa mfano, wakati ambapo yamefanyika mambo ya kupongeza tutapongeza, wakati mambo ya kusahihisha tutasahihisha, ndiyo wajibu wetu kama Wabunge. Kwa hiyo, kwa wakati huu kwanza mimi nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake na yakupongeza yapo mengi lakini mimi kwa niaba ya Wanamafinga nitasema moja tu maana yake naweza nikamaliza muda wangu kabla sijaenda kwenye hoja ya kuchangia mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la kupongeza ni suala katika elimu, sisi pale Mafinga tuna shule ya msingi Mwongozo; ilikuwa na watoto kama 1800. Tumepata fedha tumejenga pembeni Shule ya Msingi Muungano, tumepunguza msongamano kwa watoto lakini Kata ya Boma ambayo ina watu wengi kuliko watu wote katika Mkoa wa Iringa kwa mujibu wa sensa na hapa pia nitumie nafasi hii kuwashukuru watu wa takwimu, walikuja kutujengea uwezo watu wetu namna ya kutumia takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alisema jana Mheshimiwa Profesa Shukrani nadhani hapo, kwamba ile sensa ikatusaidie katika kutumia takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo; na kuna kitu wale watu wa sensa walitufundisha pale tulikuwa na viongozi wa dini na wazee na wakaanisha kata gani ina vijana wengi, kata gani ina wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tulijifunza kwamba hii kata yenye vijana wengi maana yake inabidi mipango mingi ya kuweka shule nyingi ielekezwe kule kwa sababu hao ni vijana ambao population wise wao wapo kwenye stage ya kuongeza idadi ya watu duniani. Lakini viongozi wa dini mmoja aliniambia; Mbunge nimejifunza hapa kwamba lazima nijue waumini wangu wazee ni wangapi, vijana ni wangapi, watoto ni wangapi hata tunapopanga mipango ya maendeleo ya kanisa letu au ya msikiti wetu basi tunaendana na ile takwimu na mtawanyo wa idadi ya watu katika eneo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza pia watu wa sensa. Kwa hiyo, nampongeza pia Mhehimiwa Rais katika elimu tumeona madarasa, ukienda Itimo pale kwetu Mafinga, ukienda Ndolezi, sabasaba na pale Ndolezi Kata ya Boma tuna shule mpya ya sekondari ambayo ita-accommodate sasa hawa watoto wanaotoka kwenye shule hizi za msingi. Kwa hiyo, itoshe kusema kwamba sisi kama Wabunge na hasa Wabunge wa CCM pale pa kukosoa na kusahihisha tutasema na pale pa kupongeza tutasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye mpango. Mimi nimesoma mpango na kwa jinsi ya mpango ulivyo maana yake ni kwamba ni wajibu wangu kama Mbunge kutoa maoni na mapendekezo kama ambavyo umesema mpango. Sasa yapo mambo nitashauri kwa maana katika hii matarajio au maoteo ya bajeti ya trilioni 47 ina mtawanyo wake kuna deni la Taifa kuna mishahara kuna OC na kuna mambo ya maendeleo; na fedha hizi tutazitoa wapi? Tutatoa mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kikodi, ninawapongeza TRA wamekuwa wakikusanya vizuri unaona yale maoteo wakati mwingine wanavuka zile asilimia, kuna fedha ni mikopo na misaada kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe ushauri. La kwanza katika ukurasa wa 11 wa paper ile ya Mheshimiwa Mwingulu ukurasa wa nane amesema kwamba, Mikakati. Amesema baadhi ya mikakati ni ile kuwa na one stop center ili kuboresha mifumo ya ukusanyaji pamoja na kutoa namba ya malipo jumuishi. Sasa hapa nimuombe Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa TAMISEMI, sisi Mafinga Mufindi tunategemea misitu na tunategemea msitu wa Sao Hill. Sasa wakati mipango ya Serikali ni kuwa na one stop center maeneo ya kukusanya mapato kwa jumuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi utaratibu uliokuwepo, kama mimi nikipewa ile bili na TFS kwa maana ya shamba la Sao Hill ninakwenda kulipa mle mle ndani nalipa na fedha za Cess na fedha zingine katika ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa TFS wamekuja na utaratibu kwamba ile Cess awepo mtu wa halmashauri ya Mufindi wa Halmashauri ya Mafinga pale kwenye shamba la Sao Hill awe anakusanya. Sasa tunasema makusanyo jumuishi, one stop center kwanza tunatawanya nguvu na resource; lakini pili hatuwezi kukusanya ipasavyo. Kwa hiyo, mimi naomba na ninashauri TFS na Waziri na Wizara ya TAMISEMI tuendelee na ule utaratibu kwa sababu ndiyo maona ya Serikali lakini ndiyo utaratibu ambao una ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina ugomvi na TFS na wala sijawahi kuwa na ugomvi nao naamini katika hili tukishauriana vizuri tuendelee na ule utaratibu mtu akipewa bili alipe na kwanza hata yule mlipaji unampunguzia usumbufu. Sambamba na hilo ili tuboreshe na kuongeza makusanyo, ninashauri ndugu zangu tuangalie pia kwenye VAT sio tu kwenye mambo ya misitu hata katika upana wake tujaribu kuona je, hatuwezi kupunguza ikawa user friendly watu wakalipa kwa wingi wakalipa kwa hiari kama ambavyo tumesema hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kutoka mwisho. Wapi fedha nyingine tutapata, amesema hapa Mheshimiwa Kakoso, ninawashauri watu wa Serikali, nendeni kwenye Hansard kasomeni haya mambo ya hewa ya ukaa aliyosema Mheshimiwa Kakoso. Labda watu hawaelewi hewa ya ukaa maana yake ni nini? Sisi wenye misitu, kuna kitu ukanda wa bahari kinaitwa blue carbon, ile pale misitu kila inachopumua wale wenzetu wenye viwanda ndiyo inasaidia at least kwenye mambo ya climate change ku-regulate hii hali ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna fedha na Mheshimiwa Rais kila mwaka anaenda kwenye mkutano wa mazingira. Kwa hiyo, tayari kama mkuu wa nchi tayari ameshatoa hiyo sapoti. Kwa hiyo, wenzetu tushirikiane kwenye hewa ya ukaa kuna fedha kwenye mikopo, kuna fedha kwenye misaada lakini kuna fedha kwenye biashara hiyo ya mkaa. Ninaomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho. Timu yetu ya JKT Queens mimi ni mwanamichezo jana imeshinda ipo kule Adjan wakiwa na Masau yule msemaji na ikifanikiwa kwenye mchezo ujao ikatoka sare itaingia nusu fainali. Kwa hiyo, tunavyounga mikono michezo, tuangalie Simba na Yanga lakini tuunge pia mkono JKT Queens ambao wachezaji asilimia mia moja ni wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na kama mwanasimba nasema tumekubali tunajipanga. (Makofi)