Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya bajeti ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kusimama hapa nami nikiwa mmoja katika wachangiaji siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite zaidi kwenye hotuba hii ya bajeti hasa kwenye masuala machache ambayo nitaweza kuzungumza kutokana na muda. Katika ukurasa wa 51 kwenye vishikwambi vyetu, kwenye paragraph ya 61, Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusiana na suala zima la mimba za utotoni. Mimi ni mmoja kati ya wananchi wanaotoka kwenye mikoa yenye athari kubwa sana za mimba za utotoni. Asilimia 43 katika Mkoa wa Tabora mpaka sasa kwa mujibu wa takwimu ndivyo inavyosoma, ikiongozwa na Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza mkoa wetu ni mkoa ambao uko pembezoni, lakini wakati Mheshimiwa Waziri akiwasilisha hotuba yake, amesema kwamba ili kukabiliana na mimba za utotoni, Serikali itaendelea kujenga mabweni kwenye maeneo hatari kwa watoto wa kike. Hii haiwezi kuwa tiba ya kupunguza mimba za utotoni hasa kwenye mikoa yetu. Ninapokwambia asilimia 43 ni asilimia kubwa sana na tunaathirika sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Manispaa ya Tabora na ndiyo Halmashauri yangu. Pale tuna kata za mjini na za vijijini. Umbali peke yake wa shule anayotoka mtoto kutoka nyumbani kwao mpaka kufika shule, hiyo peke yake inachangia kwa kiwango kikubwa watoto wetu hapa katikati kupata changamoto na vishawishi vikubwa sana mpaka kupelekea watoto wetu kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tabora, mtoto ana miaka 12, 13, 14 unakuta ni mjamzito, inaumiza sana. Kama unavyofahamu, sasa hivi watoto wetu akifika Darasa la Nne, amekua, akifika Darasa la Tano mtoto ameshakuwa mwanamwali, na akishakuwa mwanamwali, ni lazima upatikanaji wa mimba kwa mtoto huyu ni rahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunaposema tuongeze mabweni badala ya kufikiria kuchukua hatua mbele zaidi ya kutoa elimu. Tunaomba sana elimu ya kutosha itolewe ili kuweza kunusuru vizazi vyetu. Hali ni mbaya sana. Hawa watoto mpaka kufikia kupelekwa huko kwenye bweni, tayari mtoto ameshaharibika huku, kwa sababu ya mazingira peke yake ya elimu wanayopata watoto wetu. Kwanza ni mbali na maeneo wanayoishi.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano mmoja, tuna kata moja iko vijijini inaitwa Kata ya Ifucha. Kata ile upande mmoja inapakana na Bwawa la Kazima, upande mwingine inapakana na Kata nyingine ya Ndembelwa. Shule ambayo watoto hawa wanaotoka upande huu na upande huu iko hapa katikati. Mwendo ni mrefu kweli kweli mpaka mtoto aende akafikie ile shule. Hapa katikati anakupambana na changamoto nyingi sana za vijana wenye ushawishi, na matokeo yake hali ya watoto wetu kupata mimba wakiwa bado na umri mdogo ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali katika bajeti hii, badala ya kufikiria kujenga mabweni, fikirieni kutusaidia kuwapa elimu sisi wazazi pamoja na watoto wetu ili kuondokana na changamoto hii ya mimba za utotoni. Hii ni mikoa ambayo wananchi wetu uchumi wao ni mdogo sana. Yaani hawana uwezo mkubwa kiasi kwamba mtu akishaambiwa Shilingi 1,000/=, Shilingi 500/=, akinunuliwa chipsi, mtoto anaingia kwenye majaribu hayo na mwisho wa siku tunaendelea kuwa na kizazi ambacho hakina elimu na matokeo yake mtoto kuweza kuzaa mtoto mwenzie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali iliangalie hili, na ni jukumu kubwa kwa Serikali, lakini hata sisi wazazi ambao tunasaidia kuhakikisha kwamba jamii yetu inajua athari za mimba za utotoni.

Mheshimiwa Spika, niangalie katika ukurasa wa 150 kwenye vishikwambi vyetu, Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu kufuta kifungu cha Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA). TCRA ina majukumu yake, lakini na TBS ina majukumu yake tena mengi na mazito. Kazi ya TBS tunafahamu ni kuangalia ubora wa bidhaa zilizopo nchini na zinazoingizwa kutoka nchi za nje. Vile vile TCRA ni kwenye masuala ya mawasiliano. Huu ubora ambao Mheshimiwa Waziri ameuzungumza anaouhitaji, ambao tunasema uondolewe kutoka TCRA upelekwe TBS ni ubora wa aina gani? Ni ubora wa mawasiliano ambayo tunahitaji kuyapata ama ni ubora wa aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri hajaweka wazi, amesema tu kwamba anafuta hiki kifungu, lakini akumbuke kwamba vipo vifungu pia ambavyo tuliviweka sisi wenyewe, lakini ni makubaliano ya Kimataifa kwenye hivi vifungu. Je, hivi vifungu ameviangalia vinaitaka nini TCRA? Vinataka TCRA ifanye nini ili kuweza kuboresha mawasiliano ya Kitaifa na Kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni sawa, na kuna eneo lingine hapa wakati napitia amesema kwamba hata pamba sasa itakuwa inaangaliwa na TBS. TBS wana Mabwana Shamba? TBS wana Mabibi Shamba? Mabibi Shamba na Mabwana Shamba ndio wanaoangalia ubora wa pamba. TBS anakwenda kukutana na nyuzi ambazo tayari zimeshatengenezwa. Wao wanatakiwa waangalie ubora wa ile mali ambayo tayari inakwenda kwa mlaji na siyo kuangalia mkulima amelima nini? Zile ni kazi za watu wengine. Hii itakuja kuleta changamoto baina ya taasisi na taasisi kuweza na kukuta kunakuwa na migongano na mwisho wa siku inakwenda kuathiri wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia hiki kifungu ambacho anataka kukifuta na kukitoa TCRA kukipeleka huko kwenye TBS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kidogo kuhusiana na suala la utalii. Kwanza naomba na mimi nimpongeze Rais wetu Mama Samia kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kuhusiana na hili suala la Royal Tour ambalo Wabunge tumekuwa tukilipigia kelele muda mrefu kwamba tunahitaji kutangaza utalii wetu. Tunahitaji utalii wetu ujulikane. Leo mama ameshafanya kazi yake, ameshamaliza. Sasa kazi ni kwetu sisi kuhakikisha kwamba yale ambayo yanatakiwa kufanyika yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niko kwenye Kamati ya Maliasili na Utalii. Bado kuna changamoto kubwa sana, hususan kwa hawa wawekezaji kwenye masuala ya utalii. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba inakutana na hawa wawekezaji tulionao ndani kabla hatujaamua kwenda kutafuta wawekezaji wengine ili waje kuwekeza hapa? Kwa sababu hawa waliko ndani wenyewe wana changamoto nyingi sana ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi. Changamoto hizi zinasababisha hata mapato kwenye masuala ya utalii kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hatujiulizi kwa nini wageni wanapokuja wakiondoka hawarudi tena? Shida ni nini? Wapi kuna changamoto? Nini kifanyike? Je, hawa wawekezaji ambao wako kwenye hii sector ya utalii tumewaandalia mazingira rafiki ya kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao kwenye mazingira mazuri? Tatu, hii royal tour inaenda kutotoa? Hata sasa hivi tunasema tu kwamba Royal Tour tayari, Royal Tour bado. Hawa ni wageni ambao wamekuja kwenye mwaka huu ambao walikuwa wameweka booking. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Royal Tour ni kuanzia mwakani, tumejiandaa namna gani kuhakikisha tunapokea hawa wageni? Je, baada ya kuwapokea, tumejiandaa namna gani kuhakikisha hawa wageni wanarudi? Je, Serikali kupitia Wizara ya Utalii inafanya kazi yake ipasavyo kuhakikisha kwamba tunaleta wageni wapya lakini hata wale waliokuja na wenyewe wanaendelea kurudi katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri sana Serikali, badala ya kuangalia tunahitaji wawekezaji wengine, tuanze kuangalia wawekezaji wetu wa ndani ili tuweze kuwasaidia kwenye changamoto zao na baada ya hapo, hata hao wengine wa nje watakuja kwa sababu kuna mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naomba nizungumze kwenye hii asilimia 10. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hii asilimia tano anayofikiria kuichukua aiache tu, kwa sababu hata hiyo asilimia 10 yenyewe, tunachosema sisi Waheshimiwa Wabunge, haitoshi. Haitoshi kwa sababu Halmashauri zetu tumetofautiana kimapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Halmashauri ya Tabora Mjini, lakini huwezi kuamini sisi tunashindwa mapato na Halmashauri ya Kaliuwa. Nasi pale Tabora Mjini ndio tuna Wamachinga wengi kuliko Halmashauri ya Kaliuwa. Kwa hiyo, ukimchukulia asilimia tano huyu mtu wa Tabora Mjini, ina maana asilimia tano inayobaki haiwezi kusaidia hata wale wamama na vijana na watu wenye ulemavu ambao tunategemea kwamba hizi fedha zinawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitamani sana Mheshimiwa Waziri aje na pendekezo la kuongeza badala ya asilimia 10 zifike asilimia 15 mpaka 20 ili tuweze kuwasaidia hawa akina mama wetu, vijana pamoja na watu wenye ulemavu. Chonde, chonde Mheshimiwa Waziri, acha hiyo hela, asilimia tano hiyo iache tuendelee na asilimia zetu 10. Lete sheria, tafuteni utaratibu mzuri wa kuhakikisha tunawasaidia Wamachinga waweze kupata maeneo yao. Tunao Wamachinga wengi, lakini mwisho wa siku tutafute utaratibu mwingine lakini siyo kuchepua hela ambazo tayari tulishakubaliana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kuhusiana na suala zima la hizi nywele bandia. Nataka nipate ufahamu, Serikali imefanya tathmini ya kugundua kwamba tuna viwanda vingapi Tanzania ambavyo vinatengeneza nywele bandia? Je, katika hivyo viwanda, ni viwanda vingapi vinavyotengeneza quality, yaani nywele ile nzuri ambayo hata mtu ukivaa unaonekana umependeza? Ni viwanda vingapi ambavyo vinafanya hiyo kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu unaweza ukasema kwamba unataka kulinda viwanda vya ndani lakini ndiyo ukaenda kuviua kabisa kuliko ambavyo ilivyo hivi sasa. Leo mimi nafanya biashara ya nywele, nina uamuzi, niuze nywele za kutoka nchini kwangu ama niuze nywele za kutoka nje ya nchi? Ila tufahamu, hii biashara ya nywele inafanywa na akina mama wenzetu. Wako akinadada ambao wanaishi maisha yao kwa kutegemea hii biashara ya nywele, lakini wanalipa kodi ya Serikali, hawajawahi kukwepa kodi hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni mdau mmojawapo na-declare kwamba na mimi navaa na ndiyo maana hiki nilichokivaa mimi kinaweza kikawa tofauti na kitu alichokivaa mtu mwingine. Kwa sababu unaweza ukavaa wigi ukajikuta ukitoka hapa mtu anashangaa hivi yule dada ni Mbunge kweli! Unavaa wigi unapendeza mpaka kila mtu anakuuliza. Sasa ndiyo quality zinakwenda namna hiyo. Je, sisi Watanzania kwenye viwanda vyetu tuko tayari kutengeneza wigi ambazo hata nikija dukani nasema hii nitavaa nitapendeza? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hebu tuwaache hawa akinadada ambao wanafanya hizi biashara wamekuwa maharufu sana. Wakina Luluz, Loluwa, na kadhalika wanaleta nywele nzuri ambazo kila mmoja anatamani aweze kuvaa na aweze kupendeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakuomba sana nimuombe Mheshimiwa Waziri, hii ni sekta muhimu kwetu sisi, kwa hiyo, naomba sana atusaidie angalau kidogo kuacha ile kodi jinsi ilivyo, wanawake wenzetu waendelee kufanya biashara na waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)