Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Lameck Nchemba, Naibu Waziri na watendaji wote wa katika Wizara na Taasisi ambazo zinaongozwa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kuitangaza Tanzania katika ramani ya dunia kiutalii kupitia filamu ya Royal Tour. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kusisitiza kwa TRA na Wizara kuona kwamba wafanyabiashara katika nchi hii hawarudishwi nyuma katika kodi zao zaidi ya mwaka mmoja, lakini vile vile kutokufungiwa kwa akaunti zao. Vile vile nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuondolewa ada ya form five na form six. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba siku za nyuma hela ambazo hazitumiki ikifikia mwezi Juni zinarudi lakini sasa hivi inaonekana zitaendelea kubakia, lakini vile vile wananchi wale ambao walikuwa wananyimwa hela kwa kupata hati chafu ambayo ni ukosefu wa watendaji, safari hii wataendelea kupewa, ni kielelezo tosha kwamba kuna utaratibu ambao Mheshimiwa Rais ameufanya kwa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, nitoe ushauri kwa Serikali na niseme kwamba naunga mkono hoja. La kwanza kwenye upande wa Royal Tour, Mheshimiwa Rais ameshakamilisha kazi yake, sasa hivi kilichobakia ni jukumu la Wizara ya Utalii, Wizara ya Ardhi, na Wizara ya Miundombinu kuhakikisha kwamba tunakwenda kule katika maeneo mengine ya utalii. Katika kipindi kilichopita utalii ulikuwa zaidi kaskazini, lakini utalii uko Morogoro kupitia Hifadhi ya Udzungwa, Hifadhi ya Mikumi na hifadhi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo ni hifadhi kubwa katika nchi hii. Vile vile utalii uko Katavi kupitia Hifadhi ya Katavi.

Mheshimiwa Spika, niombe Mawaziri wenye dhamana waendelee kutangaza hifadhi hizi ili ziendelee kutoa fedha na tija kwenye bajeti ya Serikali na kuleta maendeleo kwa Watanzania. Niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi na Wizara ya Fedha kupitia Wizara ya Ujenzi na Mheshimiwa Rais, katika bajeti ya mwaka huu barabara ya Bigwa - Kisaki tumepata kilometa 78 ambayo ndiyo barabara inayokwenda kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere tumepata kilometa 78 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami, lakini tumepata kilometa 11 kutoka Ubena Zomozi kwenda Ngerengere - Mvuha nayo inajengwa kwa kiwango cha lami na barabara hii inakwenda mpaka kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali na kwa kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwa tushapitisha fedha hizi ambazo fedha hizi zitakwenda kutengeneza miundombinu ambayo itakuwa rahisi kwa wananchi, lakini vile vile kuwawezesha watalii kufika kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, ambapo ndani ya hifadhi hiyo kuna Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ni bwawa kubwa katika Afrika, linaweza nalo likawa ni kivutio kikubwa kwa watalii na kuleta fedha nyingi kwa Wizara ya Maliasili na kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe tu sasa hivi barabara hizo zikatangazwe mara moja tukimaliza bajeti, wakandarasi wakaingie kazini, tupunguze watalii kutembea kiwango kirefu cha kilometa 142 mpaka kwenye geti, maana yake tutakuwa tayari tumesha-cover kilometa 78. Niiombe vile vile Serikali, hizi kilometa zilizobakia 64 kutoka Mvua mpaka kwenye lango la geti la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nazo zipangiwe utaratibu wa kupangiwa fedha ili barabara ifike pale, kuwe na urahisi wa kuwafikisha watalii kule. Hifadhi ile vile vile ni mpya na ndani yake kuna mito mikubwa; kuna Mto Kilombero, kuna Mto Ruaha, kuna Mto Rukulunge, ningependa Serikali itenge fedha ili kuweza kujenga madaraja ili hifadhi hiyo iweze kuunganishwa katika maeneo yote na kuweza kuleta tija tunayoitaka.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kodi, ushauri wangu kwa Serikali, agizo la Mheshimiwa Rais la kusema kwamba TRA wasifunge akaunti, TRA wasirudishe kodi nyuma, hili kama kiongozi wa nchi ninachoona ni agizo kwa Bunge na ni agizo kwa Wizara husika ya Fedha. Hawa watu wa TRA wanaweza kuwa wanagombana na wafanyabiashara, lakini uhalisia wanafunga akaunti wanarudia nyuma kwa sababu kuna sheria ambazo wanazo ndiyo zinazowapa mamlaka ya kufunga akaunti au kurudia makisio ya wafanyabiashara katika miaka ya nyuma. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mwigulu kama Waziri lakini sisi kama Bunge, hizo sheria ambazo zinaonekana zinawapa mamlaka hao ziletwe Bungeni tuzijadili…

SPIKA: Mheshimiwa Kalogeris weka vizuri hicho kisemeo chako. Ahsante sana.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, nimesema, hizo sheria ambazo ziko zinazowapa mamlaka watu wa TRA kufunga akaunti, lakini vile vile kufanya marejeo ya zaidi ya mwaka mmoja kama matakwa ya Mheshimiwa Rais wetu ambaye anaona kwamba siyo haki, ziletwe Bungeni tuzijadili, tuzifanyie utaratibu na uhalisia ili ziendane na matakwa ya mama na pia ziendane na uhalisia wa watu katika kulipa kodi.

Mheshimiwa Spika, la pili, nimwombe Mheshimiwa Waziri kuna hili suala ambalo nalo ni kikwazo katika kusababisha madeni yawe makubwa kwa walipakodi. Kuna viwango ambavyo vinatengwa kwa Mameneja wa Mikoa kwamba Morogoro tufanye, unatakiwa utoe bilioni 200, je, kuna uhalisia na hawa wafanyabiashara waliokuwa hapo Morogoro? Matokeo yake nini? Meneja wa Mkoa kwa sababu anataka kuendelea kubaki kwenye nafasi ile atakachofanya ni kuendelea kubambikiza kodi ili abaki pale na tunaenda kuumiza watu wetu. Kwa hiyo ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, hebu waliangalie kwa undani, tunapofanya makisio mwaka huu inawezekana hatukufanya hivyo, lakini mwakani tunapofanya makisio, twende na usahihi wa wafanyabiashara wetu waliokuwa pale na uwezo wao wa kulipa kodi ili kodi ilipike na naamini dhamira ya Serikali kama mama anavyosema anataka wafanyabiashara walipe kodi na naamini wafanyabiashara wanataka kulipa kodi, ila kinachoonekana kodi inawabana kutokana na sheria ambazo tumezitunga.

Mheshimiwa Spika, kingine, mimi ni mfanyabiashara, kuna suala hili la kodi ya zuio ambalo wanatozwa wafanyabiashara, hakuna mfanyabiashara katika nchi hii naamini ambaye anapata zaidi ya 10% katika mradi anaoufanya. Leo hii mfanyabiashara mfano kwenye kandarasi za barabara, za ujenzi wa maji au ujenzi wa umeme, anapotoa certificate anakatwa kodi ya zuio ya 5%, maana yake nini? Kama ana bilioni moja atakatwa milioni 50 zinakaa TRA, muda wa kulipa kodi anaambiwa lete hiki, lete hiki, lakini mwisho wa yote anaambiwa kwamba haya unalipa milioni 30, milioni 20 ya zuio inaendelea kubaki kwenye TRA. Huku ni kuwarudisha nyuma wafanyabiashara, dhamira ya Serikali ni kujenga uchumi wa nchi, lakini kujenga uchumi wa watu wake vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi langu kwa Serikali, ikiwezekana tutoe zuio hili la kodi. Sasa hivi kama tulivyokwenda kwenye utaratibu wa kwenye mabasi na kwenye malori tunasema tutalipa milioni mbili, milioni tatu na kwa wafanyabiashara hawa wanaofanya kandarasi na Serikali tukubaliane tu kwamba faida atakayotegemea kuipata ni kati ya 10% na 15%, tufanye 12% tutengeneze utaratibu, huyu mfanyabiashara kila anapokatwa certificate katika madai yake ikatwe asilimia ya fedha zake, naamini tutaweza tukafika mahali, kama huyu mtu alikuwa alipe milioni 30 atalipa milioni 30 yote milioni 20 yake atabakia kujenga uchumi na kujipanua kibiashara ili afanye biashara zaidi, nchi ipate fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, niende sambamba na hii sheria wafanyabiashara wamebambikiziwa kodi kubwa sana wamerudishwa nyuma kwa miaka saba mpaka 10, matokeo yake nini ninavyosema? Sasa hivi wafanyabiashara wana kilio kikubwa nchini, kila mwezi wanaambiwa kodi ambayo imepita nyuma ambayo tayari alikuwa haijui, lakini kodi hiyo vile vile hailipiki, maana yangu nini kusema hailipiki? Huyu mtu anapochelewa kulipa anapigwa na riba, unapigwa riba kwenye kodi ambayo huijui matokeo yake kuna maumivu makubwa kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali mama amesema hataki kodi ya dhuluma, basi hizi kodi ambazo wafanyabiashra wamepigwa za dhuluma zifutwe ili watu wajenge uchumi, waanze kupanga upya, wakafanye kazi za biashara za kusaidia kuleta uchumi katika nchi yetu, au kama Serikali ikishindwa kuzifuta, basi zitoke riba na waambiwe walipe kidogo kidogo kuliko sasa hivi, umefungiwa akaunti, ghafla umeitwa unaambiwa ulipe milioni 20 kama vile fedha hiyo unayo ndani. Hii inaumiza na inafanya uchumi wa nchi wakati mwingine ushindwe kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nizungumzie kwenye suala la CSR (Community Social Responsibility), mimi natoka kwenye Halmashauri ya Morogoro Vijijini, kuna Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mradi ule ndani ya mkataba kuna kipengele cha 4% kupewa wananchi ambao wako kwenye Halmashauri ya Morogoro Vijijini na Halmashauri ya Rufiji, mpaka dakika hii hakuna. Nimejaribu kuliuliza kwenye RCC na hata kwenye ripoti ya CAG ilionekana fedha hiyo haijatoka. Kwa hiyo naomba wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up, atupe status ya jambo hili kiserikali, wananchi wa Halmashauri ya Morogoro Vijijini, wananchi wa Halmashauri ya Rufiji wana haki ya kupata fedha hii kwa sababu ni haki yao ya kisheria.

Mheshimiwa Spika, tuna matatizo ya ambulance, tuna matatizo ya barabara, tuna matatizo ya vituo vya afya, tungepata fedha hii kwa sababu katika trilioni saba ya mradi huu halmashauri zinatakiwa zipate bilioni 280, tukigawanya bilioni 140 katika halmashauri, kuna mambo makubwa yatafanyika. Upo uwezekano wasituletee ambulance na ikanunuliwa ambulance kupitia fedha hizo, wasitujengee vituo vya afya, tukajijengea vituo vya afya kupitia fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe Waziri, tumeliuliza kwenye RCC na kuna kipindi hata Mheshimiwa January alipokuja kwenye ukaguzi nilimuuliza, akasema Serikali inalifanyia kazi, tunataka tupate majibu, ni kazi gani ambayo Serikali inaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kufuta ada ya form five na form six. Ombi langu kwa Serikali kuna kundi kubwa la vijana linabakia, wanaomaliza form four ambao wanakwenda kwenye vyuo vya kati na vyuo vya VETA. Ombi langu kwa Serikali, kama tumeweza kufuta ada kwa huko, tufute vile vile ada kwenye vyuo vya kati, tufute ada kwenye vyuo vya VETA, tupate vijana wengi ambao watakwenda kusomea ufundi na kuja kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)