Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaomba nifanye marekebisho ya jina, naitwa Deodatus, ukipenda Deo.

Mheshimiwa Spika, nianze moja kwa moja kwanza kwa kusema kwamba, ninaunga mkono bajeti hii. Bajeti hii ni nzuri na niseme bila kificho nampongeza sana Waziri wa Fedha kwa kutuletea bajeti hii inayojaribu kuakisi wapi nchi hii inakwenda na wapi imetoka. Ni bajeti ambayo inajaribu kutilia maanani matatizo ya wananchi, inajaribu kuleta vilevile balance kwenye uwekezaji. Tumeona hatua nyingi za kikodi ambazo zimechukuliwa katika kuifanya sekta ya uwekezaji katika kilimo na viwanda iweze kuwa na hali nzuri zaidi, kwa hiyo nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais. Kwa kweli, kwa haya ambayo yanafanyika inaonesha kabisa ni uthubutu wa hali ya juu kabisa wa kutaka ku-address matatizo ya Watanzania. Tumeona mengi ambayo yamefanyika na hatuwezi kuyataja yote hapa maana muda hautatosha, lakini itoshe kusema nchi yetu imekuwa stable kiuchumi, macro-economic indicator zote zinaonesha tuko katika hali nzuri tunawazidi wenzetu majirani kwa kiasi kikubwa, inflation iko within reach katika single digit, Shilingi imeimarika, reserve ziko kwenye 4.8 na iko within reach. Haya yote ni maendeleo makubwa ni maeneo ambayo yanazidi kufanya uchumi uendelee kukua.

Mheshimiwa Spika, vilevile kipekee nipende kushukuru Serikali,kilio kikubwa cha wananchi ili kuwafanya wawe na hali nzuri tumeona Serikali imejaribu kuweka hiyo ruzuku katika mafuta ni jambo jema, lakini nipende kusisitiza na kusema kwamba, kama kuna eneo tutawasaidia wananchi ni kwenye mbolea.

Mheshimiwa Spika, tunaelewa fika kabisa Serikali ina mpango mahususi wa kutoa ruzuku kwenye mbolea. Niseme wazi kabisa wananchi wamepata matatizo makubwa sana kwa kulima bila kutumia mbolea, hasa maeneo ya kule Njombe, tunahitaji sana ruzuku ya mbolea. Na niombe sana Mheshimiwa Waziri aliwekee mkakati vizuri, Waziri wa Fedha ndiyo mtu ambaye sasa atatoa hizo fedha ili ziweze kwenda kwenye ruzuku. Kuwe na uratibu mzuri wa kuhakikisha ruzuku hii inawafikia wananchi kwa wakati na kusiwe na janja-janja ambayo itawafanya wafanyabiashara waweze kupata faida katika mwenendo wa ruzuku kwa hiyo, niombe sana jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Viwanda tulifanikiwa kutembelea baadhi ya viwanda na hasa tulitembelea viwanda vya chuma. Dhima ya bajeti hii ni kuwa na bajeti ambayo itafanya uchumi shindani, viwanda vya chuma kwa ujumla wake bado vina matatizo makubwa sana ambayo yanatokana na ushindani ambao hauko sawa au hauko linganifu.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kusema ni vizuri, na ninashukuru Mheshimiwa Waziri amechukua baadhi ya hatua nyingi za kikodi na za kiutawala ili kusaidia viwanda hivi vya chuma, lakini bado kuna maeneo ambayo naona yanahitaji kuangaliwa kwa karibu ili yaweze kusaidia katika kuimarisha sekta. Sekta hii inaajiri karibu watu elfu 10, watu elfu tatu moja kwa moja na waliobaki wote ni mawakala na watu mbalimbali. Vijana wengi, machinga, wako katika sekta hii ya chuma kwa hiyo ni sekta muhimu sana kwenye kutengeneza ajira.

Mheshimiwa Spika, pia kuna maeneo ya kodi ambayo yalitakiwa yabadilishwe na recommendations zilitolewa. Kwa mfano, ukiangalia HS Code 7210.3 na 722599 unaona bado eneo hili lipo duty kwenye 25. Ilipendekezwa iwe 35, sasa wale wanaoingiza bidhaa nyingine za chuma ambao wale wanatengeneza migongo tu, hawa wanakuwa na advantage kubwa katika biashara hii na kwa hiyo, wana-affect wazalishaji. Kwa hiyo, iko haja ya kuangalia kwa karibu sana.

Mheshimiwa Spika, kuna eneo moja kwa sababu ya muda niliongelee, ni eneo la kitu iinaitwa PED ambayo ni Pre-Engineered Design Structures. Hizi structures ni muhimu sana kwa kilimo, ni structures ambazo ndio wafugaji hutengenezea mahema, maghala, viwanda na show rooms. Hizi structures zinaweza zikaagizwa kirahisi na watu ambao wanazileta kwa sababu kodi iliyowekwa hapa inawa-encourage wao kuzileta badala ya kampuni zetu kubwa za chuma ambazo zingeweza kutengenezwa hapa. Kampuni hizi zilikuwa zimeomba zipewe remission kwenye suala hili ambalo haijafanyika, ningependa sana kumuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie lina-impact kubwa sana kwenye uzalishaji, kwenye kilimo na kwenye ufugaji. Kwa hiyo ni vizuri akaangalia hizo ni H Code 94062090.

Mheshimiwa Spika, nipende kuongelea kilimo, sisi wananchi wa Njombe ni wakulima wakubwa na tunashukuru sana kwamba kumekuwa na hatua mbalimbali ambazo zimepunguza baadhi ya kodi hasa kwenye misitu, sasa tunakwenda kwenye asilimia tatu ya cess, kwa hiyo hilo ni jema, tunamshukuru. Hata hivyo, tuangalie vile vile kwamba sisi tunalima chai kwa wingi sana pamoja na avocado. Njombe ina grow kubwa avocado hub lakini ukiangalia miundombinu na infrastructure bado iko nyuma sana.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi, nimeangalia bajeti ya Wizara ya Kilimo, nimeangalia bajeti hii, sisi Njombe tunahitaji kuwa na Uwanja wa Ndege kwa sababu kwenye bajeti tunaongelea ndege tano zitaingizwa au zimeshalipiwa, lakini katika hizo tano moja ni ya mizigo. Hiyo mizigo inatakiwa itoke Njombe, tuna hub kubwa sana ya uzalishaji wa parachichi na itakuwa ni hub kubwa sana huko mbele ambayo inahitaji usafiri. Katika mipango ya Serikali hatulioni kabisa hilo likijitokeza, kwa hiyo niombe sana liangaliwe tena upya na Njombe iweze kuonekana ikipewa eneo hili.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni Liganga na Mchuchuma. Limeongelewa sana sana katika Bunge hili, mara ya mwisho tulivyoongea tuliambiwa kwamba mazungumzo yamefikia mahali pazuri, wengine wangeweza kusema yamefikia patamu. Hata hivyo, kinachojionyesha ni mradi wa mkakati ambao hakuna mkakati wowote ambao upo kwa sababu hakuna taarifa tunazopewa kwamba mazungumzo yamefikia wapi. Mradi ule una Liganga na una Mchuchuma, Mchuchuma ndiko ambako kuna makaa ya mawe, makaa ya mawe bei yake imepanda. Sisi Watanzania ni watu wa ajabu, tuna makaa ya mawe ambayo bei yake ni nzuri, lakini bado tunafanya mchezo na mradi huu.

Mheshimiwa Spika, nasema ni mchezo kwa sababu hatuelewi umefikia wapi, tunafahamu Mungu ametupatia haya makaa kwa muda mrefu na makaa haya sasa yana bei nzuri sana. Shirika letu la Maendeleo ambalo limepewa hili jukumu la kuendeleza huu mradi, tunaona kwamba aidha, halina uwezo au watu wetu wanao-negotiate hawajafika mahali ambapo wanaweza wakatuambia tatizo ni nini? Tunahitaji kama Watanzania na wananchi wa Mkoa wa Njombe kuelewa Mradi wa Liganga na Mchuchuma umefikia wapi. Nimwombe Mheshimiwa Rais aweke mguu kwenye mguu huu kama alivyofanya kwenye masuala ya gesi na LNG ili mradi huu uweze kukwamuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu una tatizo lingine ambalo ni kwamba, tunafahamu kabisa Paris Climate Agreement inafikia mwisho 2030 sasa tuna makaa ya kuzalisha kwa miaka 140 kwa tani milioni tatu kila mwaka, maana yake tuna tani zaidi ya 428 lakini tuna miaka nane tu ya uzalishaji kama tungekuwa tumeanza kuzalisha leo. Kwa hiyo unaona bado tuko katika maeneo ambayo hatuoni kwamba tuna mali inayoweza ikawaondolea umaskini watu wetu mpaka leo. Niombe sana Serikali iliangalie hili kimkakati na isiliangalie hili kama jambo ambalo liko kwenye bajeti na halifanyiwi kazi yoyote.

Mheshimiwa Spika, niongelee kwa haraka haraka Sekta ya Madini kama muda utaniruhusu. Nimemsikia Profesa Kabudi akiongelea, ukiangalia sekta hii uzalishaji wake umepungua katika bajeti hii kwa kiasi cha asilimia 7.2. Ukweli wa mambo ni kwamba ni kweli tulifanya mambo makubwa, tukabadilisha sheria zetu, lakini baada ya miaka mitatu ni wakati sasa wa kuziangalia hizo sheria kwa makini zaidi kwa sababu tulifanya haya mambo kwa haraka na kulikuwa na sababu za muda kwa nini yalifanyika yaliyofanyika, lakini ukweli ni kwamba wawekezaji walio wengi wakati na wa juu na hata wadogo bado wana matatizo makubwa sana. Sekta hii haikui kwa sababu moja hakuna migodi mipya na migodi ambayo itakuwa mipya inaongelewa pengine itafunguliwa 2025 ambayo utafiti wake ulifanyika zamani. Hakuna utafiti unaofanyika sasa hivi especially kwenye maeneo mapya ya green field.

Mheshimiwa Spika, vile vile financing kwenye Sekta ya Madini imekuwa ni ngumu kutokana na sheria ambazo zipo. Hatusemi hizi sheria zote ni mbaya, tunasema tukae chini tuangalie upya na ikiwezekana watu waziangalie hizi na jicho lingine, kwa sababu hasara mwisho wa siku ni kufanya utafiti ili uweze kuzalisha, ili uweze kuwasaidia wananchi wako kuondoa umaskini. Sasa kama hatuwezi kufanya hivyo, tunashukuru kwamba tuna sheria ambazo ukizalisha tuna uhakika na sisi tutapata kitu fulani kwa maana ya hizo hisa.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye regulations mbalimbali za local content zinaongelea masuala yote ya procurement. Kwenye Serikali tumeanza kuangalia upya procurement kwa kiasi gani inazuia au inachelewesha miradi mingi, hata huku kwenye madini kuna hayo matatizo. Mfumo mzima wa manunuzi unatakiwa uangaliwe upya, ni vizuri kuwa na local content lakini tuiangalie isiwe na athari kwenye uzalishaji. Tumepunguza mapato kwenye Sekta ya Madini moja ya sababu ni kwa sababu uzalishaji umepungua. Uzalishaji umepungua kwa sababu kuna drawbacks nyingi katika mfumo, kwa hiyo kuna economics sense, kuna legal sense ya kuweza kuangalia upya. Ukiangalia kwa mfano sheria inayozungumzia participation ambayo Profesa ameiongelea, ni sheria inatupa Serikali 16%, ni jambo jema, jambo lenye afya, lakini wording ya section inayoongelea suala hilo, ukiangalia kwa makini sana ina ambiguity na kwa mwekezaji mpya yoyote akiisoma anaangalia kwamba inaweza ikawa interpreted kwamba hata ukiomba mkopo na mkopo ule ukiwa unarudishwa au ukiomba financing aina yoyote ikiwa inarudishwa, Serikali inatakiwa ipate 16% ya mkopo unaorejeshwa ndiyo sheria ilivyoandikwa na ndiyo ambavyo inaweza ikawa interpreted.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mtu ambaye yuko nchini anaweza akaliangalia aka-assess risk akaona ni sawa, lakini kwa mtu ambaye anataka kuja Tanzania, anataka kutafuta fedha awekeze, atakuwa na kigugumizi kikubwa kuendelea kufanya kazi au kuja kukiwa na ambiguity kama hiyo.

Mheshimiwa Spika, ameongelea pia ring fencing, ni tatizo lingine kubwa, ni kitu kizuri kilifanyika katika Sheria ya Madini lakini kilifanyika katika Sheria ya Kodi ya mwaka 2004. Ring fencing ina-apply vizuri na ina-make sense pale ambapo una uzalishaji, ukiweka ring fencing kwenye exploration ni kwamba unaua utafiti, hakuna mtu anakuja kufanya utafiti asiweze ku-recover gharama zake. Kwa hiyo ni vizuri tukawa sober, tukarudi nyuma kidogo, tukaangalia haya mambo kwa jicho lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)