Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpangao wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpangao wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, niseme kwamba Wizara yetu mpya ya Mipango mahali ambapo mipango yetu inapaswa kuanzia kwa mwakani na Wizara mpya ni kuangalia mipango yetu tuliyojiwekea ambayo ipo kwenye vision 2025. Muhimu hapo inasema kwamba tunataka kujenga uchumi shindani halafu ifikapo 2025 pato letu la Taifa ukiligawa GDP per capita kila mtu apate dola 3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba mipango hii lazima iwe na sura mbili. Kwanza mipango na uwekezaji ambao matunda yake yatapatikana kwa haraka sana ndani ya mwaka mmoja au miwili; halafu mpango na uwekezaji ambao matunda yake tutayaona baada ya miaka mitano na kuendelea. Sasa uchumi wetu kwa muda mrefu umekuwa kati ya asilimia tano na asilimia sita. Imedhirika kwamba ukuaji huo wa uchumi ambao tumekuwa nao kwa miaka kati ya miaka 20 na 30, haujaweza kuondoa kwa kasi kubwa umasikini nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mipango yetu ni lazima ijielekeze kwenye uchumi unaokua kwa zaidi ya asilimia sita. Duniani kote wamepiga hesabu, uchumi huo lazima ukue kwa kati ya asilimia nane mpaka asilimia kumi. Cha pili, ikifika mwisho wa mwaka huu GDP per capita yetu itakuwa dola 1,113. Bado tupo mbali sana kwenye malengo ya dola 3,000. Mpango wetu lazima ujielekeze kwenye kufuta umaskini. Mipango lazima ifute umaskini na uwekezaji lazima ufute umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya sasa umaskini nchini mwetu ni kwamba takwimu zinaonesha asilimia 18.7 ya Watanzania hawa wapo below food poverty line, matatizo ya chakula asilimia 18.7. Kwa matumizi ya kawaida, basic needs yaani poverty line ukichukua umaskini kwenye hiyo ngazi ni asilimia 35.7. Ukichukua umaskini wote kwa nchi nzima unakuta asilimia 13, mijini watu siyo maskini; asilimia 87 vijijini ni maskini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mipango yetu ijielekeze kwenye miradi ya kufuta umaskini. Bado tuna mipango ya malengo ya Kimataifa. Niliona hapa wengine wanaongelea utajiri, hili nadhani tusiliweke huko, hatujafikia huko. Kuna tofauti ya utajiri na mtu kuwa na kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mapendekezo yangu ni haya; uchumi wetu ukue kati ya asilimia nane mpaka kumi na maeneo ya kukuza huo uchumi, la kwanza tuwekeze kwenye uchumi wa gesi za aina tatu; ile gesi asilia halafu Helium, Carbon Dioxide na gesi nyingine. Kwa hiyo, miradi yetu ingeeleza sana kwenye fedha za haraka kutokana na uchumi wa gesi, halafu kwenye madini tukiacha dhahabu kuna madini ambayo yana thamani na yanahitajika sana duniani na huko tuwekeze. Mahali pengine penye kupata mapato ya haraka sana ni kwenye kilimo, uvuvi, ufugaji na utalii. Kwa hiyo, hivi ndiyo vyanzo vya vipaumbele vya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mpango tulionao, mimi napendekeza, haya yote ili yafanikiwe lazima tuwe na haya yafuatayo: Lazima tuwe na elimu bora kwa ngazi zote. Ni kwamba, tumetengeneza sera ile ambayo itaanza 2027. Hata hivyo nina wasiwasi kama Halmashauri zetu na Mabaraza ya Madiwani, yanaweza yakasimamia utekelezaji wa hiyo sera. Kwa hiyo, elimu bora maana yake ni kwamba tupate walimu na wakufunzi walio bora. Lazima tupate vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia kama maabara na libraries. Kwa hiyo, mipango yetu lazima iangalie nchi ambazo zimefanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi nyingine huko duniani ningechukua nchi tatu; South Korea, Finland na Uingereza ambao tumerithi mtindo wao wa elimu. Kwa Afrika hapa kwa elimu bora sisi hatujawa hata kwenye tano au kwenye nane bora. Kwa hiyo, ya kwanza ni South Africa, ya pili ni Kenya, ya tatu ni Botswana. Hebu tujifunze kwa nini wao wanasemekana kuwa na elimu bora? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili, kwenye mipango yetu na ambacho sidhani kama kimewekewa sana mkazo, ni mambo ya utafiti na ubunifu. Hakuna Taifa lolote ambalo linasema lina mipango mizuri ya maendeleo bila kuwekeza kwenye research development na innovation. Mpango wetu lazima uoneshe maeneo ya kipaumbele (focus areas). Mimi ningechukua upande wa kilimo, seed science na technology; ningechukua space science halafu ningechukua nuclear science na life sciences kwenye mambo ya matibabu na kadhalika. Mipango yetu lazima iseme hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mipango yetu nayo ituoneshe tuna watafiti wangapi? Tuna wataalamu wangapi? Kuna viwango vinatolewa Kimataifa kwa watu 1,000 walioajiriwa, sisi tuna wangapi? Kwenye Bajeti ya Utafiti, vilevile lazima mipango yetu iongoze bajeti. Inasemekana kwamba mwaka 2022 Tanzania tumetumia dola milioni 870, lakini majirani zetu Kenya wametumia bilioni mbili. Dunia utafiti umetumia zaidi ya trilioni 2.5. Kwa hiyo, unaona jinsi ambavyo mipango yetu haijaweka mkazo kwenye mambo ya utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mbali ya hayo, lazima twende kwa vitu ambavyo Watanzania wanavihitaji kila siku. Hapa nachukua vinne tu. Watanzania Mipango yote tunayojadili wanataka wapate chakula, wanataka maji, wanataka umeme na wanataka matibabu. Kwa hiyo, mipango yetu ishughulikie hayo. Kwa mfano, suala la chakula ni lazima tujue miaka 10 au 20 ijayo tunahitaji chakula kiasi gani? Hili tumeliongelea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni maji. Kipimo hapa ni washauri. Hiyo ya kusema kijiji, wilaya fulani imefika asilimia 70, siyo kipimo kizuri. Hicho ni kipimo cha fursa, lakini kipimo kizuri ni kile ambacho mtu anatumia maji kiasi gani kwa mwaka? Hicho ndicho kipimo kizuri cha kitaalamu, lakini kile cha fursa, maji yanaweza kuwa mjini, maji yanaweza kuwa kijijini, fursa inasema asilimia 70 au 80, lakini ukija kwenye utumiaji, unakuta ipo chini kabisa. Kipimo cha kitalaamu hapa wanakiita Water Stress Indicator, yaani eneo ambalo mwananchi mmoja mmoja kwa mwaka hatumii zaidi ya lita 1,000,000. Duniani huko kitaalamu inasemekana kuna matatizo hapo. Kwa hiyo, ripoti za kusema tu asilimia 70, haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni umeme. Haya yote yapo kwenye document ya UN, Sustainable Development Goals, yapo African Union ambayo Waziri alisema wametumia kama hili la umeme ni SDG Seven. Sasa umeme nao tatizo ni hilo hilo, mtu anasema sehemu fulani ni asilimia fulani, lakini siyo kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je ukisema kwamba Musoma Vijijini, kijiji changu kimoja asilimia 75 wanapata umeme, hiyo ni fursa kwamba umeme umekaribia, umesogea lakini kipimo kizuri ni umeme kiasi gani ambao mtu anautumia kwa mwaka. Kwa hiyo, mbali na kutoa hizi asilimia Waheshimiwa Wizara mbalimbali lakini waende mbali sana watoe na umeme kiasi gani. Sasa hapa nitakuonesha jinsi ambavyo utumiaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia dakika moja.

PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, unachukua nchi tajiri Africa ni Seychelles umeme wanaoutumia watu kwa mwaka ni unit 4,640 na GDP yake ni zaidi ya dolla 17,000. Unakuja unachukua majirani zetu Kenya, umeme wanaotumia kwa mwaka kwa unit ni unit 180, GDP yao per capital ni zaidi ya dola 2,000. Unakuja Tanzania, umeme tunaoutumia zile zero-unit ni 99.6 na GDP yetu ni karibu dola 1,100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba labda nirudie kwa kusema tuwe na mipango ambayo tukiwekeza kwenye kilimo, kwenye uvuvi na mifugo tutapata mara moja lakini tuwe na mipango ya kuwekeza vilevile kwenye mabarabara na reli ambapo mapato yake yanaweza kupatikana baada ya muda mrefu. (Makofi)