Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, napenda kushukuru kwa kupata nafasi hii niweze kuchangi machache katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda nimpongeze ndugu yangu Waziri Mchengerwa kwa kazi kubwa anayoifanya, na Naibu Waziri dada yangu Pauline Gekul, Katibu Mkuu, Dkt. Abbas, Naibu Katibu Mkuu, Bwana Saidi Yakubu na timu yote ya Wizara na pia sitamsahau Mkuu wa Chuo changu cha Bagamoyo TaSUBa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi za pili ziende kwa mama yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya Royal Tour. Jambo la Royal Tour Mheshimiwa Rais amelianzia pale Bagamoyo na jambo lolote likianza Bagamoyo basi mambo yake yatakuwa mazuri kabisa na mnaona kabisa idadi ya utalii imeongezeka sana katika nchi yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nazungumzia suala la Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo au Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Chuo hiki cha siku nyingi sana lakini kazi kubwa sana chuo hiki imekifanya na viongozi waliyoko pale wanaendelea kudumisha na kuhakikisha kwamba kazi kubwa iliyokuwa inafanyika inaendelea kuwa nzuri. Mwaka 2021 kulikuwa na Tamasha la Sanaa Bagamoyo tarehe 28 mpaka 30 Oktoba, lilifanyika mwaka jana. Tamasha hili kwa kweli lilikusanya watu wengi sana; wa ndani na wa nje ya nchi, makadirio ya Wizara wanasema kama watu 75,000 lakini mimi ninasema zaidi ya 100,000; yalikuwa makadirio madogo sana. Kwa kweli chuo hiki kinafanya kazi kubwa na chuo hiki kinaitangaza nchi yetu, kwa mfano mwaka 2021 Chuo cha Sanaa Bagamayo wamechukua Uni Award ya mwaka 2020/2021 wameingia nusu fainali. Mwaka huo huo 2021 katika Uni Talent katika suala la kuimba wameingia fainali, katika Taifa Cup, katika masuala ya bongo fleva wameshika nafasi ya kwanza, katika Uni Talens ya 2022 katika suala la kuimba wameshika nafasi ya kwanza na vilevile wameiwakilisha nchi katika suala zima la kuhamasisha Royal Tour kule Marekani, wamefanya maonesho kadhaa.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema Mheshimiwa Waziri hiki chuo kinatakiwa kiangaliwe kwa jicho la tatu, siyo macho mawili; maana yake ni chuo ambacho kinafanya kazi kubwa sana. Nimeona katika bajeti ya mwaka huu 2022/2023 chuo kimetengewa shilingi milioni 550 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kufundisha, kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu, mabweni, ukumbi, jengo la maji safi, maji taka, kununua vifaa vya uzio, kununua vifaa vya tv, kununua vifaa vya redio na kuweka mtambo wa redio pale. Kwa hiyo hivi vitu naomba Mheshimiwa Waziri, kama mmedhamiria kuvifanya mvifanye kweli kweli kwa sababu hiki chuo kinatembelewa na watu wengi na hiki chuo kimefundisha wageni wengi sana.

Mheshimiwa Spika, miaka iliyopita mpaka wazungu walikuwa wanacheza ngoma pale, wengi kabisa, kabisa, wanakuja wanajifunza. Mimi hiki chuo natamani kukiita Chuo cha Kimataifa cha Sanaa Bagamoyo kwa sababu ni chuo ambacho kinatambulika dunia nzima na kazi kubwa inafanyika na waliopo pale viongozi wangu wanafanya kazi kubwa sana. Naomba Mheshimiwa Waziri hebu jaribu sana kuongeza bajeti hii ya hiki chuo ili kiweze kuwa bora kiweze kushindana kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia, Mheshimiwa Waziri siku moja ulinidodosea na tulizungumzia kuhusu sports arena na ukanihakikishia siku moja ungeweza kufanya mpango tukapata sports arena pale Bagamoyo. Kwa sababu kuna Chuo cha Sanaa pale, kuna utalii Bagamoyo, ni jambo la msingi lile wazo lako kwa sababu sijaliona katika bajeti yetu ya mwaka huu. Naomba liwepo Bagamoyo ipatiwe sports arena kwa sababu ni sehemu ambayo ina utalii wa hali ya juu sana ukichukia na Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo pale cha Utamaduni, ukichukua na vivutio vya kitalii basi mkiweka sports arena pale mambo yatakuwa mazuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, niipende sana kuipongeza timu yetu au timu zetu za Serengeti, timu za wanawake kwa kazi kubwa wanayoifanya, nizipongeze timu zote za mpira wa miguu Tanzania, niipongeze klabu ya Yanga kwa hatua nzuri ambayo wanaendelea nayo, wanafanya kazi kubwa. Na nawaomba wakaze msuli kwamba baada ya kuchukua kombe mwaka huu lisitoke ndani ya miaka nane mpaka tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)