Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kuweka senti 50 zangu kwenye bajeti ya Wizara hii ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ndugu yangu Sharifu wa Kipumbwi kule Pangani Jumaa Hamidu Aweso anasema asiyeshukuru kwa kidogo, hawezi kushukuru kwa kikubwa. Nitambue mchango mkubwa na kazi nzito inayofanywa na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwenye Wizara hii; ndugu yangu Waziri, Mohamed Mchengerwa; Naibu Waziri, dada yangu Pauline Gekul; Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbas; na ndugu yangu Said Yakubu, Naibu Katibu Mkuu ya kuitafsiri dira na maono na huruma za Mheshimiwa Rais kwa wanamichezo, wanasanaa na wanautamaduni wa nchi hii. Kazi nzuri wanaifanya na kusema kweli tunaiona na tunawashukuru sana na ushirikiano wanaotupa ni Mungu tu anayeweza kuwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo kadhaa ambayo napenda kuchangia, kwa hiyo, muda usipotosha mengine nitayaweka kwenye maandishi. La kwanza kabisa ambalo sitaki kuliweka mwisho, usije muda ukaniishia na sijalisema ni hili suala la mirabaha. Kusema ukweli kazi nzuri imefanyika, kazi nzuri imefanyika na hasa kwenye uthubutu. Mirabaha hii siyo mara ya kwanza kugawiwa, lakini mara ya mwisho iligaiwa mirabaha ya mwaka 2018 na kabla ya hapo ilikuwa ya 2014. Kusema ukweli kuna mazingira mengi ambayo yalikuwepo, yalikuwa yanafanya mirabaha ishindikane kugaiwa, lakini pia yalikuwa hayawezi kurekebishwa kama hatutaanza kuigawa, yaani ile lazima mvua inyeshe ndio tujue wapi panapovuja. Sasa hivi mvua imenyesha, tumejua wapi panapovuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa pamoja na kuwa na complain, complain, kutoridhika kwetu kuhusiana na ugawaji wa mirabaha ile, nani kapata kiasi gani, kwa nini na vitu vya namna hiyo, lakini niwapongeze kwa uthubutu ule. Shida yangu kwenye mirabaha ni namna ambavyo tunaifanya tokea mwanzo, ukusanyaji na ugawaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze mwanzoni kabisa, mirabaha iko kwa mujibu wa sheria. Sheria ya Hati Miliki na Hati Shiriki, Sheria Na.7 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2003. Moja ya vitu inachosema ni kwamba maeneo yote ambapo yanatumia kazi za sanaa, yanatakiwa kulipa mirabaha. Maeneo ambayo kusema kweli yanatumia kazi za sanaa yako mengi, hoteli, buses, hair saloons na barbershops, restaurant, cafe, bars and social clubs, radio na televisions, shopping malls, medium size shops, night clubs, telecommunication companies na music festival. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa safari hii COSOTA wamegawa Shilingi milioni 321 na mirabaha ilikuwa haijagaiwa toka mwaka 2018. Kwa hiyo, hiyo milioni 321 hii ni ya miaka minne, ndio tafsiri yangu. Nikajaribu kuchukua effort kupiga simu kwa watu wetu TRA watusaidie kujua sehemu ambazo COSOTA wanatakiwa kuchukua mirabaha. Kusema ukweli tumeshindwa ku-capture kila kitu, lakini beverage servicing activities ziko 3,009 nchi hii. Passenger land and transport ziko 66,738, restaurants mobile food activities ziko 30,957, urban and sub-urban passenger land transport ziko 1,347. Jumla ni biashara ambazo zimesajiliwa TRA ambazo zinatakiwa kulipa mirabaha 102,051. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii milioni 321 ambayo tunasema ni mirabaha ya miaka minne kwa biashara 102,051 inamaanisha biashara hizi zote zimelipa shilingi elfu tatu tatu kwa miaka minne kutumia kazi za sanaa. Yaani nafikiri hii ni sahani ya chipsi mayai kwa Edo pale. Watu wamelipia kupiga muziki, kutumia kazi za sanaa kwa miaka minne bila kipingamizi, anapiga mtu yoyote, saa yoyote 24 hours a day kwa siku 365. Sasa unaweza kuona jinsi ambavyo COSOTA haijaanza kufanya kazi yake. Ninachojaribu kufanya, ni kulinganisha ile scope ambayo COSOTA wanakusanya na ile potential ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, biashara hizi kama ambavyo zingelipa Sh.30,000 tu ambayo ni Sh.2,500 tu kwa mwezi ambayo hamna mtu yoyote anayeweza kukataa kati ya hawa kulipa, bado tungekuwa na mara 10 ya kiwango ambacho COSOTA wamekikusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kusema ukweli sheria inasema waziwazi kwenye marekebisho ya mwaka 2003 na nikisoma kipengele cha tatu inasema: “No person shall hold a public performance or a broadcasting of a work in which a copyright subsists except under a license issued by the society.” By the society wanamaanisha COSOTA.

Mheshimiwa Spika, sasa swali la kwanza kuwauliza ni kama COSOTA wametoa leseni za sehemu hizi 102,000 ambazo ni wazi zinatumia kazi za mziki. Kama hawajatoa kwa miaka 23 toka sheria hii ilipotengenezwa, ni wazi COSOTA hawajaanza kufanya kazi yao. Kiwango tunachokusanya hakijafika hata asilimia tano ya hasa ambacho tulitakiwa tuwe tunakikusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria iko wazi haijamumunya maneno, you pay to play as you want na hicho ndio ambacho kinatakiwa kufanyika. Kwa hiyo, kazi za muziki, kazi za sanaa zinatumika na hakuna anayelipa. Maeneo haya yote ya biashara ninayokwambia, OSHA wanakusanya chao, NEMC wanakusanya chao, TRA wanakusanya chao. Watu pekee ambao hawalipwi kutokana na shughuli hizi za kibiashara zinazofanyika ni wasanii wa nchi hii. Sasa unaweza kuona na sheria iko wazi, yaani siyo kitu ambacho tunaenda kuifanya sheria tukae tena tutengeneze sheria upya ama nini. Sheria iko wazi inasema, kwa hiyo, kuna mtu tu hafanyi kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hoja yangu ni kwamba, kwa mujibu wa maelekezo ya sheria, kiwango tunachokusanya ni kidogo sana na tumejaribu kuongea na COSOTA miaka nenda, miaka rudi kujaribu kuwaelekeza hili kuhusiana na uwezekano wa ku-outsource shughuli hii ili watu wengine waifanye. Hata kama ikibidi ku-privatize moja kwa moja, halafu COSOTA ikawa inalipwa kutokana na makusanyo kwa kiwango wanachokiweka, ingekuwa sawa. Serikali inapoteza pesa nyingi na wasanii wanapoteza pesa nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama Serikali haitaki kukusanya hela yake, wasanii wanataka kukusanya hela zao. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri, akae chini upya na COSOTA, waseme maeneo yote ambayo yanatakiwa kukusanywa mirabaha, wana mpango nayo gani na kama kwa miaka 23 wameshindwa kufanya shughuli hii, wanatuambia nini sababu ambayo itafanya shughuli hii isiwe outsourced na maeneo haya yakaanza kukusanywa na watu binafsi wengine kwa sababu wao shughuli hii imewashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hili ndiyo eneo ambalo lina pesa nyingi kwenye Wizara yake kuliko maeneo yote. Tulijaribu kupiga hesabu maeneo yote kwa ka-research kadogo ambacho siyo rasmi sana, tulipata tunaweza kukusanya takribani bilioni 56 kwa mwaka. Bilioni 56 kwa mwaka Waziri anajua ni kodi ya kiasi gani ya Serikali, anafahamu ni hela ngapi kwa wasanii. Uzuri wa royalties ni kwamba hata wasanii kama wameacha kufanya muziki, familia zao zinaweza kufaidika hata kama wao hawapo duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii familia ya Mzee wangu Waziri Ally, familia ya Remmy Ongala, Marijani Rajabu zingekuwa zinalipwa kwa pesa hizi, lakini baadae unapata malalamiko kuna mtu royalties amepata Sh.50,000 kwa sababu tu COSOTA wameshindwa kufanya kazi yao. Hii siyo ramli, hizi ni hesabu na hiki kitu kiko wazi kabisa kwa mujibu wa sheria, hatuhitaji kupita kokote ili kukifanya kitokee. Hilo ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tarehe 31 mwezi uliopita, Mheshimiwa Rais alihudhuria concert ya hip hop pale Dar es Salaam na moja ya vitu alivyosema ni kuhusiana na umuhimu wa kuanza kukusanya blank tape levy na aliisema hii kwa nia njema kabisa. Blank tape levy ni ile tozo ambayo inatakiwa kuchajiwa kwenye vifaa vyote ambavyo vinaweza kubeba kazi za sanaa kama flash disks, memory cards na CDs wakati vinaingia tu. Tukichukulia kwamba asilimia 90 ya vifaa hivi vinakwenda kutumia kuhamisha shughuli za sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hatuna teknolojia, hatuna human resources ya kutosha ya kuanza kupita sehemu moja moja kuhakikisha kila ambaye anahamisha muziki, anahamisha shughuli ya sanaa tunamchaji. Kwa hiyo, namna pekee ambayo tunaweza kufanya ni wakati vifaa vile vinapoingizwa kwenye nchi hii tunaongeza katozo kidogo ili wasanii wa nchi hii nao wakafaidika kwa kazi zile zinazokwenda kuhamishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja nimalize.

SPIKA: Sekunde 30.

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa hivyo, Mheshimiwa Rais ameliweka wazi hili. Pamoja na ile kazi ya COSOTA ambayo tunamwomba Mheshimiwa Waziri akahakikishe inafanyika ya makusanyo, lakini kwenye blank tape levy kwa sababu maelekezo ya Rais ni maagizo tayari, imeshakuwa sheria. Nategemea hili kuliona linaaanza as soon as mwezi Julai na ndugu yangu Mheshimiwa Mchengwerwa asipolifanya hili tunarudi kumsemea kwa Mheshimiwa Rais kwamba amepuuza maelekezo yake. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine nitauweka kwenye maandishi kwa sababu nina mengi ya kusema na muda haunitoshi. Nakushukuru sana. (Makofi)