Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHADIJA S. TAYA: Bismillah Rahman Rahim.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa leo afya njema ya kusimama katika Bunge lako tukufu kuzungumza masuala ambayo yanaenda kustawisha maisha ya vijana wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais sana na siyo kinafiki. Tuzungumze ukweli, Royal Tour siyo kitu ambacho kinaenda kunufaisha utalii peke yake, Royal Tour inaenda kunufaisha wasanii wa Tanzania hii. Mama alipoenda Marekani, alitembelea Paramount Studio. Katika hii studio amezungumza na watu masuala ya kuwekeza Tanzania kupitia hiyo hiyo Royal Tour.

Mheshimiwa Naibu Spika, mama alipoenda Los Angeles amekutana na wadau zaidi ya 15. Hawa wadau wamejadili mambo tofauti tofauti, wanakuja hapa Tanzania na amezungumza nao kabisa kuhusu fursa zinazopatikana hapa nchini. Leo hii mama anatuletea wasanii wakubwa ambao wanaweza kutuletea maendeleo katika hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachana na hayo, mama pia katika mtu ambaye ametengeneza hii Royal Tour anaitwa John, yule jamaa Producer, amekuja Tanzania, amezungumza na wasanii, amefanya kikao na wasanii tarehe 29 Aprili, ameona changamoto gani ambazo wanapitia na kadhalika ili waboreshe kazi zao katika maeneo tofauti tofauti. Mama anaupiga mwingi sana. Jiulizeni sisi tunaupiga wapi? Umeuliza swali zuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuipongeza timu ya Serengeti Girls na pia niipongeze timu ya Tembo Warriors. Pia naomba niwaambie kwamba tunahitaji timu za makundi maalum ziendelezwe vizuri. Tunahitaji timu hizi za makundi maalum waanze kuwa na maslahi mazuri, kwa sababu katika upeo wangu sasa hivi naanza kuona hizi timu ndiyo zinazotutangazia nchi yetu vizuri, na sasa hivi tumesaini mkataba wa masuala ya usawa wa kijinsia. Tunaomba maslahi ya hawa wanatimu ambao wanaenda kwenye kutuwakilisha katika nchi nyingine huko, maslahi yawe sawa na hizi timu za wanaume ili tuweze kutimiza masuala ya usawa wa kijinsia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakienda kwenye hotels, wasifikie huko uchochoroni, Hapana. Waende kwenye hoteli, kama ni Four Stars au Serengeti Boys au Taifa Stars nao pia waende huko. Kuwe na bajeti nzuri ambayo itasaidia hawa vijana, kwani watajitoa sana na wanaumia sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie suala hili sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna timu hizi za watu wenye ulemavu, tunazisaidia vipi? Naomba nimwambie leo Waziri, kuna timu imekuja hapa Tembo Warriors tayari wanaenda kuwakilisha Kombe la Dunia, lakini kuna timu ya Albinism Sports Club ambao nao wanaenda Kenya keshokutwa hapa kwa ajili ya kuwakilisha nchi. Sasa tunazisaidiaje hizi timu? Tutafute namna yoyote ile ambayo Wizara na Bunge lako Tukufu zisaidie hizi timu ili ziweze kwenda kuwakilisha michezo hii ili tuweze kukuza hii nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze kuhusu masuala ya muziki pia leo. Kaka yangu hapa Mheshimiwa Babu Tale amezungumza sana kuhusu BASATA na COSOTA. Naomba niwaambie jambo moja, msanii mpaka mnamwona amefika pale, amepitia mambo mengi sana; anapitia changamoto nyingi sana. Ukizingatia kwamba huyu msanii hana pesa, hana capital ambayo inamwezesha kufanya hizi kazi zake. Kwa hiyo, wanapitia kwenye changamoto nyingi hapa katikati kiasi kwamba zinaondoa yale maadili ya Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo hii msanii ameshakuwa hivyo: Je, Serikali mnafanya nini? Kazi yenu kubwa ni kutoa elimu siku hadi siku ili hawa watu tuweze kuwa-shape, wajue sasa kwamba wanaenda kuwakilisha nchi. Tuwa-shape wawe wasanii wazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukisema tu msanii amekosea, amevaa vibaya, hujamtengeneza au hujamkuza vizuri au hujamlea vizuri, hujampa elimu vizuri, unamfungia kazi yake. Hivi mnafahamu tunatumia gharama kiasi gani kutengeneza hizi video? Hivi mnafahamu tunatumia muda kiasi gani ku-invest kwenye hizi videos? Hivi mnafahamu vyote hivi? Hamfahamu! Sisi ndio tunafahamu ndiyo maana leo hii tulipambana kuja humu Bungeni tuwazungumzie wananchi wetu waliotuleta humu Bungeni, lakini tuzungumze juu ya masuala ya sanaa ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii umemsikia pale Mheshimiwa Riziki Lulida hajaniita Mheshimiwa Khadija, ameniita Mheshimiwa Keisha. Hilo ndiyo jina ambalo linatambulika katika nchi hii. Hili jina halikuja hivi hivi tu, limekuja kwa juhudi.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa taarifa kwa mwongeaji kwamba mambo yote yanayotokea, kwa kweli wanatakiwa Wizara hii pamoja na yote waelezee kwamba wameshawatafutia masoko ya kazi zao wasanii hawa katika maeneo au nchi ngapi? Watupe idadi. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taarifa hiyo.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Sijaielewa taarifa. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Haya tuendelee. (Makofi)

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa ni kwamba wasanii tunatumia muda mwingi sana kutengeneza majina yetu ili tufike pale tunapopataka. Tunatumia investment ambazo hatujui hata namna ya kuzipata lakini tunazipata. Sijui mnanielewa! Hatujui hata namna tunavyozipata, lakini tunazipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kutumia hizi changamoto tunazopitia, sometimes tunakuwa frustrated, tunahitaji elimu, tunahitaji semina nyingi, nyingi. Kwa hiyo, naomba hii Wizara ikiwezekana, mwakani mwongeze bajeti ya kuwaelimisha wasanii, na sio wasanii kubwa peke yake, mwende Tanzania nzima kutoa elimu kwa wasanii ili wajue namna gani wanazifanya kazi zao vizuri katika maadili ya Kitanzania ili tuweze kutangaza nchi yetu Kimataifa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu leo hii kuna wasanii jamani wanafanya kazi. Hii ni kazi kama kazi nyingine. Mfahamu hilo, hizi ni kazi kama kazi nyingine. Kuna wasanii wamesoma katika hii nchi. Kuna wasanii wamesoma; Nanji amesoma, Billnass amesoma, Zuchu amesoma India Advance Diploma ya Business, Saraphina amesoma Petroleum Chemistry Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na leo hii ni msanii pale amesimama, Mwana FA ana Masters ya Uingereza, ana Degree ya pale IFM, mimi nina degree ya pale CBE. Tumesoma, msitudharau. Msione kama vile katika hii nchi hatuna mchango wowote. Tuna mchango mkubwa sana, na leo hii tunazungumzia kila siku hapa masuala ya ajira, sijui ajira ndogo, ajira nini! Tukiweza kutengeneza vijana vizuri vijana humu ndani, nawambieni suala la ajira litakuwa ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kila nyumba kuna msanii mmoja, katika kila nyumba, kuna wanamichezo, tunataka nini tena? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)