Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii adhimu. Kwanza nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na timu nzima, lakini nimpongeze zaidi Mheshimiwa Rais kwa kuwateua watu hawa kwa sababu naamini kabisa yeye ana maono, ameona kwamba watatuvusha katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwa kuangalia kwenye suala la mikopo zile asilimia 10. Kuna hili suala la asilimia 10 kuna suala la umri ambao umri wenyewe unaanzia miaka 18 mpaka 34. Hiki kipindi cha sasa kwa umri ule wa nyuma uliokuwa unaanzia miaka hiyo ilikuwa ni sahihi, lakini ukiangalia mbele zaidi vijana wa sasa mpaka miaka 45 bado ni vijana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia miaka 18 mpaka hii miaka 34 wengi wao wanakuwa ni wale vijana ambao bado wanatabia zile zinaitwa tabia za utoto zaidi. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Kwa hiyo, ukiangalia kuanzia hapo miaka 36 mpaka miaka 45 kundi hili ndiyo kundi ambalo lina maono kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi binafsi ningeishauri Serikali basi iongeze umri kutoka umri ule wa miaka 18 mpaka 34 sasa ifikie kwenye miaka 45 ili kusudi hata hii mikopo wanapopewa wapewe watu wanaojifahamu wanaojielewa, ili kusudi kuleta tija katika jamii yetu lakini katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hili suala la bajeti kwa kweli mimi nimuombe tu Mheshimiwa Waziri na timu yake msione aibu kwenda kuomba bajeti na kurudi mara mbilimbili kuomba bajeti na mkirudi kwetu sisi Wabunge basi tutawapitishia kwa sababu Wizara hii ni muhimu sana na nimtambuka na haswa kwa jamii yetu kutokana na mambo mbalimbali. Kwa kweli bajeti hii ni kidogo sana, haiwezi kukidhi mahitaji au uwitaji wa bajeti hii au uhitaji wa eneo hili kutokana na kwamba shughuli zake ni nyingi sana na hasa ukizingatia kama hivi unavyoona hali ya sasa hivi ni mbaya mbaya sana. Lakini bado hao hao Maafisa Maendeleo ya Jamii hawana usafiri na saa nyingine pia wanaleta usumbufu sana kwetu sisi Wabunge wanatuomba wakati sisi wenyewe na sisi wenyewe ni tia maji maji, kwa hiyo wanakuja kutuomba pesa za usafiri na nini suala ambalo tunaamini kabisa Wizara ikitengewa bajeti ya kutosha basi na wo watapata usafiri na vitendea kazi vingine ili kusudi boresha mambo mbalimbali katika wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia walivyotangulia kusema Wabunge wenzangu kwenye hili suala la mikopo midogo midogo; hii mikopo nafikiri sasa imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu ukienda sehemu nyingi wengine wanashindwa kurudisha mikopo, lakini wengine wanacheleweshwa, lakini wengine pia hawaendelei, kila siku wanakuwa pale pale ni kwa nini basi? Ni kwa sababu hii mikopo wanapopewa ni midogo sana kwa mfano shilingi milioni tano unawapa watu 10 ukigawanya nafikiri ni kidogo sana. Mimi kwenye somo la hesabu nilikimbia umande nafikiri mkiangalia mkipiga hapo hesabu mtaona kwamba ni pesa kidogo sana, kwa hiyo ni pesa ambazo hazitoshelezi kwa ajili ya mtu au mjasiriamali kujiendeleza kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na ndiyo maana wengine sasa wanaishia kula nyumbani, lakini kwa wale wenzangu na mimi wanaishia kwenda kununua carolight, anaona kwamba sasa mbona hii hela ni kidogo sana mimi itabidi nikapendeze, labda nitairudisha lakini sasa inakuja kutokea anashindwa hata kuirudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niishauri Serikali hii pesa inatakiwa iongezwe, huu mkopo at least basi wawe wanapewa kwa awamu lakini wapewe fedha ya kutosha kwa mfano hao watu 10 wanaweza kupewa awamu ya kwanza hiyo milioni tano halafu tena wakaangaliwa awamu nyingine wakaongezewa tena milioni tano, tena wakaja wakaongezewa kidogo ili kusudi ile mikopo iwe na tija na hasa kwa Watanzania. Tunamshukuru sana mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake anaotuonyesha kwa Watanzania na hasa Watanzania wajasiliamali wadogo na wanawake kwa mikopo aliyoitoa ya milioni 10 kila mkoa ombi langu au ushauri wangu kwa Serikali; mikopo hii ili iwe na tija iende ikasimamiwe vizuri kwa sababu huko kwenye Wilaya zetu au mikoani kwetu huko huwa kuna ile hali ya wanasiasa kuingilia mikopo hii wanapoingilia mikopo hii wanaweza ukakuta kuna kikundi cha shangazi, mjomba, bibi, babu unakuta yuko Mheshimiwa Meya tayari kawandaa ndugu zake au kawaandaa kikundi fulani anajua hapa sasa hapa hiki kikundi huyu Agnes ani-support, huyu ndiyo mpiga debe wangu hawa wapiga debe na wengine hawapati lakini hiyo siyo nia ya Mama Samia Watanzania wote mnapaswa kujua Mheshimiwa Wetu Rais hajali itikadi ya mtu, itikadi ya chama, wala kuangalia huyu mtu katokea sehemu gani yeye ametoa pesa imsaidie kila Mtanzania. Kwa hiyo, wale watendaji wabovu mimi niombe tu Mheshimiwa Waziri nenda kashughulike nao, lakini sasa ufanyike ufuatiliaji wa kina, kwa sababu pesa hizi ukizifuatilia kwa undani zaidi utakuta ziko kwa hao hao viongozi ambao ni viongozi wetu wa pale manspaa na nipesa ambazo vikundi vingi vinalalamika sasa unajiuliza kwamba kwa nini vikundi vingi vinalalamika...

MHE. LUCY T. MAYENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Agness kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Lucy Mayenga.

T A A R I F A

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kumpa taarifa itakuwa ni vizuri sana Hansard iweze kukaa vizuri ni Mheshimiwa Agnes mchangiaji wetu akaweka rekodi vizuri Maafisa ya Maendeleo ya Jamii ni watu ambao tunawategemea sana kwenye halmashauri zetu, wanatufanyia kazi kubwa sana kwa hiyo ni vizuri tu labda nadhani aweke vizuri rekodi kwamba siyo kwamba wanaomba omba, labda pengine mtu akiwa na jambo anaweza akahitaji msaada wa hapa na pale; hilo moja lakini lingine Mheshimiwa Rais akutoa fedha hizo milioni 10 kwa ajili ya mikopo huko kwenye halmashauri zetu, ahsante sana ni vizuri aweke rekodi vizuri isiye ikaonekana kwamba kuna vitu ambavyo tunaviweka havijakaa sawa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo na hapo hapo nimesahisha kutokana na maneno yake. Lakini tu mimi niseme tu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, kengele ya pili imegonga.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana haya yote pia katika hii wizara maendeleo ya jamii michezo pia ni furaha kwa maana hiyo kwa furaha hii mnyama kule Mwanza tulimpiga chini na sasa tunasema furaha ipo basi katika maendeleo ya watu nashukuru sana, Yanga oye. (Makofi)