Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa dakika chache, nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka eneo la watu wanaofuga na wanaovua. Mheshimiwa Waziri, uncle, Halmashauri ya Bunda unaijua, wanafuga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ulega Halmashauri ya Bunda unajua wanavua, lakini Wizara hii hamjatuendea haki zaidi ya miaka mitatu mfufulizo tumekuwa tukiomba majosho, tumekuwa tukiomba mtukarabatie na kutujengea uzio kwenye minada, tumekuwa tukiomba machinjia kwa sababu lililopo ni la mwaka 1979 Mheshimiwa Ester Bulaya sijazaliwa. Lakini Mheshimiwa Ulega umejibu swali hapa maswali yangu ya kuomba vikundi vya uvuvi, Kikundi cha Wauza Samaki Bunda Mjini, Kikundi cha Ushirika cha Uvuvi cha Nyatwali vipatiwe mikopo; wameitikia wito wa Serikali wa kuvua kisasa, hivyo vifaa vya kisasa hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana sasa Mheshimiwa Waziri sisi tunauhitaji wa majosho Matano, Halmashauri ya Mji wa Bunda ina Kata 14, Kata saba ziko vijijini huko wanafuga. Tulikuwa tumeomba majosho Matano na ninajua kwenye fedha za majosho mnazo; Anko naomba hata mawili kwa mwaka huu wa fedha mahitaji yapo kwenye Kata ya Kunzugu, Mchalo, Kabasa, Waliku na Guta. Tunaomba walau kwa kuanzia mwaka huu wa fedha mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri unajua sisi Bunda tuna minada mitatu, lakini tunaomba walau kwenye minada miwili wa Bitalaguru Kata ya Kabasa na wa Kinyambwiga Kata ya Kunzugu. Halmashauri iliomba Milioni 257 kwa ajili ya hii minada na tukikarabatiwa tukaweka na uzio; mosi itasaidia utoroshaji wa mifugo lakini vilevile tutachangia hii Halmashauri mpya ya Bunda ili iweze kukusanya mapato na kufanya maendeleo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tulikuwa tunaomba machinjio na tayari tulishakuwa tumeomba milioni 150 kupitia mradi wa TACTIC bado hatujapata. Tunaomba machinjio, lile lililopo ni la mwaka 1979 wala Bulaya sijazaliwa, nimezaliwa, nimekuwa Mbunge, tunaomba machinjio mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ulega, umenijibu maswali zaidi ya mara tano kuahidi vikundi, leo hapa sema neno; vikundi vyangu vya wavuvi na vinanisikia sasa hivi vinahitaji fedha waweze kuvua kisasa na waweze kujiendeleza kimaisha. Amesema Mheshimiwa Tunza, hii sekta ya uvuvi mnaona kama ya watu maskini maskini hapana wawezesheni ili na wenyewe kama watanzania wengine. Ahsante. (Makofi)