Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nichangie kwenye eneo hili la Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Mifugo aliwahi kuja Jimboni kwangu kwa lengo moja la kuhakikisha kwamba anagawa vizimba au blocks kwenye eneo la ranch ya Wizara ya Mifugo ili kusudi watu wanaofuga Ng’ombe waweze kupeleka ng’ombe zao pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa hilo lakini pia kwa kazi ile iliendelea pia kwa sehemu imekamilika. Sasa bado kazi ya kuelimisha wale Wasukuma, na wewe ndiyo uje uongee kisukuma na waondoe ng’ombe katika vijiji vyote 61 vya Wilaya ya Uvinza. Sasa hivi wakulima wanalima na hawavuni kwa sababu ya ng’ombe zilivyotapakaa katika Jimbo na vijiji vyote. Sasa Ng’ombe tunazipenda zina maziwa, zina nyama lakini sasa utakula nyama na maziwa bila ugali? Haiwezekani! Sasa uje.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa tu taarifa mchangiaji anayeendelea kuchangia aondoe neno Wasukuma maana anagusa kabila la watu wengi ambao tumo hata humu ndani. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sasa hiyo siyo, ungesema kuhusu utaratibu kwa sababu umetumia Kanuni tofauti, lakini na wewe Mheshimiwa Bidyanguze jaribu kuji-refrain kutumia majina ya watu. (Makofi)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, sizungumzi hivyo kwa nia mbaya lakini ndiyo wafugaji na ndiyo matajiri wa ng’ombe, Waha hatufugi ng’ombe sisi ni wakulima. Kwa hiyo, akija yeye ana lugha ambayo ataweza kuongea nao ili waweze kuondoa ng’ombe katika vijiji na waweze kupelekwa katika eneo ambalo Waziri alikuja kuliandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niondoke kwenye eneo hilo la mifugo ambayo mifugo yetu katika eneo la Wilaya ya Uvinza inakaribia takribani mifugo Laki Mbili na mifugo haiharibu tu mazao ya wakulima inaharibu na reserve ya misitu ya Serikali ambayo imewekwa pale, ambayo lengo la Serikali kuacha misitu ile ni kuendelea kuwa na mvua na sifa ya Mkoa wa Kigoma ni kweli kwamba hatujawa na ukame hata siku moja, sasa kwa ujio wa hizi ng’ombe Laki Mbili maana yake kama Serikali haikufanya juhudi ya kuhamisha hizo ng’ombe maana yake na Kigoma tunakwenda kuwa na jangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihamie kwenye eneo la uvuvi. Naomba nikupongeze Mheshimiwa Waziri pia Naibu Waziri nikupongeze. Mheshimiwa Waziri, ulipokea ujumbe wa Wavuvi kutoka Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake wavuvi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini Pamoja na Kigoma Kusini. Ulitoa elimu nzuri na sasa hivi Waziri au Naibu Waziri anapokwenda katika Jimbo la Kigoma Kusini au Kigoma kwa ujumla haendi tena kuchoma nyavu hafanyi hiyo kazi tena, kwa sababu tayari elimu ilikwisha patikana. Juzi alikuwepo Naibu Waziri, kwakweli hakuna nyavu alizooneshwa ili achome, kwa hiyo Waziri elimu ile uliyotoa wakati wale viongozi wa uvuvi wamekuja ile elimu iko vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo bado tunahitaji Wizara iweze kuwasaidia wavuvi wetu vifaa vya kisasa vya uvuvi. Sasa hivi wavuvi wa Ziwa Tanganyika katika Majimbo Matatu wanakwenda kuvua na wanarudi bila samaki, wanarudi bila dagaa na vyombo wanavyotumia ni vilevile walivyokuwa wakitumia zamani wakati samaki zikipatikana na dagaa zikipatikana. Kwa hiyo, nadhani imefika wakati sasa Wizara ilete wataalam, iweze kubuni ni vyombo gani vya kisasa viweze kuletwa katika Mkoa wa Kigoma kwa maana ya wavuvi wetu waweze kufaidi matunda ya nchi ili waweze kuvua. Siamini kwamba samaki katika Ziwa Tanganyika hawamo! Kwa mujibu wa tafiti zilizopita samaki bado ni wengi ingawaje nimeongea na Afisa Uvuvi ameniambia kwamba TAFIRI wamefanya utafiti mwingine, tunaomba Wizara utafiti huo uletwe tujue samaki wapo kiasi gani na wapo katika maeneo gani? Tumechoka wavuvi wetu kwenda kuvua kwa kubahatisha gharama ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze shirika moja linaloitwa ‘TUUNGANE’ hili shirika linawasaidia wananchi wa jimbo la Kigoma Kusini sijui kama majimbo mengine kama wapo lakini hawa ndiyo ambao kidogo wanawasaidia wavuvi katika Ziwa Tanganyika. Nadhani Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja mara mbili mfululizo pale Buhingu, Nakatumbi, wamejengewa vyombo vya uvuvi viwili vya thamani ya Milioni 38, jambo la kuunga mkono na jambo la kupongeza sana hawa watu wanaojiita tuungane ni shirika zuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Buhingu pia wanajenga mwalo wenye thamani ya Milioni 300 unaweza ukaona kama ni shirika …

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Bidya kengele ya pili.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naomba kwa hayo machache niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)