Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupewa fursa ya kuchangia hoja ambayo iko mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kazi kubwa anayoifanya ya kulijenga Taifa hili. Kwa wizara hii niwashukuru kwa kuleta habari njema katika Mkoa wa Kagera kwa vizimba 9 ambavyo wametupatia, na vinne vinakwenda wilaya ya Muleba wanakwenda kututengenezea ajira hii ni habari njema kwa wakazi wa Muleba na wakazi wa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru tena kwa kutupatia boti moja na injini moja Wilaya ya Muleba kama ambavyo nimekuwa nikichangia ni wilaya yenye visiwa vingi yenye maji mengi lakini pia yenye matatizo mengi vizimba vinne tunashukuru tukiongezewa vingine viwili tutashukuru zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende kuchangia suala la migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Muleba. Naomba niseme ni Mbunge wa Wilaya ya Muleba, Wilaya ya Muleba tuna Kata 43 lakini ni wilaya yenye majimbo mawili ya uchaguzi niko mimi na yupo kaka yangu Charles Mwijage. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi amechangia lakini kilio chetu migogoro au mgogoro mkubwa wa ardhi ambayo NARCO ameichukuwa ameivamia, bila kufuata taratibu za kisheria na ninashangaa sijui kama NARCO wana mwanasheria pale. Hili utengeneze Ranch hii ardhi ya halmashauri ichukuliwe kwa ajili ya matumizi ya umma upo utaratibu. Huwezi kuamka asubuhi unakwenda unavamia ardhi ya halmashauri yeyote kwa kisingio chochote kile bila kufuata utaratibu unasema naanzisha Ranch hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa Mwisa na Utoro au hizi Ranch za Rutoro na Mwisa imeanzishwa kinyume cha sheria cha sheria za nchi hii. Rutoro kilikuwa Kijiji tangu mwaka 1976 mwaka 2005 NARCO wakaenda wakapima Ranch pale mwaka 2010 Serikali hii Tukufu ikapandisha hadhi Kijiji cha Rutoro ikawa kata vile vitongoji vilivyokuwa chini ya kile Kijiji ikapandishwa hadhi vikawa vijiji, sasa nashindwa kuelewa NARCO wamepima vitalu mwaka 2005 sijui kwa mamlaka ipi lakini Serikali mwaka 2010 inapandisha vile ambavyo vimepimwa kama vitalu inaipa hadhi ya kata na vitongoji inaipa hadhi ya kijiji sielewi hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria tunazitunga sisi wenyewe na lazima mashirika na taasisi za Serikali zifuate sheria. Katika mgogoro huu wa Mwisa unahusisha kata saba Mheshimiwa kaka yangu Mwijage asubuhi amesema wananchi ambao wako kwenye hizo Kata za Kebitemba, Karambi Kasharunga Mbunda Burungula Genge na Rutoro ambazo zina vijiji 12 vitongoji 19 wako kwenye kilio na kazi ya mama ni kupangusa watu wanaolia machozi namuomba mama awapanguse hao watu wa vitongoji 19 awapanguse machozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamelia sana naomba kilio chao kifike mwisho. Lakini NARCO wamekwendaje kwenye eneo la Mwisa na lenyewe ni kizungumkuti hakuna sheria yoyote ile ambayo wameifuata kama nilivyotangulia kusema ili ardhi yoyote itwaliwe lazima Sheria ya Ardhi ya Vijiji ifuate sheria namba tano ukisoma kipengele cha section 4 subsection one ya sheria ya ardhi ya vijiji ili waanzishe Ranch Rais lazima atwae lile eneo na anapolitwaa kuna hati ambayo inatolewa na nimesoma bajeti ya Mheshimiwa Waziri wakati anasoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma kiambatisho kwenye hotuba yake kiambatisho namba 15 imeongelea migogoro ya NARCO kiambatisho namba 12 ameongelea maeneo ambayo yametwawaliwa na NARCO yametolewa notice ya Serikali lakini kiambatisho 11 ameongelea maeneo ambayo yametwawaliwa bila notice ya Serikali sasa nashangaa unatwaaje maeneo unaanzisha ufugaji bila kufuata sheria hakuna notice hakuna nini tunashindwa kuelewa nchi tunaipeleka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi ardhi yao imechukuliwa kinyume cha sheria hapa tunapoongea kwenye lile eneo ambalo wametwaa kinyume cha sheria hakuna notice na nitamuomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hapa atuambie bila kupepesa macho eneo la Rutoro notice ambayo inakupa mamlaka ya kulichukuwa ni notice ya mwaka gani ya tarehe ngapi, ya siku gani utuambie na wananchi wasikie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utuambie eneo la Mwisa umelipatajepataje kama kuna notice ya Serikali utuambie notice namba ngapi kama hakuna notice uwaambie wananchi wa Mwisa ambao leo wananyanyaswa wanaamishwa na hakuna mtu ambaye anafuata hata sheria ya kuhamisha makaburi mnaleta mifugo mnalishia kwenye makaburi ya wazazi wetu wazee wetu ambao wamepumzika pale hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama hakuna notice hiyo tuwatangazie wananchi ambao wanahamishwa waendelee kuishi kwenye maeneo yao mpaka utaratibu utakapofuatwa. Mheshimiwa Rais anayo madaraka akiamua atatwaa ile eneo afuate utaratibu.

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Dkt., Kengele ya pili hiyo, ahsante.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO Mheshimiwa Naibu Spika, sitaunga hoja mkono mpaka nipate maelezo ya kina, tupate zile notice.