Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi hii awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwanza kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati kabisa kuhakikisha sekta zetu hizi za uzalishaji kilimo, Mifugo na uvuvi vinakwenda sasa kumuinua Mtanzania na kuinua uchumi wa Taifa hili, na hayo hayatekelezi kwa maneno bali anatekeleza kwa vitendo kwa maana kubwa kwamba sekta hizi ameziongezea bajeti katika matumizi yake kwa kipindi cha mwaka huu bajeti yetu ya Wizara hii imefikia bilioni mia moja tunapongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulea mimba ni kazi lakini kulea mwana ni kazi zaidi Serikali, Rais wetu, Viongozi wetu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wanahangaika huku na kule kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na kimaendeleo. Tunaomba fedha hizi zitumike kwa dhamira zilizokusudiwa zisiende kutumika kwa matumizi mengine kwa maana ya kwamba Serikali kupitia Wizara hii iwe wakali na iwe wasimamizi wazuri kuhakikisha fedha hizi zinafanya kazi zilizokusudiwa kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia sekta ya mifugo, sekta ya mifugo ina changamoto nyingi lakini kutokana na mpango wa Bajeti hii tuliyopewa na Mheshimiwa Waziri baadhi ya changamoto nyingi zinakwenda kutatuliwa kutokana na fedha zitakazoingizwa kwenye bajeti tunaomba fedha hizi Mheshimiwa Waziri na wanaohusika na utoaji wa fedha, fedha hizi ziende kwa wakati na zitoke zote ili zikatekeleze hayo majukumu yaliyopangwa kumuinua mfugaji kumuinua mvuvi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uwekezaji katika sekta hii ya mifugo suala la ngozi, ngozi zetu bado zina changamoto katika soko la dunia masoko yapo lakini ngozi hazikidhi viwango. Wizara imetoa mpango wamesomeshwa Maafisa Ugani kwenda kuangalia madaraja ya ngozi, lakini hawa maafisa ugani wanatakiwa kufanya zaidi ni kumuelimisha mfugaji namna ya kuhakikisha ile ngozi haiharibiki na inapata madaraja ya juu mfano kuwapiga mikwaju hovyo wale wanyama ng’ombe inaharibu sana ngozi na inakosa thamani kuwachoma choma hovyo sasa hapa elimu itolewe kwa wafugaji kwamba sio nyama tu lakini hata ngozi ni bidhaa kubwa ambayo itamsaidia kuinua kipato chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la ndani kwa maziwa lipo natoa mfano ASASI anapata asilimia 60 tu ya mahitaji yake kutokana na uwezo wa kiwanda ana ukosefu wa asilimia 40 ili kukidhi mahitaji ya kiwanda nashauri kwa vile miundombinu ya uwekezaji pale ipo eneo karibu na ASASI basi tuongeze uhamasishaji wa ufugaji bora katika maeneo yale vijana tuwahamasishe wafuge kisasa tupate mazao bora ya maziwa kwa maana tayari soko kwenye eneo lile lipo la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni soko la ndani wala sio soko la nje na hivi sasa mfano Kiwanda cha ASAS kina mpango wa kutengeneza maziwa ya muda mrefu kwa maana ya maziwa ya unga kwa hivyo watahitaji sana malighafi ya maziwa. Hilo soko lipo kwa maeneo ya Iringa. Nikiendelea kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Serikali imezuia kiwanda cha kuchinja Punda na wameomba kwamba uwekezaji ule sasa ubadilike matumizi wachinje mbuzi, kondoo na ng’ombe hapa inaonekana kwamba soko la punda ni kubwa na linaweza likaongeza uchumi wa nchi na linaweza likatoa ajira kubwa kwa vijana na wanawake na wafugaji kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ihamasishe ufugaji wa punda ili kukidhi masoko ya hawa wawekezaji waliokuja kuwekeza punda ili tuweze kupata fedha za kigeni lakini tuongeze ajira kwa vijana wetu hapa inaonekana punda wanatakiwa sana huko duniani sasa kama sisi punda wetu wamepungua tumezuia sasa hawa waliokuwepo tuongeze uzalishaji wawe wengi zaidi ili tupate hilo soko la punda duniani na vijana wetu wapate ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ufugaji mnahamasisha tuwekeze zaidi kwenye malambo kwa maana ya mabadiliko ya tabia nchi, yanaharibu sana upatikanaji wa uhakika wa maji. Nashauri wafugaji na wavuvi waitumie benki ya kilimo ile benki siyo ya kilimo peke yake, tutoe elimu kwa wafugaji wetu na wavuvi kwamba benki ya kilimo inawahusu wao pia wafugaji na wavuvi. Kwenye sekta ya uvuvi kwanza nipende kuchukua fursa hii kuwapongeza wavuvi wote Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya. Uvuvi ni kazi ngumu unatoka usiku unaacha nyumba na watoto, unakwenda baharini hujui kama utafika au hufiki, hujui kama utakwenda au utarudi, hujui kama utavuna au hauvuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi tu ya kubahatisha vyombo vyenyewe ni duni hali ya bahari tunaijua haina muda haina wakati wakati wote inapata wazimu huko baharini. Nashauri Serikali iongeze uwekezaji kuinua wavuvi wadogo wadogo ili kunusuru Maisha yao lakini kupata tija ya kipato chao kwa muda wote huu wanafanya kazi tunapata lishe tunapata vitoweo lakini bado hali ya mvuvi ipo chini na duni na hana kipato cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea ufugaji wa viumbe kwenye maji Wizara imeweka mpango mzuri napongeza Serikali kwa mpango huu tuimarishe na tushajirishe vijana wetu kuingia kwenye uwekezaji wa uvuvi kwenye maji, hivi viumbe maji sio samaki tu kuna kaa, kaa wana faida kubwa na wana fedha nyingi za kigeni lakini kuna majongoo, majongoo yanatakiwa sana duniani na yana fedha nyingi za kigeni kupitia majongoo, lakini katika uvuvi huu wa viumbe kwenye maji tunapata madini ya Lulu pale, tukiwafundisha wavuvi wetu namna ya kutengeneza Lulu tutapata fedha za kigeni kupitia madini ya Lulu, Lulu ni madini na yanapatikana kupitia viumbe kwenye maji na yanafugwa, Lulu haichimbwi, lulu inapatikana baharini na lulu inatengenezwa kwenye vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uvuvi wa bahari kuu Serikali ihakikishe kwamba tunawekeza zaidi kwenye bahari kuu, mipango na mikakati mingi tumeiona tunaomba mpango hii ifanikiwe kwa sababu tunahimiza uvuvi wa bahari kuu tunataka kulitumia shirika la TAFICO, Shirika la TAFICO linahitaji uwekezaji mkubwa linahitaji fedha nyingi kwa sababu ukiliangalia hayo maeneo yake ya uwekezaji tayari mmomonyoko bahari inakwenda kula yale majengo, kwa hivyo kwenye uwekezaji ule wa majengo kunahitaji fedha nyingi kuzuia bahari yale majengo yasiharibiwe na maji ya bahari yakianza kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)