Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba yetu hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza nipende kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na timu yao katika wizara kwa yale ambayo wameweza kufanikiwa kuyafanya ambayo bado yapo kwenye mchakato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mwana CCM na huwa nikipenda kushauri ukweli napenda kutumia kati ya moja ya ahadi zetu za uanachama, nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa Sangara katika Ziwa Victoria ni mbaya sana; sasa sijajua kama kwenye vipaumbele vya wizara yetu hii wameliona hili na kulitaka kulitafutia ufafanuzi. Kwa nini nasema hali mbaya? Sangara ni bidhaa kubwa sana katika Soko la Samaki la Export katika dunia, Europe ndiyo soko kubwa sana ambalo zaidi ya asilimia 70 ya mazao ya Samaki yanayotoka Afrika yanakwenda huko Europe, zaidi ya asilimia 70. Mwaka 2014/2015 Tanzania tulikuwa tunatoa zaidi ya tani 45,000 za minofu ya Sangara na mazao yake; lakini mwaka 2021 tumetoa tani 14,000 tu; lakini viwanda vyetu vilivyokuwepo mwaka huo 2014/2015 tulikuwa tunaajiri zaidi ya vijana 12,000 kwenye sekta hii. Nasikitika kusema ajira imepungua zaidi ya asilimia 50 na leo hii tuna takriban vijana 4,000 tu ambao wameajiriwa kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Wabunge wa Mikoa ya Mwanza na Jirani ni mashahidi, ukienda kuhoja wamachinga waliokuwepo mtaani, miaka kumi kumi na ngapi nyuma wengi walikuwa waajiriwa kwenye viwanda hivi; Lakini hapo zamani viwanda vilikuwa vinafanya kwa siku shift tatu na vilikuwa operational wiki nzima siku saba ndani ya wiki; lakini cha kusitika hali sasa hivi viwanda hivi vinafanyakazi kwa shift moja na nusu kwa siku na siku nne tu kwenye wiki. Kwa hiyo, nimetoa picha hii ili tujue leo royalty inakuwa inapatikana kwenye biashara ya sangara ndiyo ilikuwa inasaidia kuleta maendeleo kwenye nchi yetu; ilikuwa inasaidia kujenga hospitali, Vituo vya Afya na maeneo mengine ya kimaendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa nimeangalia sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri bado sijaona. Ninaamini jambo ambalo linasababisha hali hii ni uvuvi haramu. Lakini nimesikitika kuona kwamba katika vipaumbele vya wizara sijaona palipoandikwa kwamba mna mkakati wa aina gani madhubuti wa kupambana na uvuvi haramu. Lakini naweza kutoa tu maoni na kama mnayafanyia kazi mmesahau tu kuandika mtanitolea majibu huko wakati mnajibu hoja zangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niulize Mheshimiwa Waziri nimefuatilia unazo takwimu kweli kuhusu viwanda ambavyo uko navyo, kwa sababu kati ya wageni mliowaalika wamiliki wa viwanda kuja kuhudhuria bajeti hii, mmewaalika Kampuni inaitwa Prime Catch lakini hii Prime Catch imefungwa miaka 10 iliyopita hakipo hiki kiwanda; kuna kiwanda kinaitwa Vick Fish, hakipo kilishafungwa hiki kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Uganda ambayo inasehemu ndogo sana ya Ziwa Victoria inatuongoza kwa kuwa na idadi ya viwanda vingi kuliko sisi; Leo hii kwenye nchi 10 Afrika zinazopeleka minofu ya Samaki kwenye soko la dunia Tanzania hatupo; Uganda ambao ni landlocked country inayo Ziwa Victoria peke yake haina ukanda wa Bahari kama wa kwetu ipo ni nchi ya 10 Afrika. Sasa naongea hivi kwa masikitiko makubwa sana, yapo maeneo Mungu ametubariki mno, kikubwa ni utashi wa kutambua tatizo lipo wapi tukapata uthubutu wa kushughulikia hili tatizo ili kunusuru hali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niulize huko nyuma kuna operation ilianzishwa kwa ajili ya uvuvi haramu, al-maarufu operation Sangara, nia ilikuwa njema lakini niulize kama wizara je, mnayo tathmini ya operation kwa sababu kwa wananchi leo ukiwauliza kuhusu operation hii ni majeraha matupu. Operation iliyokwenda kutia umaskini watu, iliyosababisha vifo kwa watu kupata mapresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui kwa upande wenu Serikali tunaomba mje na tathmini je operation hii ilikuwa na manufaa gani kwa nyie mnavyoona huko; na je mlichopanga kufanya kikaende ndivyo sivyo mnarekebishaje ili basi tuweze kuwa na mipango Madhubuti, kwa sababu nimesoma gazeti la Guardian la tarehe 20 Mei, 2022; Wizara mlitoa kauli kwamba mmejipanga kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kupambana na uvuvi haramu. Sasa nataka kuliko kwenda kulitia tena Taifa kwenye hasara tujue ile operation ilifeli wapi, hasara ilikuwa wapi, ili kabla hamjachukua fedha hizi za umma kuziingiza huko tayari muwe na tathmini na tujue mmejipanga vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri unao maafisa wetu wa uvuvi katika kila nyanja kwa maana ya vijijini mpaka mikoani. Tumewaweka hawa kule kwa ajili ya kusimamia hizi rasilimali zetu kama vitendo hivi vinaendelea inamaana wao wanaviruhusu; wao ndiyo wapo kwenye mialo, wao ndiyo wapo kwenye catchment area; Je, mmewawajibisha vipi hawa wanaosimamia hii rasilimali iwe ya kinidhamu ama kiutendaji, je wanawaletea ripoti, hizo ripoti mnazifanyia kazi, je kama ni uzembe wao mmewachukulia hatua gani tuanze nao hao ili watatupa majibu mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongereni mmechukua hatua ya kukaa na wadau kwa maana ya wavuvi wadogo, wakubwa lakini na wamiliki wa viwanda. Tujiulize kila mmoja yuko bitter kwenye suala la uvuvi haramu, wote wahusika wako bitter. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hebu tukae chini tena kama kila mtua anachukia Serikali, wananchi wanachukia, wadau wanachukia shida ni nini Uvuvi huu haramu unaendelea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaona katika Ziwa Victoria tunali-share na majirani zetu kwa maana ya Uganda na Kenya na tunaona Uganda ndiyo inaongoza na Uganda ndiyo ina control bei, ina maana leo Uganda ghafla kwa vile wao ndiyo wameshika soko wanashusha bei inakuja kuathiri. Je, mmejipangaje kama Serikali katika kulinda hawa wavuvi wetu wasipate hii athari; cha kwanza kwa kukaa chini na hizi Jirani, kuona kama tunaweza kuwa na bei elekezi ili haya mabadiliko ya kiholela yasiathiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mjifunze kutoka Wizara ya Kilimo, leo hii wamekuja na bima kwa ajili ya wakulima wao kwa nini na sisi tusione namna ya kuwa na bima ya hawa wavuvi wetu ili hali inapotokea waweze kukaa vizuri lakini pia muone namna gani tunaweza kuwa na soko la uhakika; kuliko mtu anakwenda huko usiku kucha yupo gizani anavua halafu akirudi bei imeshuka na inakuwa hasara kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema tunalo Ziwa Tanganyika, dagaa zinazopatikana Ziwa Tanganyika ni dagaa ambazo ni nzuri haijawahi kutokea. Lakini nasikitika kusema mpaka leo biashara ya dagaa hizi ni kiholela; leo Ziwa Tanganyika, Rukwa, Katavi, Kigoma hakuna kiwanda kikubwa cha Samaki na ukiacha dagaa kule kuna Samaki nzuri, kuna migebuka, tunazo kuhe wanaita kuku wa ziwani, Serikali imejipangaje katika kuvutia uwekezaji wa kiwanda kikubwa kwenye Ziwa Tanganyika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hamna taarifa ninayo, wako wawekezaji wanaotaka kuweka kiwanda kule lakini tangu waanze mchakato imekuwa mchakato mpaka mchakato. Fuatilieni, mjue kama kuna engagement Serikali muwasaidie basi wananchi wetu waweze kuongezewa thamani ya mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna mpango wa kuanzisha viwanda kwenye ukanda huu wa Bahari, kwamba kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara, Tanga huu ukanda wote. Miaka sita iliyopita nataka niulize je kipindi chote tangu tuanze kujinasibu na Tanzania ya Viwanda hasa kwa maeneo ambayo tunatumia rasilimali zetu; kwenye ukanda huu wa Bahari kuna kiwanda kipya kimeanzishwa mpaka leo; na kama hakijaanzishwa ni kwa nini; kwa sababu taarifa nilizokuwa nazo ni viwanda kufungwa tu sasa sijui inawezekana hatuna huo ufahamu basi wakati mnajibu hoja mje mtuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tuanze adhma hiyo ya kuanzisha viwanda kwenye ukanda ule, viwanda vingapi vimeanzishwa na vina hatua gani, kama havijaanzishwa sababu nini, na tunajipangaje? Kwa sababu haiwezekani leo hii Morocco ambaye ana sehemu ndogo tu ya Bahari atuzidi sisi kwa ku-export mazao ya Seafood kwenda nje ya nchi, kwa kweli tunamkosea Mungu, Mungu ambaye ametubariki sisi eneo kubwa sana la Bahari. (Makofi)

MWENYEKITI: Kengele imelia Mheshimiwa Mariam.

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi napenda tu leo nimechangia kwa utulivu na hisia kwa sababu kama wizara hatutoweka mipango madhubuti katika kunusuru hali ya bahari na maziwa yetu yakaleta tija kwa Taifa, tutakuwa tunamkosea sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye ameonekana ni mtu mwepesi, msikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo tulikuwa tunapiga kelele kuongezewa bajeti miaka yote lakini bajeti imeongezeka; kwa kweli niwaambie kweli wizara hii mmeniangusha, hotuba hii haijanigusa, naomba kama mna majibu ambayo kidogo yataamsha ari yangu na kuwa na matumaini mapya mje nayo wakati mnahitimisha mjadala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja nashukuru sana.