Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa hili. Sambamba na hilo nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuwapa dhamana wadogo zangu Mheshimiwa Bashe pamoja na Ndugu yangu ili kuweza kuiendeleza Wizara hii, kiukweli wamekusudia kuweza kutengeneza legacy ya aina yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiongozi mzuri ni yule ambaye anao uwezo wa kuchukua maamuzi na kuyasimamia maamuzi hayo. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Bashe, pale kwetu katika Mkoa wa Pwani tulikuwa na mfanyabiashara ya uchuuzi wa kukamua mafuta lakini kwa bahati mbaya hakufuata taratibu husika ikiwemo kupata leseni za kibiashara, vyombo vya usalama vilimkamata lakini nikushukuru sana Mheshimiwa Bashe ulichukua maamuzi magumu na uliweza kusimama katika maamuzi yale, ulisema kwamba asaidiwe mtu yule ili aweze kufanyiwa registration na process zingine zote hivi ninavyozungumza umefanya multiply effect ya hali ya juu, mtu yule sasa hivi anaichangia Serikali kwa kulipa kodi, safi sana endelea Ndugu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najivunia kuwa na Rais Samia kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia kuwa kama Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, pia najivunia vilevile Chama cha Mapinduzi kuwa ndiyo Chama kilichotengeneza dola. Kuna sifa nyingi sana lakini nitagusia sifa moja Serikali hii ni Serikali sikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisimama hapa mwaka jana, nilileta kilio cha watu wa Jimbo la Kibiti wakiwa wanalalamika katika mambo makubwa mawili, jambo la kwanza ilikuwa ni suala zima la bei ya korosho na ufuta lakini jambo la pili ilikuwa ni suala zima la tarehe za kufanyika minada. Wale Ndugu zangu Wamakonde kule Mtwara na pale katikati Lindi walikuwa wanafanya minada tofauti nasi huku Baba zao watu wa Rufiki, hii ilikuwa inapelekea wakulima wetu kuuza mazao kwa bei ya chini, nilivyoleta kilio hicho nakushukuru sana Mheshimiwa Bashe na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana bei ya juu ya ufuta iliuzwa shilingi 2,556 katika Mkoa wa Pwani, kama hiyo haitoshi bei ya korosho iliuzwa shilingi 2,155 tunakushukuru sana na tunamshukuru Mheshimiwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Pia ninamshukuru sana Mheshimiwa Mkuu wangu wa Mkoa Alhaji Abubakar Kunenge, Baba yule anafanyakazi kwelikweli, alihakikisha anafanya transformation katika masuala mazima ya kilimo ndani ya Mkoa wetu wa Pwani. Namshukuru sana Mkuu wangu wa Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo makubwa mawili tu ya kushauri kwa Serikali, jambo la kwanza hili Bonde la Mto Rufiji kule ambako kuna ule mradi wanasema Rufiji Hydroelectric Power kuna upstream na downstream, sisi tupo kule downstream Wandengereko watu wa Rufiji, watu wa Kibiti pamoja na watu wa Mkuranga, ninaishauri Serikali tuweze kuangalia uwezekano wa kufanya kilimo cha umwagiliaji, nililisema hili mwaka jana lakini ninakuamini Mheshimiwa Bashe utalichukua na utakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka niishauri Serikali ni kwamba katika taratibu zetu za kufanya mambo ya mauzo ya korosho na ufuta kuna kitu kinaitwa Fomu Na. Saba.

Mheshimiwa Bashe niliwahi kukufuata katika jambo hili, tunapozungumzia suala zima la Fomu Namba Saba ni pale ambapo wale venders wanaonunua ufuta ama korosho wakiwa wanalipia kama tani 500, wanapokwenda katika ghala wanakuta tani 200, kwa tafsiri hiyohiyo makampuni ya insurance yanakuwa yanahusika kuweza kuwalipa. Mwaka jana 2021/2022 fedha ambazo mpaka hivi sasa zipo kule katika Bodi ya Maghala tunazungumzia bilioni 1.4. katika fedha hizi shilingi milioni 600 tu ndiyo zimelipwa. Kuna baadhi ya makampuni ya insurance hayalipi malipo hayo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na Kanuni zetu za Kibunge naomba niyahifadhi makampuni hayo lakini Mheshimiwa Bashe nitakufuata nikwambie makampuni gani yanayotuangushwa. Hawa venders ndiyo wadau wetu wakubwa wa maendeleo, tunategemea kwa kiasi kikubwa sana tunapokuwa tuna shughuli mbalimbali za kimaendeleo wao ndiyo wanakuja kutuchangia, pale ambapo wananunua mazao halafu mazao yale hawayapati na pale ambapo panakuwa panatokea upungufu halafu hawalipi kwa wakati hii inawakatisha tamaa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)