Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nami nichangie Wizara hii ya Kilimo. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali na pia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuikomboa nchi kutokana na utegemezi na kwa bajeti hii ya Wizara ya Kilimo ambayo kwa kweli kwa mara ya kwanza mimi nikiwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, nimeona Serikali imetenda haki kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa dhamira yake ambapo alisaidia sana wananchi wa Mkoa wa Singida, Simiyu na Dodoma kwa mbegu za alizeti ambazo zilikuwa zina daraja kidogo nafuu ambazo kwa sasa zinaenda kuongeza tija na uzalishaji wa mafuta katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishauri Serikali yangu hii kupitia Mawaziri hawa vijana, waongeze mbegu zilizo bora. Walitupa mbegu za kawaida ambazo zitaongeza tija ya mafuta. Tuna upungufu mkubwa wa mafuta katika nchi hii. Tunatumia mafuta ambayo yana cholesterol nyingi, inatakiwa tutumie mafuta haya mazuri ya mbegu za alizeti ambayo yatasaidia wananchi wetu kuepuka maradhi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu walizotupatia ni nzuri kwa kiasi, lakini mbegu zinazofaa sana kwa kilimo ni mbegu za hybrid ambazo ndiyo zina tija na uzalishaji mzuri sana wa zao hili la alizeti. Sisi Mkoa wa Singida ni Mkoa wa kielelezo, lakini Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Simiyu ambao mmewapa ruzuku na kuifanya kuwa mikoa ya kielelezo, mmeona jinsi ambavyo tumezalisha vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ambayo imeongezeka kwa kiasi kikubwa kwa asilimia 155. Natamani kuona Serikali inaweka ruzuku katika mbolea lakini iongeze ruzuku katika pembejeo yakiwemo matrekta. Matrekta ndiyo yatakayokomboa kilimo cha nchi hii. Mkulima mmoja akinunua trekta katika Kijiji, anawalimia wanavijiji zaidi ya 20 mpaka 30 mpaka 50 kwa kipindi kimoja. Kwa bei za trekta za sasa wananchi wetu wanashindwa kununua matrekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali iweke ruzuku ya kutosha, pale ndiyo unamsaidia mkulima. Kumsaidia mkulima kwa kilimo cha mkono bado hatujamkomboa na ndiyo maana mnatamani kuleta wakulima wakubwa kwa sababu wakulima wetu wanatumia kilimo duni. Sasa kama tuna dhamira ya kuwasaidia wananchi wa Tanzania katika kilimo na hasa vijana ambao wamekosa ajira, hebu tuwasaidie katika kuwawekea ruzuku ya kutosha katika pembejeo hasa matrekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji pia ni suluhisho kubwa sana. Tukiendelea kutegemea kilimo cha mvua, bado uduni wa wananchi wetu na uchumi wa wananchi wetu utaendelea kudumaa. Tukiweka kilimo cha umwagiliaji hasa mikoa ile ambayo ni mikame; mje na mkakati wa kujenga mabwawa katika mikoa kame hii ya Singida, Simiyu, Dodoma na baadhi ya Mikoa ya Tanga kama Handeni huko ambako ni kukavukavu na Kilindi. Tukijenga mabwawa wananchi watalima mazao ya chakula na mazao ya biashara, tutatoka katika sura hii ambayo tunayo sasa ya kutegemea kilimo cha mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo lipo mbele yetu, Mheshimiwa Mbunge aliyetangulia kusema hapa amezungumza kwamba njaa ipo. Nchi itakumbwa na njaa. Naomba sana Wizara hii kupitia NFRA waanze mapema sana kutoa chakula cha bei nafuu. Hatuhitaji msaada, wananchi wetu wamelima alizeti, wamelima mazao mengine, wakiuza basi kipatikane chakula ambacho ni cha bei nafuu ili tuweze kutoka. Katika kipindi cha kilimo kijacho wananchi wasianze kuhangaika, waweze kulima vya kutosha na waweze kuingia katika kilimo wakiwa na chakula ambacho kinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameitikia wito lakini hali ya mvua haikuwa nzuri sana, mvua ilikatika mapema na mazao mengine hayakuwezwa kupandwa, sasa hivi watu wanahangaika na dengu ambazo pia nazo pengine zikawa na mashaka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii uliyonipa nami niunge mkono hoja hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)