Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa nafasi, hii lakini naomba niseme mambo machache sana kwa sababu ya muda. Pamoja na mambo mengine, uhitaji wa sekta za uzalishaji ikiwemo sekta hii ya kilimo kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, ni muhimu sana. Kwanza ni kwa sababu asilimia 65 ya Watanzania wameajiriwa na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini kwamba tukipata ukuaji mzuri kutoka kwenye hii sekta ya uzalishaji tutaajiri watu wengi; pili, uchumi wetu utakua; tatu, uwezo wa wananchi wetu kustahimili madhara ya mtikisiko wa uchumi wa kidunia ambao unakuja na inflation ambazo wananchi wanashindwa kuzistahimili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa. Mwaka 2021 wakati naongea nilisema Malabo Declaration ilituhitaji tuchangie sekta hii kwa asilimia 10. Mwaka huu tumejitahidi; Mheshimiwa Rais amejitahidi, ni msikivu, ameongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 294 kwenda bilioni 751. Niseme wazi kwamba, hii ni hatua moja nzuri sana, lakini bado hatua hii tuliyokwenda nayo haitupeleki kwenye asilimia 10 tuliyoisema, bado tuko mbali kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bilioni 751 niseme wazi kwamba hili ni hatua moja nzuri sana lakini bado hatua hii tuliyokwenda nayo haitupeleki kwenye asilimia 10 tuliyoisema bado tupo mbali kidogo. Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana timu yako. Hoja yetu nataka tuhakikishe kwamba hii sekta ya kilimo inapatiwa fedha ya kutosha ili ukuaji wa uchumi wetu badala yakuwa single digit uwe double digit. Sasa hivi tuna single digit, na unaona inaendelea inacheza inashuka ikicheza inapanda. Tusipowawezesha hawa wananchi wetu kutokana na sekta hizi za uzalishaji hatuwezi kutoka mahali tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme wazi, pamoja na pongezi hizi tumeona wazi kwamba kuna ongezeko kwenye utafiti, mahali ambapo tumewapigia kelele sana mwaka jana, kutoka bilioni 7.35 tumeenda bilioni 11.63, umwagiliaji kutoka bilioni 11.5 kwenda bilioni 17.7, lakini mbegu kutoka bilioni 3.42 kwenda bilioni 10.38, haya ndiyo yalikuwa matatizo yetu. Sasa tukiongeza pesa ya kutosha maana yake ongezeko katika maeneo haya niliyoyataja kila atayelima atalima kwenye udongo anaoujua una characteristics gani? Kila atakayelima atalima eneo ambao limewezeshwa skimu za umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi, kwenye umwagiliaji hapo bado kuna shida. Tumeona wazi kwamba ukilima mpunga kwenye skimu za umwagiliaji kutoka tani mbili unapata tani nne au tani tano na unaweza kulima mara mbili kwa mwaka. Sasa, je, skimu tunazo ngapi? Tumeona wazi kabisa kwamba hadi sasa katika hekta milioni 29 sisi lengo letu ilikuwa hekta milioni 1.2 lakini bado tumefikia 700 na kitu tu. Kwa hiyo, bado tupo mbali kidogo kwenye sekta hii ya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kutoka kwangu jimboni kwangu. Sisi kwetu kwa upande wa huduma za ugani tuna maafisa ugani 27 na tuna kata 37. Maana yake ni kwamba, kuna kata 10 ambazo hazina ushauri wowote wa kitaalamu. Nimuombe Mheshimiwa Waziri atupatie maafisa ugani watakaoweza kutoa huduma za kigani ambazo zitafanya wananchi wetu waweze kupata mapato yaliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba mwaka jana kwamba tupate skimu za umwagiliaji, na tukaomba kwaajili ya maeneo ya Saraburwa, Magenge, Nyamaruru pamoja na Nyakagomba, lakini mpaka sasa jimbo langu ninalotoka mimi halina skimu hata moja. Kwa hiyo, haya yanayotajwa kama ndiyo faida za umwagiliaji kwangu kule bado ni ndogo kwasababu hakuna skimu hata moja. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho ahakikisha kwamba kuna skimu fulani inayopatikana jimboni Busanda ili watu wangu pamoja na kupata wakajifunze na waweze kupata uzalishaji huu ambao wenzetu maeneo mengine wanautegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza, pamoja na ongezeko hili bado asilimia 10 ya bajeti yetu iende kwenye kilimo ili tuweze kufanikiwa. Hii tulinayo, ukipiga hesabu utagundua ni one out of six. Kama tuna bilioni arobaini na kitu maana yake ni kwamba tulitegemea tupate trilioni nne. Kwamba kama tuna trilioni 41 tunategemea tupate trilioni ndani ya Sekta ya Uzalishaji, lakini ukipiga hesabu unaona hapa kuna bilioni 751 ukipiga ni one out of six, ambayo kimsingi ukifanya hesabu utagundua hii ni asilimia 16 mpaka 20. Naomba twende kwenye namba, namba hazisemi uongo. Tukienda vizuri naamini kwamba wananchi wetu wataweza kufanikiwa katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)