Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii muhimu na adhimu sana. Ni kama mwaka mmoja na nusu nilisimama hapa na nikasema juu ya mambo muhimu ambayo marehemu Hayati Baba yetu Dkt. Magufuli aliyasema kwa ajili ya kufanya Mji wa Mbeya na Mbeya nzima kuwa ni hub ya uchumi kwa nchi za Kusini mwa Afrika na katika mambo hayo nilitaja TAZARA, nilitaja Bandari ya Nchi Kavu Inyala lakini nikasema pia juu ya barabara.


Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninafurahi kusema kwamba ninawashukuru sana waliomshauri Mheshimiwa Rais kubuni mfumo wa EPC+F; na hao sio wengine ni Waziri wa Fedha ambaye anajua hizi ni kodi za wananchi ambazo zinaenda kulipa, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. Pia ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kulipokea hili. Leo Mbeya tunaenda kujivunia barabara ya njia nne, mbili mbili kutoka Igawa mpaka Tunduma, hili si jambo dogo. Ukilisema kwa maneno mepesi ni dogo lakini kwa kweli nataka niseme, Mheshimiwa Rais ametuheshimisha sana Mbeye, ahsante sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, tunaenda kupata bypass ambayo ina kilometa 48. Ndugu zangu, Tanzania tulizoea ni barabara moja inatoka huko mpaka inakoishia. Sasa kwa mfano mpya tutapata barabara mbili mbili kila upande kilometa 218. Mimi ni nani leo nisimshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan? Nitakuwa nimekosa kibali mbele ya Mwenyezi Mungu. Na mimi nataka niseme, kama kuna watu wataendelea kushukuru kama kuna watu wataendelea kupiga magoti basi mimi nitaendelea. Kama kuna watu wana wivu nikimshukuru Mheshimiwa Rais basi wanywe sumu wajinyonge, sisi tutaendelea kumshukuru. Haiwezekani leo unafanyiwa mambo makubwa kama haya kwa muda mfupi halafu usishukuru, kwani kuna tatizo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niseme, pamoja na haya mambo yote ambayo yamefanyika, nataka nikumbushe baadhi ya mambo katika hizo barabara. Barabara zetu zina matatizo makubwa sana, hasa kwa hawa wanaofanya usanifu. Kwanza ni wakatili wakubwa, wanawakatili walemavu, hawataki walemavu watumie barabara. Ninaomba kwenye barabara hizi zinazojengwa waache mambo ya kujenga vighorofa vya kupandia sehemu ambazo ambazo kunatokea overpass. Kwa nini msijenge subway ambapo hata mlemavu anao uwezo wa kupita, mtu anayetembea kwa mguu atapita? Mnapojenga vile vidude vya kupanda juu zile ngazi mlemavu hawezi kupanda, tuache ukatili. Ninaomba Mheshimiwa Waziri walisimamie hili, fedha ni za wananchi, walemavu ni walipa kodi pia, wapate ku-enjoy kwenye barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, inapoijengwa ile barabara, kuna barabara ambayo itakatisha inatoka Uyole kuelekea Kasumulu, tunaenda kufungua bandari. Wewe ni shahidi na wewe umeshuhudia kwamba sasa bandari yetu inaenda kufunguka. Malawi wataitumia sana, hawataenda tena Kusini kule Beila, wataitumia bandari yetu kwa sababu itakuwa attractive. Ninachoomba, tunapojenga hizi barabara tukumbuke kwamba kuna barabara inayotoka Uyole kuelekea Kasumulu ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo ninaomba niseme jambo moja ambalo ni muhimu. Jambo hili ni la pongezi nyingi kwa Serikali kwa sababu Serikali hii imekuwa Sikivu. Na leo nataka niwasifu Waheshimiwa Mawaziri wawili na niwashukuru. Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Ashatu Kijaji Waziri wa Viwanda na Biashara. Nawashukuru kwa sababu wamesikia kilio cha Wanakyela kwa kwenda kukomboa soko la zao la cocoa; ninawashukuru sana. Mmefanya kitu kikubwa na wananchi wa Kyela wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwakomboa kwa sababu leo wanatoka kwenye utumwa na fedha zinaenda kukaa mifukoni mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu malipo ya wafanyakazi wa Kiwira Coal Mine. Ninaomba nikumbushe, Mheshimiwa Rais tarehe 7 Agosti, 2022 alipofika Kyela mliahidi kuwalipa. Ninaomba hili lishikiliwe katika kipindi hiki. Hawa wananchi, hadi wengine wamefariki hawajapata hizo fedha. Wameahidiwa muda mrefu zaidi ya miaka 12. Ninaomba wananchi hawa wapate fedha zao na walipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kyela kuna eneo linaitwa Ikombe ninaomba, hata kama kwenye bajeti hakuna fedha, hata tunapojenga haya mambo ya barabara kubwa, trilioni 5.7 ni fedha nyingi mno kwa mwaka mmoja. Nimeangalia nchi nyingi nimefunua hakuna nchi ambayo imesaini mikataba na kujenga kilometa 2,035 kwa mpigo, hata Ulaya hakuna. Wakisaini sana ni kilometa 500. Sisi Samia amesaini 2,035; hii ni ajabu, na ukitaka kuweka kwenye maajabu ya dunia hili ni ajabu mojawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofanya haya ninaomba tusiwasahau wale waliopo kule chini. Kuna watu wilayani kwangu Mheshimiwa Waziri hawajawahi kuona barabara wala kuona gari, Kijiji cha Ikombe, wananchi kule wanakufa. Nimesema hapa mara nyingi, sio utani. Mheshimiwa Waziri nilikubeba hapa tukaenda; niliwahi kumbeba Mheshimiwa Mwenyekiti pale, alishuhudia kilio cha wananchi wa Ikombe wakitulilia. Ninakuomba Waziri, niko chini ya miguu yako, ninapiga magoti, twende tuwakomboe wananchi wa Ikombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nichangie ni juu ya mambo ambayo yanahusu mikanganyiko ya wafanyabiashara. Ninakuomba sana wafanyabiashara kukitokea tatizo tusiingie kwenye kutoa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Hitimisha hoja yako Mheshimiwa.

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba dakika nane zimeisha? Hapana ni dakika tatu hizi. Mimi nimehesabu dakika tatu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la ETS. Ninaomba sana hili suala ni muhimu hatutakiwi kuliacha, kinachotakiwa ni kuongeza wigo wa kwenda sehemu zingine. Lakini kwa mambo ambayo yanawaudhi wafanyabiashara ninaomba Serikali wafanyabiashara na watoa huduma mkae pamoja muyafanyie kazi haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaomba niishukuru Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa kunipa shilingi bilioni moja kujenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, halmashauri ambayo ilikuwa inakaa kwenye majengo ya mkuu wa wilaya, sasa tunaenda kujenga ofisi nashukuru sana Mungu awabariki sana na kwa maneno haya naomba niunge mkono hoja ahsante sana. (Makofi)