Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi nichangie lakini nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya hasa ya kupeleka fedha nyingi kule chini kwenye grassroot kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie jukwaa hili na nafasi hii kipekee kabisa kuwashukuru sana Watanzania wanaolipa kodi kwenye Taifa letu. Tumeambiwa takwimu zao kwamba ni wachache sana lakini wanabeba mzigo mzima wa watu milioni 61 na sisi tuna walipakodi tumeambiwa walioandikishwa hapa milioni nne na wanaofanya vizuri wapo. Nichukue nafasi hii niwashukuru sana Watanzania mnaolipa kodi kwa ajili ya Taifa letu. Kama unaona kuna mtoto anakwenda shule, kuna hospitali zinajengwa, kuna barabara zinajengwa ni kwa sababu yako wewe Mtanzania unayelipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo nitoe wito kwa Watanzania wengine na sisi tujisikie wivu kuchangia maendeleo ya Taifa letu. WHO wameainisha maeneo ambayo yanaweza yakasababisha tuka-improve biashara au tukafanya biashara zetu zifanikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa wanasema lazima tuweke mazingira mazuri kwenye biashara. Hawa Watanzania milioni nne wanaolipa kodi hebu tuwawekee mazingira mazuri tuwaheshimu, tuone kwamba jambo wanalolifanya kwenye Taifa hili ni kubwa sana. Kwanza tunapoweka mazingira mazuri tutaweza kukuza biashara, tutakuza uwekezaji, tutakuza ajira lakini tutajiletea maendeleo ya Taifa letu na wanaendelea kusema kwamba yapo mazingira tunayotakiwa kuongelea ambayo tutatakiwa kuyaweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuwe na mazingira huru ya biashara, tuwe na kanuni nzuri rafiki kwa ajili ya wafanyabiashara, tuwe na soko huria lakini tuwe na mipango ya kutafuta masoko mapya na kukuza masoko tuliyonayo. Kubwa zaidi tuwe na mipango ya kuwahakikishia wafanyabiashara mazingira mazuri ya kufanya biashara. Hapo ndipo tutakapoongeza hiyo tunasema tax base yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea suala la kuongeza au kutanua masoko tumeshaambiwa hapa. Tumeona kazi moja tu ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya ya Royal Tour, namna ambavyo imeongeza fursa mpya katika soko letu la utalii ilivyotanua soko letu la utalii na kuvutia utalii. Sasa tunatamani katika hiyo hali na sekta nyingine ziige ili kuweza kupalilia kile ambacho Mheshimiwa Rais amekifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba tunataka kuweka mazingira mazuri, tuongee tu kwenye utalii. Leo watalii wameongezeka lakini watalii wakija kutalii wanapenda wapate huduma stahiki, wanapenda wale bata. Leo watalii wetu wakiingia Tanzania hata uwezo wa kupata kubadilisha fedha za kigeni ni shida kutokana tu na kutokuwa na maduka ya fedha za kubadilisha yaani maduka ya kubadilisha fedha za kigeni hakuna. Taarifa inasema hapa mpaka Mei, 2023 tayari tuna maduka ya fedha tuliyoyasajili 11. Kule wakati kwenye semina tuliambiwa ni maduka nane yenye matawi 36. Kutoka kwenye Bureau de Change tulizokuwa nazo 2019, 400. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wazungu wakija Iringa hawana kwa kubadilisha dola ili waende wakale bata Ruaha. Sasa wale Mama aliokwenda kuwaita wanakuja, wanakuja huku wanakutana na broke hakuna pa kubadilisha fedha za kigeni wanarudi mwaka mwingine? Hayo ndiyo mazingira lakini kilichosababisha ni kutokuwa na kanuni rahisi za kufanya biashara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naona kwanza kwenye biashara hii kuna ubaguzi. Huwezi kuniambia umewapa watu leseni nane wana matawi 36 nchi nzima. Wenye capital requirement ya shilingi bilioni moja moja mmeanza kutubagua Watanzania kwa kuwapa fursa za kufanya biashara kwenye nchi hii watu wenye uwezo wa fedha. Tusio na uwezo wa fedha maana yake tusiwekeze wenye mitaji yetu midogo midogo. Hao mabilionea ndiyo wawekeze. This is not right! Lazima Watanzania wapewe fursa sawa ya kufanya biashara, huo ni ubaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kujenga imani kwa wafanyabiashara ni pamoja na kauli za viongozi kuzingatiwa. Watanzania wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo hii kama Rais atatoa kauli au atatoa maelekezo kwa idara yoyote au Wizara yoyote ya Serikali isipozingatiwa ni kumdharau Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo Watanzania watamwamini nani? Hata Mbunge nikaenda kusema kuna mpango mzuri huu hapa, kama Rais alitoa kauli haikuzingatiwa haikufanyiwa kazi, tunapoteza imani kwa wafanyabiashara kuendelea kuwekeza. Leo tuliambiwa kodi za miaka mitano Rais kasema miaka mitano ya nyuma, miaka sita zisichajiwe lakini hakuna lolote lililofanyika kwenye Mamlaka zetu kuhakikisha hilo halifanyiki na sana sana ukienda wanasema sisi tunasimamia sheria. Nchi hii Watanzania watamsikiliza nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Rais anapokuja anapotoa maagizo anakuwa ameshafanya tit for tat amejua hili linatakiwa mabadiliko ya haraka lakini haya mambo hayafanyiki ndiyo kuweka ugumu kwenye mazingira ya biashara. Watu wanashindwa kutanuka, watu wanashindwa kuwekeza kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ahadi za viongozi zitekelezwe. Mheshimiwa Waziri wa Fedha pale Iringa mwaka jana mwezi wa nane saa hizi tunakaribia mwaka mzima Mheshimiwa Rais alisema na kupitia wewe kinywa chako Mheshimiwa Waziri naongea na Mwenyekiti lakini kwa maelekezo ya Spika kwamba shilingi milioni 700 tutapewa kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya machinga. Wale machinga wakiwezeshwa kwenye mazingira yao hayo madogo wata-graduate watakuwa wafanyabiashara wakubwa kuja kuungana huku kwenye shilingi milioni nne. Tukiwawekea mazingira saa hizi ya kumaliza mitaji yao na kuua mitaji yao hatutapata wafanyabiashara wengine wanao-graduate kuingia shilingi milioni nne. Waongeze idadi ya shilingi milioni nne ifike sita wote wanatakiwa watoke huko kwenye biashara ndogo. Kwa nini tunashindwa kuona umuhimu wa kuwatengenezea mazingira mazuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mheshimiwa Waziri amesoma taarifa yake hapa kwamba anaziwezesha benki, Tanzania Postal Bank na ile benki nyingine wanazipa mitaji lakini kuna benki nchi hii Mheshimiwa Waziri ni community banks, benki ambazo mama ntilie wamechanga hela zao wamepata mtaji wamefungua community bank kama Mkoba Bank ya Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TRA mmewachukulia shilingi milioni 600 kutoka kwenye account yao kwamba wanadaiwa kodi za miaka hiyo ya nyuma sita, saba huko. Shilingi milioni 600 za mama ntilie wa nchi hii. Hivi Tanzania sisi huwa hatusamehewi kweli madeni huko na mataifa makubwa? Sisi tunakosa kuwasamehe mama ntilie unakwenda ku-freeze account yao, shilingi milioni 600 mama ntilie waliochanga wakaanzisha community bank yao kwa mtaji wao Benki ya Mkoba Tawi la NMB Mkoa wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipotengeneza mazingira dunia hii kila nchi inatengeneza destiny yake yenyewe. Tunaongea haya maneno ili wenzetu wayafanyie kazi. Kama benki nyingine unazipa mtaji unaziwezesha, kwa nini community bank usizisamehe madeni yao hii ili wale wakinamama waendelee kukopeshana wenyewe? Tusipoangalia tunapigana wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kingine ni cha mwisho. TRA nawaomba sana TRA wao ni Watanzania wanapata mental health bila sababu za msingi. Wanakuwa hawana afya nzuri za akili bila sababu za msingi wanakuja kustaafu wanakufa mapema bila sababu za msingi. Wanakosa marafiki mitaani bila sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiajiriwa TRA siyo kwamba umepewa kazi ya kutoa roho za watu. Salimia watu tengeneza mazingira mazuri, hawa Watanzania unayekuwa umemnunia unampa hiyo waliyosema Mheshimiwa Nyamoga lazima alipe shilingi 200,000 lazima akulipe wewe shilingi 50,000 ndiye aliyekuajiri, ndiyo anayekulipa hapo mshahara na kodi yako.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: …Kwa nini usimhudumie vizuri umbambikize kodi kwa sababu hajasoma halafu unakuja unasema usipojua sheria siyo sababu ya kutosamehewa sheria? Wewe ulisomeshwa na kodi yake ili umsaidie kumuelimisha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Jesca.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)