Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji katika hotuba hii ya bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifaya, hasa tuki-refer ukurasa wa 29 wa Bajeti ya Serikali, tumeona kwamba wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na vyuo vya kati vya ufundi wakitokea Kidato cha Nne wameondolewa ada, chuo cha DIT, Chuo cha Arusha Tech na Mbeya Tech, kwa hiyo hii inatupatia ma-technician na watu wengine wakati wa kuweza kusaidia hasa miradi hii mikubwa inayoendelea katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuanzisha program maalum ya mikopo kwa wanafunzi waliochaguliwa kwenda kusomea Vyuo vya Afya na Sayansi, Ufundi na Ualimu. Ni maendeleo makubwa kwa sababu wote Waheshimiwa Wabunge mnaelewa hali ambayo wananchi wamekuwa wanaipitia, ulikuwa ni usumbufu mkubwa sana lakini hii itatusaidia kupiga hatua mbele ili kipindi tunapata wale wa kada ya juu na hata kada ya kati pia waweze kwenda na sisi tuweze kwenda pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ninataka nichangie eneo moja, niki-refer ukurasa wa 80 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba acheni Watanzania walipwe pesa nyingi acheni Watanzania watajirike. Nataka nianze na statement hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Viwanda Biashara, Kilimo na Mifugo na wewe ni Mwenyekiti wangu wa Kamati, tunapotaja biashara sehemu kubwa tumekuwa tuna-refer hasa biashara ambayo inafanywa na wazawa. Mimi leo nataka nisimame kwenye habari ya wakandarasi wanaofanya miradi ya ndani. Kwenye hotuba ya CAG 2021 nakumbuka kulikuwa na riba zilizolipwa takribani bilioni 68.7 na wakati nachangia nilisema riba nyingi zinazolipwa, zinalipwa kwa wakandarasi wa nje, kwa sababu wakandarasi wa ndani huwa hatutozi riba. The moment mkandarasi wa ndani ametaka kudai riba kinachofuata kesho yake anapoomba kazi hatapewa. Ni haki yake kudai, lakini wale wanaompa kazi wanaona kama anawasababishia hasara, ingawa yeye kwa upande wake anapata hasara kwa sababu mabenki yanamdai na malipo yanavyochelewa analipa interest kwenye mabenki lakini anapotaka kudai yeye inaonekana si haki yake. Lakini wanapodai watu wa nje tunahangaika kuwalipa zaidi kwa sababu wao hawahofii kwamba utawanyima kazi kwa sababu wana sehemu nyingine za kupata kazi ila Mtanzania hana sehemu nyingine ya kupata kazi ispokuwa humu humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba kipindi tunatangaza miradi mizuri hii ambayo inakuja na bajeti kubwa ya trilioni 44, bajeti ambayo ina miradi mingi sana ya maendeleo na tukitegemea kwamba Watanzania wanaenda kunufaika huko, na ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais pia alishasema wakandarasi wa ndani wawe considered kwenye kazi na kwenye malipo. Sasa tuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakumbuke vijana wenzako wa Kitanzania, watu wengi sana wamechukua mikopo kwenye mabenki, kwa riba za juu sana asilimia 20 mpaka 22, lakini malipo ya wakandarasi wengi hayajalipwa kwa muda mrefu sana. Sasa wakandarasi wengi wanalalamika, Wabunge wengine wako humu ni wakandarasi na tuko humu tunafanya kazi hizi hali kadhalika tuna madeni makubwa tunadai hatujalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachoomba Mheshimiwa Waziri hili liangalie, kwa sababu kipindi hii miradi unaileta, wenzetu wanafilisika kwenye mabenki, hakuna benki inayouza nyumba unachofanya kila wakati unaomba extension ukimwambia hujalipwa na yeye anajua hujalipwa, yeye ana-extend lakini yeye anavyo-extend interest ya benki haisimami, utajiukuta mtu amefanya mradi wa bilioni moja bilioni mbili au bilioni tatu matokeo yake interest benki ameshalipa karibu milioni 500 hana faida tena. Kwa hiyo, tunaomba hili uliangalie ili uweze kuwasaidia wakandarasi wa ndani hatimaye waondokane na tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitu kingine ambacho Mheshimiwa Waziri nataka nishauri, kama inawezekana kuondoa adha hii inayofilisi wakandarasi wa ndani na pia kujikuta tunalipa pesa nyingi sana kwa wakandarasi wa nje kwenye issue ya riba. Kwa nini kusiwe na utaratibu maalum wa kuomba vibali kwako wewe kwenye Wizara ya Fedha? Mtu anapotaka kutangaza miradi mikubwa aombe kibali Wizara ya Fedha, mmhakikishie kwamba fedha ipo. Siyo Wizara inatangaza pesa halafu pesa ni mradi ambao unakuja kuomba pesa hazina, matokeo yake anapoomba pesa hazina unajikuta kwamba ile pesa kwako haipo au hujaikusanya, matokeo yake tunaanza kukulaumu wewe, kumbe na wewe hukuwa umetarifiwa wakati ile miradi inatangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe kama inawezekana iwepo procedure maalum ya kukuomba wewe kibali, utakapo ruhusu Wizara au Taasisi kutangaza maana yake pesa una uhakika nayo ili tusitoze riba kwa wakandarasi wa nje wanaotutoza lakini hali kadhalika wakandarasi wa ndani wasiumie, hilo naomba nimalizie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unakumbuka wiki mbili zilizopita Kamati yako ya Viwanda na Biashara na Kamati ya Bajeti tulikutana kwenye eneo la Wizara ya Kilimo pale, tukiwa na Waziri Bashe na hali kadhalika Waziri wa Viwanda. TBL walikuwa wametukaribisha pale wakiwa wanatangaza ufunguzi wa kiwanda chao kipya cha Kilimanjaro Breweries. Kiwanda ambacho wamehakikisha kwamba kitatumia shayiri ya ndani kwa asilimia mia kwa ajili ya kufanya uzalishaji wa bia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza mwaka 2021 hapa ndani ya Bunge lako, tulipitisha kushusha exercise duty kwa bia ambayo inazalishwa kwa kutumia shayiri ya ndani kwa asilimia 20 tukashusha kutoka 765 kwa lita ikaenda 620. TBL wakawa attracted kuwekeza kama siku ile ulivyosikia pale, hali kadhalika Waziri Bashe aka-attract watu kuwekeza kwenye ngano. Kwa hiyo, tulichokuwa tunategemea ni kwamba TBL wangesaidiwa ili ngano hii ambayo wamesema inakwenda kulimwa Makete, ngano inayoenda kulimwa Babati iweze kuwanufaisha Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake tunachokiona hapa, ile shayiri ya ndani huyu mtu amemaliza kuwekeza hajaanza kuzalisha anaanza mwakani imeongezeka tena 20 percent na shayiri ya nje imeongezewa tena 20 percent, inazidi kupanda lakini kwenye kuingiza ngano kutoka nje tunaona ngano ya nje inashushwa by 35 percent ninaenda 25 percent, sasa maana yake ni nini? Huyu aliyekuwa anataka azalishe kwa ngano ya ndani umempandishia halafu anayetoa nje umemshushia, tunaenda kuua hata hawa wakulima ambao juzi tuliambiwa wananufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili jambo aliangalie. Unajua unapoongeza wigo hasa kwa watu wanaoweza kuzalishia kwa ndani; kinachotusaidia ni kwamba, tutengeneze ajira za Watanzania walio wengi. Sasa huyu mtu kawekeza, kamaliza hapa tena, kodi zinaongezeka, extra duty inaongezeka, halafu import duty kwenye ngano ya nje inapungua. Tutakuwa hatujengi, ila tunabomoa. Kwa hiyo, naomba hilo mweze kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Mheshimiwa Waziri siku nachangia Wizara yako ya Fedha niliongea habari ya ETS, mimi ni mwaka wa tatu sasa unaenda niko kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara, Mwenyekiti wetu huyu hapa anaongoza kikao hiki, hakuna siku wafanyabiashara wamekuatana na sisi bila kuongelea habari ya ETS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, naomba kwa mara nyingine, Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya ku-rectify hili tatizo. Hatusemi yule aliyepo aondoke, kwa sababu tayari ameshawekeza muda mrefu, lakini kaa naye uone kama anaweza aka-adjust price. Kwa sababu leo ameenda kwenye sukari, ameenda kwenye cement. Ina maana tayari wigo wake wa kukuonesha kwamba mapato unayapata wapi, ni mkubwa. Angalia basi, wafanyabiashara wa ndani wasiendelee kulalamika kila wakati, inawaumiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, it is very bad, wafanyabiashara wanapokuja wanategemea Bunge liwasaidie na Bunge ni la kwao, lakini wanaona Bunge haliwasaidii, wameenda kwenye Kamati ya Bajeti hawasaidiwi, wamekuja kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara hawasaidiwi, basi tulilete kwa Mheshimiwa Waziri atafute jinsi ya kuwasaidia watu hawa ili tuwe na balanced state ambayo itaweza kusababisha wafanyabiashara wafanye vizuri na naye akusanye kodi yake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Waziri amekuwa muumini wa kusema kwamba unapokuwa na watu wachache uliowabana kwenye kodi haisadii zaidi ya kwamba wao wanaumia. Atengeneze wigo mpana. Wigo mpana ni pamoja na kuwa na hawa watu. Wasipolalamika, watawekeza zaidi, watapanua wigo wa kukusanya kodi, kuliko leo unapokuwa na walipakodi wachache huku ukiwakaba mashati mpaka damu ya mwisho wanaitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda na kwa nafasi hii, naunga mkono hoja. Nina uhakika kwamba Mheshimiwa Waziri kwa sababu ni msikivu, haya ameyasikia, atayafanyia kazi, hatimaye walipakodi katika mwaka wa 2023/2024 watalipa kodi huku wakiwa wanatabasamu, hatimaye tupate mapato haya ya kufanya miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru. (Makofi)