Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ili nami niwe mchangiaji katika bajeti hii ya Serikali. Awali ya yote naomba pia nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha jioni ya leo kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. Aidha, kama ilivyo ada nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashahidi, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameeleza bayana kwamba pato la Taifa limeongezeka kutoka bilioni 68 hadi 85, jambo hili ni la kujivunia sana. Jambo hili linajidhihirisha kwenye huduma za jamii katika maeneo tunayotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashahidi, kwenye Jimbo langu la Nanyumbu, miradi mingi ya maendeleo imefanywa ndani ya miaka hii miwili na mwaka uliokwisha. Kuna miradi mikubwa ya maji; Mradi wa bilioni 3.6 kwenye Kata ya Maratani ambao kwa kweli ni mkombozi wa wananchi wa Jimbo langu. Kuna Mradi mkubwa wa bilioni 3.4 katika Kata ya Sengenya, lakini tuna mradi wa bilioni 40 wa kutoa maji katoka Mto Ruvuma kuleta katika Mji wa Mangaka. Miradi hii ya maji ilikuwa ni kero kwa wananchi na imekuja kukomboa wananchi wa jimbo langu. Namshukuru sana Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mama yetu ameonesha ukomavu, amerudisha demokrasia. Sisi ni mashahidi, leo hii Vyama vya siasa vimeruhusiwa kufanya siasa, jambo ambalo lililkuwa ni ndoto. Vile vile, amerudisha mchakato wa Katiba Mpya, kwa kweli jambo hili jambo hili linatia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya miaka hii miwili tumeona kiwango cha investment kilichowekezwa ndani ya nchi yetu, zaidi ya trilioni 23, karibu nusu ya bajeti yetu imeingizwa katika uchumi wetu. Ni jambo la kumshukuru sana Mama amekuwa muungwana, wafadhili na wawekezaji wamekuja kuwekeza ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tuliona zile fedha za Covid ambazo kwa busara ameweza kuzitumia katika kujenga shule na miradi ya maji. Ndani ya Jimbo langu nimenufaika na hizi fedha za Covid karibu madarasa 68 yalijengwa. Vile vile, mradi wa maji wa bilioni moja ulijengwa ndani ya Jimbo langu na kuondoa kero hii kubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pato la mtu mmoja mmoja (per capita income) imeongezeka kufikia dola 1,252. Kwa hiyo, kwa haya yote na mengine namshukuru sana Waziri wetu wa Fedha na Naibu wake kwa ushauri mzuri wanaoufanya kwa Mheshimiwa Rais ambayo haya yote leo tunayoyaona yanafanyika ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie kidogo kwenye bajeti hii. Tumeona makadirio yetu ya kodi katika mwaka ujao wa fedha ni karibu trilioni 44.3. Makadirio haya ya kodi yanatokana na vyanzo mbalimbali, kuna direct tax na indirect tax, kwa hiyo hizi kodi ili zikusanywe lazima tuwe na watumishi waadilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, kuna vyanzo vya kodi ambavyo kwenye ripoti ya CAG vilileta hoja nyingi sana, ningemwomba Mheshimiwa Waziri aangalie kama kuna uwezekano hebu tubadilishe jinsi ya kukusanya hizi kodi. Mfano, ukiangalia taarifa ya CAG hii kodi ya withholding tax imekuwa na hoja nyingi. Waajiri wanakusanya withholding tax at source lakini hawapeleki TRA. Sasa nini matokeo yake? Matokeo yake yule mtu aliyekatwa anapoenda kukadiriwa kule TRA inaonekana hajalipa chochote. Kwa hiyo, yule aliyekata ananufaika lakini yule aliyekatwa inakuwa ni tatizo kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwamba, kwa nini tusitumie mabenki kukusanya hizi pesa na kuzipeleka TRA? Mwajiri alipe kama ilivyo deni la mhusika lakini benki ndiyo ikate hizi pesa na at the end of the day benki anapeleka TRA moja kwa moja na mtu anapotaka kujua amelipa kiasi gani anaenda kwenye website ya TRA ana-click button anapata kiasi alichochangia katika ile final payment analipa ile tofauti na jambo hili tutaondoa hata kero hoja za ukaguzi ambazo miaka na miaka tunakuwa tunakutana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye direct tax nyingine ambayo tumekutana nayo ni tumekuwa waagizaji wakubwa wa magari kutoka nje ya nchi, lakini watu wengi wameshindwa kukomboa magari yao kutokana na kodi. Sasa wakati umefika tukubaliane, mtu anapoagiza magari nje ya nchi alipe na kodi moja kwa moja. Kama kodi inajulikana ni shilingi milioni tano gari milioni 30 alipe milioni 35 moja kwa moja. Hii itasaidia sana kupunguza hizi bonded warehouse ambazo zinahifadhi magari miaka kumi, miaka 15 mtu hana hela ya kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo itatusaidia sana, kwanza itarahisisha kukusanya kodi kwa mara moja lakini pili itapunguza mzigo kwa watumishi wa TRA. Watumishi wa TRA kazi yao itakuwa inakuja tu paper work kuangalia hii ndiyo gari uliyoagiza? Hii ndiyo CC number? Hii sijui na nini na nini, at the end of the day maisha yanakuwa mepesi. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo tutarahisisha sana na kukusanya hela kwa mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye indirect tax, hii pia ni kodi ambayo mwananchi anaweza akalipa bila kujihisi kwamba amelipa kodi, hiki ndiyo chanzo ambacho tukitumie zaidi na zaidi, sasa nilikuwa nimeangalia hapa hawa ETS wao wameingiza katika baadhi ya bidhaa ku-stamp bidhaa zetu, kwa ku-stamp imesaidia sana, kwanza inamtambulisha kwamba hii bidhaa ni ya Tanzania lakini pili inarahisisha kuondoa bidhaa feki, tatu inaweza kujua ni kiasi gani cha kodi ambacho kinaweza kukusanywa kwa mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tuwatumie hawa katika bidhaa mbalimbali, hebu tuongeze wigo wa bidhaa zetu. Mfano Mheshimiwa Waziri amezungumza kuongeza kodi kwenye vifaa vya ujenzi, badala ya kuongeza kodi hebu tuende kwa utaratibu huu tuone tuki-stamp hizi cement tunayozalisha je, hatuwezi kukusanya kodi nyingi kuliko kuongezea wananchi kodi. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri katika maeneo hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho naomba tena nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Mheshimiwa Waziri wewe hujioni lakini umekuwa mtu laini sana, unafikika. Kulikuwa na Mawaziri hapa Waziri wa Fedha ananata huwezi kuamini kama huyu ni binadamu, lakini wewe tunakutana wewe Yanga mimi Simba tunachati unaondoka zako maisha yanaendelea, hii imerahisisha watu kukuambia mambo mengi ya msingi. Kwa hiyo, usiache tabia hiyo na wananchi wanakujua unafikika. Sasa kwa kuwa unafikika tunakuomba sasa urahisishe uwezekano wa wananchi kurahisisha maisha yao, kubali hoja zao zifanyie, kazi ndugu yangu Shabiby amesema hoja za wananchi zichukuliwe kama ni changamoto, zifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba tena nishukuru sana Serikali kwa miradi mbalimbali ambayo imeendelea kutekelezwa ndani ya Jimbo langu. Jimbo la Nanyumbu tulikuwa hatujawahi kuona barabara ya lami na taa za barabarani lakini ndani ya Mama Samia tumeyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo baada ya kusema hayo najua muda siyo rafiki naunga mkono hoja mia kwa mia, ahsante sana. (Makofi)