Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia. Mimi nitachangia masuala ya Bandari yetu ya Dar es Salaam lakini si kwamba nitachangia kwa sababu labda kuna sintofahamu fulani lakini nitachangia yale ambayo hata kama kusingekuwa na uwekezaji lakini haya ningeyasema kwa sababu nilishasema kwamba nitasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza nataka niseme tu na nitoe rai kwa Waheshimiwa Mawaziri wetu, kwamba haya yanayozungumzwa na wananchi kuhusu kuboresha mkataba wa utekelezaji huu unao kuja ni lazima yazingaitiwe. Lazima tuzingatie mkataba wa utekelezaji, tusiyapuuze maoni ya wananchi kwa sababu si kila mwananchi anayechangia basi anakuwa mpinzani wa Serikali, Hapana. Wako watu wazalendo ambao wanachangia kwa manufaa ya nchi. Kwa hiyo tuchukue mawazo yao mazuri yaingie kwenye hiyo mikataba ya utekelezaji, tusiwaone kwamba ni watu ambao labda wanapinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, kwenye uwekezaji kwenye bandari ndugu zangu ni kitu cha msingi sana. Kwa nini nasema hivyo? Mimi niko kwenye Kamati ya Miundombinu sasa hivi nafikiri karibia ni kipindi cha nne. Kamati ya Miundombinu tumetembelea bandarini pale zaidi ya mara tano sita. Ukisikiliza bandari kwa watu na yale mapato unayoambiwa kwamba yanakusanywa tofauti na faida wanayoileta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape mfano tu; kwa mfano mapato ya 2021/2022 ilikuwa ni shilingi trilioni 1,144 (shilingi trilioni 1.14). Matumizi ni shilingi bilioni 805, faida ni shilingi bilioni 339. Kwa hiyo ukiangalia matumizi ni asilimia 73 faida ni asilimia 27 hilo ni tatizo. Kwa nini nasema ni tatizo? Faida ni ndogo matumizi ni makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hata kwenye ushushaji wa mizigo; ushushaji wa mizigo 2019/2020 tumeshusha tani milioni 17.2; 2020/2021 milioni 17.6; 2021/2022 milioni 20. Sasa nia yangu ya kuzungumza ni kama reli ya standard gauge tunayoijenga ina uwezo wa kubeba tani milioni 25 peke yake ambayo imezidi uwezo wa bandari, hapo bado reli ya kati tunaifanyia ukarabati, bado reli ya TAZARA tunaifanyia ukarabati, bado kuna malori ya nchi nzima maana yake itabidi yasimame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama reli hii moja tu ya standard gauge ikichukua tani milioni 25 wakati bandari uwezo wake ni milioni 20 ina maana hakuna reli hata moja itakayofanya kazi. Sasa athari yake ni nini? Athari inakuja moja; kwenye malori tunaona kama yanaharibu barabara, yanaleta matatizo lakini ndio yenye mchango mkubwa na yenye ajira nyingi kuliko sehemu yoyote kwenye hii nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lori moja likitoka hapa kwenda Rwanda au Burundi linatumia lita 2,000 za mafuta, kodi ya Serikali kila lita inachukua shilingi 1,200, kwenye 1,200 ina maana Lori likienda hapa na Burundi katika lita 2,000 ina maana kodi inachukuliwa milioni mbili na laki nne kwenye trip moja ya Lori. Kwa hiyo lori likienda mara nne Burundi kwa Mwezi ina maana ni 8,800,000. Na ukiangalia mfuko wa barabara, nimeona hapa Wabunge wengi mnasema hapa barabara ndizo zinafungua uchumi. Barabara zinatengenezwa na magari kwa sababu zinatengenezwa na kodi ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama bandari yetu isipofanya vizuri, tunasema tu reli ikija barabara zitapona na mfuko gani utakaotoa fedha ya kutengeneza barabara kama malori hayatapata mzigo? Cha msingi ni kuhakikisha kwamba bandari inafanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba treni zinafanya kazi na malori nayo yanapata mzigo wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukisema usimamishe malori ina maana umeshapoteza ajira zaidi ya milioni moja, kwa sababu tayari malori yapo zaidi ya laki moja kwa hiyo kila lori moja lina Tingo, lina dereva na mafundi. Ukija malori yanakopita kuna guest houses kuna, mama ntilie kuna kila aina. Ina maana miji yote ya pembezoni isiyopitiwa na reli nayo itakuwa ndiyo biashara yao imekufa. Kwa hiyo cha msingi tuzingatie kuweka mikataba yetu vizuri lakini lazima tuweke uwekezaji, bila uwekezaji haitawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika kupitia bandari, tutabadilisha Ma-MD wa bandari lakini hakuna kitu. Nataka niwaambie nchi hii wazalendo ni wachache, wapigaji ni wengi. Pale pale bandarini utakuta mashine za kushusha unaambiwa zimekufa ilhali haizijafa halafu kuna watu wenye tender ya kuleta Spear wanaingia na kagari, wakitoka unaambiwa tumetengeneza milioni 500, kumbe ile mashine haijafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna kingine ambacho tulikigundua hata zile Meli ambazo zinapaki kule nje, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu juzi mmesema amesema kwamba demurrage charge ni dola 25,000 lakini zipo Meli ambazo zinalipwa demurrage charge mpaka dola 35,000 ambazo ni takriban milioni 95, ile kupaki tu. Kwa hiyo wakiharibu hivi vifaa wanafanya mpango na hawa watu wa bandarini, wakiharibu vile vifaa zile meli kule zinatengeneza faida huku zimesimama kwa sababu wanalipwa charge ya milioni 95, ya milioni 58 mpaka 60 huku meli imesimama, kwa hiyo uwekezaji kwenye bandari ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Watanzania tusiogope uwekezaji, 2014 walikuja hapa Qatar kuja kuwekeza kwenye ndege, tukaona aaa, amekwenda sasa hivi Rwanda Air. Rwanda Air asilimia 51 ni ya Qatar, sasa hivi anajenga uwanja pale iwe hub; kwa hiyo maana yake Watanzania, Wakenya, watu wa Afrika Mashariki na Kati tukitaka kusafiri kwenda Ulaya, kwenda wapi twende tena tukapandie Rwanda. Kwa hiyo tusiogope, kama uwekezaji Serikali ilishashindwa, imeshindwa, tuache wawekezaji lakini wawekezaji wenye mikataba mizuri yenye manufaa na nchi wawepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni masuala ya viwanda hivi vya nguo. Muda umeisha au niendelee mzee kidogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya nguo vya Tanzania.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, tumia sekunde 30 kumalizia muda wako, nyongeza hiyo.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nilikuwa nataka nizungumzie vitenge sasa hii habari ya sekunde thelathini haiwezi kutosha, ahsante.