Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nipate kuchangia kwenye hoja hii muhimu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja iliyoko mbele yetu. Sina mashaka na nia ya Serikali ya kuweza kuboresha hali yetu ya uchumi hasa ukizingatia bajeti imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka sasa tuna shilingi bilioni 44.4 nyongeza ya 7% kutoka bajeti ya mwaka jana lakini ninashukuru kwamba kiasi kikubwa cha Bajeti hii karibu 71% inatoka kwenye mapato yetu ya ndani lakini kabla sijaendelea nitoe shukrani zangu kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu mpendwa kabia anayefanya kazi ya kutukuka katika nchi hii kwa kutoa fedha nyingi katika miradi mbalimbali inayoendelea hata hivi juzi katika Jimbo langu la Kalenga tuliweza kusaini mkataba wa kujenga barabara mpya inayokwenda vijijini kutoka Wenda kwenda Mgama kwa shilingi bilioni 29.8 ni fedha nyingi kujengwa barabara kwenda vijijini lakini nashukuru zaidi alituongezea fedha kwa ajili ya kujenga kipande cha lami kinachokwenda kwenye Makumbusho ya Mkwawa. Kwetu sisi jambo hili ni la heshima kubwa kwa hiyo, nipende kumshukuru kwa niaba ya Wananchi wa Kalenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe pole kwa Wananchi wa Jimbo la Kalenga hasa Kata ya Maboga na Kata ya Mseke ambako wamevamiwa na simba na mpaka sasa simba zimeshakula ng’ombe zaidi ya 10. Niwape pole wote waliovamiwa lakini Serikali inafanya kazi. Tumesha shauriana na vyombo vinavyohusika na wako site wanajaribu kulikomesha kabisa tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia hasa kwenye eneo la utalii. Eneo la utalii ni eneo muhimu sana kwenye uchumi wetu wa Taifa linachangia 25% ya pato la kigeni (fedha za nje) lakini 17.5% kwenye Pato la Taifa na Nyanda za Juu Kusini kama tunavyojua, Nyanda za Juu Kusini bado ni kama bikra katika eneo hili la utalii kwa sababu maeneo mengi hayajapata kufunguliwa na tunaamini Mpango wa Serikali wa kuanzisha ile miradi ya regrow Nyanda za Juu Kusini itakwenda kusaidia utalii kuweza kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, rai yangu ni kwamba niiombe Serikali sasa iweze kuharakisha mipango yake ya kujenga hii miradi ya regrow pale Iringa kile kituo cha utalii kiweze kujengwa kama Serikali ilivyoahidi pia na maeneo mengine ambayo yatakwenda kurahisisha watalii kuweza kwenda Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na kumalizika kwa ule uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapokwenda kumalizia Uwanja wa Ndege wa pale Iringa ambao unaitwa Nduli ambao hauna sifa sana kwenye Taifa hili la Tanzania; maana Nduli Iddi Amini kwetu huku tukimzungumza kwa kweli ni kichefuchefu. Ningependa, kwa ushauri wa wananchi wa Mkoa wa Iringa kwamba ule Uwanja wa Ndege wa Iringa unaoitwa Nduli sasa uitwe Mkwawa, kwa sababu Mkwawa ni jina la kitaifa katika nchi hii kwa mambo mengi ambayo yalifanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie pia kwenye utalii. Nilikuwa nashauri kwa sababu Mbuga ya Ruaha imekuwa ikikauka mara nyingi kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu zinazoendelea katika maeneo mbalimbali, kwa hiyo ile mbuga imekuwa ikikosa maji. Sasa kuna mpango wa kujenga lile Bwawa la Lyandembela au Lugodaluchali, ambalo bwawa lile ni kubwa kama likijengwa inaonekana litakuwa na kina kirefu sana hata kuliko haya mabwawa mengine tunayojenga, kama Bwawa la Kidunda, ambalo ujazo wake unakisiwa kuwa utakuwa na mita za ujazo milioni 350. Kwa hiyo hili bwawa tukilijenga litaweza kutiririsha maji angalau mita sita kwa mwaka ambayo yataweza kutiririka kwenda katika maeneo ya Madibila kwenye yale mashamba ya mpunga. Maji mengine pia yatakwenda Mtera, Bwawa la Kihanzi na hatimaye Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali itaamua kujenga bwawa hili itakuwa ni rahisi kwanza kudhibiti ule mtiririko wa maji. Kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba, kwa kuwa Wizara ya Maji imefikiria kulijenga bwawa hili ningeweza kushauri pia hata wenzetu wa utalii katika hii miradi ya REGROW wafikirie namna gani wanaweza kushirikiana kwa sababu bwawa lile ni likubwa na linagharimu fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwa kuwa sasa nchi yetu inakuwa katika eneo la utalii, changamoto tuliyonayo nchi hii ni katika kutoa huduma hasa kwenye maeneo ya hoteli. Huduma zinazotolewa na hasa wafanyakazi wetu hawana ujuzi wa kutosha. Ningeomba Serikali ione namna gani tunaboresha huduma (hospitality) ambazo kwenye hoteli si nzuri. Sasa ukuaji wa uchumi katika maeneo haya ya utalii uendane sambamba na zile huduma ambazo tunazitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza kwenye eneo la kilimo. Tunaishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya mbolea, wananchi wengi wamepata. Lakini ushauri wangu kwenye hilo, ili tuendelee kuongeza uzalishaji ambao utakula fedha nyingi kaka yangu Mwigulu ningeshauri yafuatayo. Kwenye upande wa mbolea tuhakikishe kwamba vituo vya kusambazia mbolea tunavisogeza viwe karibu na maeneo ya wakulima lakini mbolea pia iweze kupatikana kwa wakati. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuzalisha zaidi na tutaweza kukupa fedha nyingi ili wewe uweze kutekeleza miradi mingi ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeshauri, ukiangalia kwenye Kata ya Nzihi katika Jimbo la Kalenga ndiyo kata kame kwenye Jimbo langu la Kalenga. kwa hiyo kulikuwa kuna mpango wa kujenga bwawa miaka mingi iliyopita. Tangu mwaka 2008 utafiti ulishafanyika, walishafanya angalau upembuzi kwa kiasi fulani. Kwa hiyo ningeiomba Serikali iendelee sasa na mpango wake wa kulijenga lile bwawa na kukarabati skimu mbalimbali zilizoko kwenye Jimbo la Kalenga. Tuna skimu takriban 19 ambapo tutakuhakikishia kwamba tutaongeza kilimo lakini utaweza kupata pesa nyingi kutokana na hili eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye wakulima; mwaka jana tunashukuru tulifanya usajili wa wakulima wengi, lakini wapo wakulima ambao kwa bahati mbaya hawakuweza kusajiliwa. Ningeomba Serikali iweze kuchukua hatua sasa waanze kusajili wakulima sasa ili wakulima wengi waingie katika hii fursa ya kupata mbolea za ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulishauri ni kwa upande wa ulipaji kodi. Wapo Watanzania wenzetu wengi ambao wamekuwa wakikwepa sana kodi na wakati mwingine kuisingizia TRA, kwamba TRA wamekuwa brutal, lakini wao wengi wanaongoza katika kukwepa kulipa kodi. Sasa kama ukikwepa kulipa kodi tutatekelezaje miradi hii mikubwa namna hiyo? Kwa hiyo mimi ningeomba Watanzania wenzangu wafanyabiashara, suala la kulipa kodi ni suala la lazima na suala la kutoa risiti za eletroniki ni suala la lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione namna gani inaweza kufanya mifumo mbalimbali ya ukusanyaji wa fedha iweze kusomana ili kuziba mianya ambayo inapelekea leakages, fedha kuvuja katika maeneo mbalimbali. Hili nalo liweze kuangaliwa, Serikali iharakishe sana mifumo yake ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali isomane na iwe rahisi. Hili ni jambo ambalo ni muhimu sana tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri, kwa kuwa umefanya marekebisho ya kupunguza na kuongeza kodi katika maeneo mbalimbali, ningeshauri katika eneo la majengo na eneo la ardhi hasa eneo la viwanja; huku kuna fedha nyingi sana ambayo imelala. Watu wengi hawalipi kwa sababu kama mnavyojua hali ya uchumi imeathirika sana duniani hata mfukoni namo mmepata changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningependa kushauri kwamba, zile faini ambazo zinatolewa kwenye kodi za majengo na kwenye kodi za viwanja ziondolewe angalau kwa kipindi cha miaka miwili, na tuendelee kuhamasisha watu waweze kulipa hizi kodi. Hata kwenye majengo ya Serikali hata taasisi nyingine zinadaiwa fedha nyingi sana na hizi faini zimelimbikizwa, zipo nyingi. Tafuteni namna ya kulifanya hili. Mkifanya hivyo ninaamini mtakwenda kupokea makusanyo mengi sana na yataweza kusaidia kuingia kwenye mfumo na hizi fedha tuweze kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kama Mwenyekiti wa Mazingira ningependa kushauri, hakuna uchumi bila kutunza mazingira. Suala la mazingira katika nchi hii ni baya zaidi. Tafiti zanasema kwamba ifikapo mwaka 2030 asilimia 66 ya ardhi inayolimika, itakuwa hailimiki kwa sababu ya uharibifu wa mazingira. Ukiangalia kile kilichotokea Malawi, mmomonyoko wa ardhi na mafuriko ambao umeleta hasara ya karibu trilioni moja na milioni mia mbili, watu takriban elfu moja wamekufa ni kwa sababu mazingira yameharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nitoe rai katika eneo hili kama tunataka kuendelea kuwa na uchumi suala la uharibifu wa mazingira lichukuliwe kipaumbele na Serikali itumie nguvu zake za kisheria kuzuia ukataji wa miti na kuhimiza upandaji wa miti. Ukipita kwenye ndege hapa utakuta kwenye vilima vingi ni mawe tu ndiyo yanayoonekana. Hii inaonesha ni kiasi gani mazingira yameharibiwa. Kwa hiyo kwa hili niwaombe sana hatuna uchumi bila mazingira kwa hiyo Serikali iweke sheria kali. Hakuna kukata mti katika mlima wowote katika nchi hii. Kama kuna watu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: …itapaswa ijengwe kwa mikataba maalum, nakushukuru sana napenda kuunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)