Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia bajeti yetu ya trilioni 44 ya mwaka huu. Kwanza, nianze kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mzuri na kwa kuja na bajeti ambayo inakwenda kutatua matatizo ya Watanzania wengi. Tunampenda Rais wetu, maono yake na dhamira yake ya kuondoa matatizo kwa Watanzania inaonekana wazi na tunamuunga mkono Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, pamoja na Mheshimiwa Hamad Chande, kwa uongozi wao mzuri wa Wizara ya Fedha na Mipango. Hakika Wizara hii imepata viongozi wenye maono, kazi zao zinaonekana na sisi Wabunge na Watanzania tunawaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee vile vile kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara, walioniona mwaka ule wa 2020 wakaamua kunileta Bungeni kwa dhati kabisa ili niweze kuwatetea, kuwatumikia, kulinda masilahi yao na kwa kweli kazi hiyo naendelea kuifanya. Kwa mara nyingine niendelee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara kwa kuweza kuniamini na kazi yao naendelea kuifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na maeneo manne ambayo nakwenda kuchangia. Eneo la kwanza niende kwenye miundombinu na vifaa vya zimamoto hapa nchini. Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa na Jeshi la Zimamoto ambalo halina vifaa kwa ajili ya kuzimia moto. Yapo maeneo ambayo imewahi kutokea majanga ya moto, Watanzania wanakimbia wanasimama uwanjani wanashuhudia namna ambavyo mali zao zinavyoteketea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo la Ngara, kuna wakati tulipata majanga kama hayo, tulilazimika kwenda kuazima helkopita ya kuzima moto kwenye kanchi kadogo. Kwa kweli jambo lile lilituumiza Watanzania na lilitufedhehesha, kwa sababu kama Taifa tuliona kuna haja ya kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kuliwezesha Jeshi letu la Zimamoto ili liweze kupambana na majanga ya moto yanapotokea nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti hii tumeiona dhamira kubwa ya Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwasaidia Watanzania ambapo ametenga dola milioni 100 kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Ndani iweze kununua vifaa vya kuzimia moto, kama helkopta na magari ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwaomba Wizara ya Fedha na Mipango, kaka yangu Mwigulu aende akakope hizi dola milioni 100, atafute mikopo ya masharti nafuu, walete magari na mimi Ngara kwa kweli naomba niwe wa kwanza kupata gari hili. Maana nimeendelea kuwatetea na nimeendelea kulisemea hili na sasa naona mwelekeo ni mzuri. Tumetenga dola milioni 100 kwa ajili ya kwenda kununua mitambo hii ya kuzimia moto hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili huenda Watanzania wengi hawajalielewa, iko hivi; hakuna mwekezaji wa aina yeyote atakubali kuleta fedha nyingi kuwekeza kwenye nchi ambapo ile miundombinu yake ikipata moto itaungua na kuisha na hakuna vifaa vya kuweza kuzima moto huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji huu unakwenda kuongeza confidence kwa wawekezaji hapa nchi ambao wataleta mitaji yao, mali zao na mitambo yao na endapo itatokea majanga ya moto tutaweza kuyazima. Hongera sana kwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuliona hili na pongezi nyingine zimwendee Waziri wa Mambo ya Ndani, kaka yangu Hamad Masauni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kwenye kodi ya asilimia mbili ambayo imeletwa kwa ajili ya wachimbaji wa madini. Kodi ya asilimia mbili ku–introduce kwa mara ya kwanza kwa ajili ya wachimbaji wa madini nchini ni kubwa mno, ambayo badala ya kwenda kujenga inakwenda kubomoa na pengine wachimbaji wa madini nchini wanaweza kuanza kutorosha madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili eneo la kodi za madini kwanza tuna ada ya ukaguzi ambayo inatozwa tozo ya asilimia moja. Wakati huo huo kuna mrabaha, huu mrabaha ni asilimia sita. Vilevile kuna service levy, 0.3 percent, wakati huo huo kwenye kila halmashauri kuna tozo, ushuru mbalimbali wa Mwaro, karasha, viroba na kadhalika. Hii nayo iko estimated kama asilimia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kodi hizo ambazo jumla yake ni asilimia 8.3, sasa hivi yamekuja mapendekezo ya kuongeza kodi ya mapato ya asilimia mbili. Introduction ya kodi ya mapato ya asilimia mbili kwa mara ya kwanza ni kubwa. Kwa unyenyekevu mkubwa Mheshimiwa Mwigulu naomba a-note hiyo, nimwombe kabisa badala ya kutuletea kodi hii ya mapato ya asilimia mbili, watuwekee asilimia moja. Watujaribu kwanza wachimbaji wa madini tuone kama inatekelezeka hii asilimia moja kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakileta asilimia mbili watu wataona hii asilimia mbili ni kubwa na matokeo yake watu wataanza kupitisha madini kwa njia za panya, watu watajificha. Jamani hivi kweli waliona wapi tuna-introduce kodi ya mapato kwa mara ya kwanza tunadumbukiza asilimia mbili yote hiyo? Jumla inakuwa ni asilimia 10.3, it’s a lot. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kabisa kwenye eneo hili, iwe ni asilimia moja pekee itatutosheleza, tui–test kwanza kwa mwaka wa kwanza. Mwakani ikienda vizuri waongeze hiyo nyingine iwe asilimia mbili na hapo mambo yatakwenda sawasawa. Naomba eneo hili kwa kweli lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri wa Madini pamoja na Mheshimiwa Rais wamelitendea kazi eneo hili la madini. Mazingira ya uwekezaji kwenye eneo la madini sasa hivi yamenyooka na yako sawasawa. Madini sasa yanachimwa kwenye maeneo ya TFS kwa kufuata sheria za nchi, kwa kulipia misistu, kulipia ada ya kukaa kwenye lile eneo na sasa nimeona kuna initiative ambayo tumeendelea kuizungumzia ya kumwomba Mheshimiwa Rais aridhie baadhi ya maeneo ambayo yako kwenye TANAPA yamegwe yarudishwe kwenye TFS ili nchi yetu iweze kuchimba madini kwenye maeneo hayo ili tax iendelee kukusanywa kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumwomba Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aridhie yale maeneo mengine ambayo hata sungura hakuna pengine kuna nyoka na ndege, maeneo hayo ayalete hapa Bungeni tuweze kuyaondoa kwenye TANAPA yaingie TFS, ili Watanzania wachimbe madini waweze kufaidika ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni eneo hili la kuruhusu kuuza mazao nje ya nchi ambalo kwa kweli limeendelea kuongelewa tangu jana na Wabunge wengi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ametoa ufafanuzi. Iko hivi, yako makampuni ambayo yameomba vibali vya kusafirisha mahindi, maharage na mazao mengine nje ya nchi. Vilevile makampuni haya yana vibali vyote vinavyowaruhusu kufanya biashara hii kuanzia kusajiliwa BRELA, kuwa na TIN na vibali vingine ambavyo Waziri wa kilimo amevielezea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa hakuna sababu ya kusubiri, wanasubiri nini? Nawaomba hawa ambao tayari wana vigezo vyote wapewe vibali. Kama mtu ameomba tani 1000 kama shida ni ku–restrict, basi wampe hata tani 200 waaachane na 1000, kwa sababu hatuwezi kusimamisha maisha ya Watanzania, lazima waendelee kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani kwenye Jimbo langu la Ngara, jana nimewambia wafanyabiashara wote wanitumie zile nyaraka zao, wote wamesajiliwa na wana leseni. Vile vile, kwa bahati nzuri nimemtumia Waziri wa Kilimo. Nimemtumia Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, nimemtumia Dkt. Kessy ambaye ndiye anayeratibu vibali. Niombe wafanyabiashara wangu wa Jimbo la Ngara, sisi Ngara hatuna njaa, tunalima mara mbili kwa mwaka na mazao ambayo tulishavuna msimu wa kwanza bado yako majumbani. Wanatuchelewesha kufanya biashara kwa sababu kama njaa ziko katikati ya nchi, Wizara waje kununua kwetu, tuwape mazao. Niwaombe Wizara ya Kilimo, makampuni yote ambayo yamekidhi vigezo wawaruhusu waanze kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni makampuni ambayo hayana vigezo na hapa naomba Watanzania wamwelewe Waziri wa Kilimo. Sisi ni Taifa huru, haiwezekani mtu akatoka nchi jirani anaingia Tanzania na gari lake au lori lake, anakwenda kwa wakulima, anaaanza kukusanya mazao, anapakia mzigo anaondoka na anakwenda anawalipa madalali anavusha mzigo, anatoka nje ya nchi bila kulipa kodi haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania kwenye eneo hili tumemwelewa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, aendelee kuwabana, lakini wale Watanzania ambao wameshakidhi vigezo, Waziri wa Kilimo awaruhusu waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kundi lingine la sorrow proprietors, ni Watanzania ambao wameendelea kufanya biashara hiyo bila kuwa na makampuni au kusajiliwa BRELA. Naomba hawa nao waweze kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)