Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema kubwa ya kutuwezesha kuwa hapa kwa ajili ya kupigania maslahi mapana ya Taifa letu. Aidha, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya bajeti hii yenye maono makubwa yanayoelekea kustawisha ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimeisoma bajeti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri mbele ya Bunge lako tukufu na nimeona nichangie mambo machache; moja ni suala la ulipaji kodi; nchi yetu inao uwezo mkubwa wa kujiendesha kibajeti kwa kuwa ina maeneo mengi ya kukusanya kodi hususan kupitia nyanja mbalimbali za biashara, za uzalishaji, lakini jambo kubwa linalokosekana ni elimu, utayari, sheria na msukumo wa uhakika katika suala la ulipaji kodi. Ni ukweli usiopingika kuwa wananchi wengi hawana utayari wa kusimamia masuala ya kikodi hususan utoaji risiti, jambo hili linaturudisha nyuma.

Pili ni suala la makubaliano yasiyo rasmi katika ulipaji kodi, kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara wasio waaminifu kufanya makubaliano ya kulipa kodi nje ya utaratibu na kuwanufaisha watumishi wachache wasio waaminifu wa mamlaka za mapato huku wao wakilipa kiasi kidogo cha kodi. Kupitia mwenendo huu Serikali inapoteza mapato mengi na kupelekea uhafifu wa kutekeleza malengo ya Serikali.

Tatu ni saula la mikopo kwa wazawa, kumekuwa na mwenendo wa wawekezaji au wataalam wazawa kukosa sifa za kiushindani katika masuala ya uwekezaji kutokana na kutokuwa na mitaji ya kutosha. Ni muhimu Serikali iweke sera ya kipaumbele juu ya wazawa kupatiwa mitaji kupitia mikopo inayotolewa na mabenki yetu. Kwa kuweka umuhimu wa jambo hili kundi la wanawake ni moja ya eneo ambalo Serikali inaweza kuwekeza mtaji na kuwa na uhakika wa matokeo chanya.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni sera ya uwekezaji wa viwanda vya ndani na kilimo katika mazao ya kimkakati hususan chikichi, ngano na alizeti, ni lazima Taifa letu litoke kwenye mfumo wa kutegemea bidhaa kutoka nje na badala yake tuwe wazalishaji ambao kazi yetu itakuwa kutafuta masoko ikiwa tumeshajitosheleza. Hivyo nashauri maeneo haya muhimu yapewe kipaumbele ili kuweza kujitegemea kupitia soko la ndani na kuokoa fedha nyingi inayokwenda nje kwa ajili ya kuagiza bidhaa ikiwemo mafuta na ngano.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.