Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kupongeza hotuba nzuri ya bajeti ikiwa ni pamoja na hatua kadhaa ambazo zimeelezwa kama vile kurejesha retention ya 20% ya kodi za ardhi na majengo kwa Halmashauri zetu, kuanzishwa kwa Single Window Payments System pamoja na Taarifa ya Kamati ya Bajeti ikiwa ni pamoja na maoni, mapendekezo.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya mchango wangu baadhi nimerejea mchango wangu wa Bunge la Novemba wakati Kamati zikiwasilisha taarifa za Kamati na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya ninayorejea ni umuhimu wa Taifa letu kuhusu namna ambavyo itanufaika na fedha za mifuko ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani. Zipo fedha kwa ajili ya grants ku-support nchi zinazoendelea katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Fedha hizi zingeweza kusaidia katika kujenga miundombinu ambayo itasaidia wakulima kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mifuko kama Green Climate Fund, Climate Investment Funds, Adaptation Fund na Global Environment Fund baadhi ya hii mifuko inatoa mikopo ya riba nafuu au ku-support miradi ambayo inasaidia kupunguza ongezeko la carbon. Kwa mfano Rwanda wamepata pound milioni 24.5 ambazo zilisaidia kuanzisha Rwanda Green Fund ambayo imewezesha kutoa renewable energy kwa kaya 57,500 na ilizalisha so called Green jobs 137,500.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo nashauri mapendekezo ya kutoza shilingi 20 kwenye cement iondolewe na mbadala wake iwe ni hizi fedha za mifuko niliyotaja kwa sababu nyingi kati ya fedha hizo ni grants.

Kuhusu ATCL, napongeza jitihada zote za kuongeza ndege, nashauri yafuatayo; pawepo route ya kutoka Dodoma kwenda kwenye Kanda Kuu kama vile kwenda Mwanza kwa maana ya Lake Zone, kwenda Mtwara kwa maana ya Southern, kwenda Mbeya kwa maana ya Southern Highlands, kwenda KIA na pia kwenda Kigoma. Ilivyo sasa kama abiria atatoka Dodoma anataka kwenda Mbeya, lazima kwanza aende Dar, akifika Dar anaanza upya safari na tiketi mpya kwenda Mbeya, hii sio sawa, tutafute namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, niliwasilisha mchango wangu wa kwanza kwa Maandishi na pia nilipata nafasi ya kuchangia kwa kuongea tarehe 21 Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango wangu wa awali, naomba kuwasilisha tena mchango wangu wa maandishi kwa masuala kadhaa, kwanza ni kuhusu Mradi wa REGROW; Mradi huu wa kuimarisha utalii Kusini ulisainiwa Februari, 2018 na Mheshimiwa Rais wakati huo akiwa Makamu wa Rais. Lengo la mradi huu ambao ni mkopo wa Benki ya Dunia wa USD milioni 150 ni kuboresha utalii Kusini, ikihusisha kuimarisha miundombinu ya kuwezesha kuinua utalii kama vile upgrading of 14 airstrips, barabara kama kilometa 2000 ndani ya mbuga, njia za kutembea kwa miguu kilometa 350, ujenzi wa Kituo cha Taarifa za Kitalii pale Kihesa, Kilolo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ni mradi ambao ulipaswa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano, lakini utekelezaji wake kwa kweli ni wa kusuasua. Nafahamu suala hili lipo Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini Wizara ya Fedha ndio mshiriki mkuu wa mijadala ya masuala yote ya mikopo na misaada, na mpaka kupatikana kwa fedha hizi USD milioni 150. Kwa hiyo inao wajibu wa kujua je, fedha hizi zinatumika kadri ya malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; kwa kuzingatia kwamba jitihada za kutangaza utalii kuanzia filamu ya Royal Tour zinaendelea kuongeza idadi ya watalii, ni muhimu sana mradi wa REGROW kasi ya utekelezaji ikaongezeka na kwa kuwa kupatikana kwa fedha hizi Hazina ilihusika, ni vizuri pakawepo mfumo wa kuitaka Wizara ya Kisekta kutoa taarifa ya utekelezaji ya miradi husika. Kwa hiyo, natamani kuona Serikali ikitueleza suala hili linaendeleaje.

Kuhusu suala la kodi kwa magari ya abiria; katika ukurasa wa 101 wa hotuba ya bajeti, imependekezwa kuwa magari ya abiria yatozwe viwango kadri ya idadi ya abiria. Hata hivyo nashauri kodi hii itizame pia umbali ambao gari inasafiri. Kwa mfano yapo mabasi makuukuu yanayosafiri mikoani ndani ya Wilaya, kwa mfano hapa Dodoma, yapo mabasi yanatoka mjini yanaenda vijijini kama vile Mvumi, Mlowa Bahi na kadhalika. Yapo mabasi huko mikoani ambayo yanatoka makao makuu ya Wilaya yanaenda vijijini umbali usiozidi kilometa 100 na yanapita katika barabara ambazo wakati wa masika hazipitiki kwa wepesi, kwa hakika basi la aina hii linaweza kusafiri wiki moja, wiki ya pili lifikie gereji, ni yale mabasi tunayoyaita spana mkononi.

Mheshimiwa Spika, sasa basi kama hili ambalo nauli kutokana na umbali unaweza kukuta nauli ni shilingi 5000 kwa kiwango cha juu. Kwa mabasi ya abiria 65 ni sawa na makusanyo ghafi shilingi 325,000, hapo bado mafuta na gharama nyingine za uendeshaji kama vile spare na tozo mbalimbali, je ni sawa basi kama hili kutozwa shilingi 2,200,000 kwa mwaka?

Mheshimiwa Spika, nashauri viwango hivi vitizamwe upya na ikibidi vizingatie masuala kama uchakavu wa gari na umbali linalosafiri, na suala hili lizingatiwe pia kwenye magari ya mizigo.

Mheshimiwa Spika, magari ambayo yameanza kuchoka, kodi isiwe sawa na magari ambayo bado hayajachoka. Kwa mfano tuangalie umri wa gari kama moja ya kigezo, kwa sababu gari ambayo imeanza kuchoka, kwanza inatumia mafuta mengi hii inafanya gari hilo kununua mafuta mengi na hivyo Serikali inapata fuel levy, na pia gari la aina hiyo ambalo ni spana mkononi pia linatumia spare mara kwa mara ambapo pia Serikali inapata kodi kupitia kodi mbalimbali kutokea kwa wauza spare.

Kwa hiyo ushauri wangu kodi hii itazamwe na ikibidi izingatie umri wa gari na umbali inaosafiri kwa upande wa mabasi ya abiria.

Mheshimiwa Spika, kuhusu sewa ya ukaa, naomba Serikali irejee mchango wa Mheshimiwa Kakoso siku ya tarehe 20 Juni, 2023 kuhusu namna ambavyo tunaweza kunufaika kama Taifa na utajiri wa misitu kupitia biashara ya hewa ya ukaa. Hii ni biashara kubwa, lakini inayohitaji utaalam wa juu sana kwa sababu inataka sio tu umakini, lakini imejaa ulaghai mkubwa miongoni mwa makampuni. Kwa mfano sisi watu wa Mufindi, Kampuni ya Green Resources Limited-GRL walinunua maeneo mengi ya vijiji na wananchi katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Njombe, wamepanda miti na wanalipwa fedha za hewa ya ukaa, lakini wananchi na wanavijiji hawapati kitu.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu kwa Wizara ya Makamu wa Rais-Mazingira nimeshauri kwamba tuliwekee mkazo eneo hili kwa kushirikisha sekta binafsi na NGOs, hili ni eneo ambalo Serikali hatujalitizama kwa kina, kuna fedha nyingi sana na Mheshimiwa Rais ushiriki wake kwenye COP 26 Glasgow ulithibitika kwa sababu alikuwa jasiri akayaeleza mataifa makubwa kwamba yanapaswa kuheshimu ahadi zao za kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu mataifa makubwa yanaongoza kuchafua mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, nashauri ndani ya Serikali tuweke mkakati maalum, tuwe na timu ya wataalam hata kwa kulipia, tuijue habari hii ya biashara ya hewa ya ukaa na masuala mazima yanayohusu mabadiliko ya tabia nchi, fursa zilizopo na kadhalika. Tusiwaze kupanda tu miti, zipo fursa nyingi, tujifunze Wilaya ya Tanganyika kwa kuanzia lakini tutumie Balozi zetu kama Ubalozi wetu wa Brasilia kujua nchi kama Brazil imefanikiwa vipi kunufaika na biashara ya ukaa na msisitizo wangu ni kushirikisha sekta binafsi, tusijifungie ndani kwa sababu ukweli ni kwamba utaalam wa suala hili ni wa kipekee, kwa hiyo, wakati huu tufanye ushirikishwaji, pia wakati huo huo kama ambavyo tuliwahi kuwa na mipango mahususi wa kuzalisha vijana wetu kwa ajili ya sekta ya oil and gas basi tutumie mfumo ule kuwekeza katika elimu kwa vijana wetu kwa ajili ya suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na yatokanayo ikiwemo biashara ya hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Spika, naamini Serikali ikikaa na Mheshimiwa Kakoso na baadhi ya wataalam itaona wapi pa kuanzia.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.