Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi nami kuwa mchangiaji wa jioni hii ya leo. Kama ilivyo ada nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai nami kusimama jioni hii kutoa mchango wangu. Nitaendelea kumsifia na nitaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kwamba baadhi ya watu hawataki. Ni bora niitwe chawa lakini niseme ukweli ili nafsi yangu ibaki huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya makubwa sana kwenye nchi hii, nami niendelee kumwambia Mheshimiwa Rais, yuko kwenye njia sahihi, yuko kwenye taaluma sahihi. Wanaotaka kumtoa nje ya reli hawataweza sisi tukiwepo hai. Tutaendelea kumuunga mkono na tutaendelea kumsifia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunamsifia Mheshimiwa Rais? Leo kwenye Jimbo langu, niliposimama kwenye Bunge hili kwa mara ya kwanza, nilisema tuitoe Liwale Kisiwani, ilikuwa haifikiki kwa mawasiliano ya simu wala kwa barabara, leo Liwale inawasiliana kwa simu, inafikaka. Kesho Liwale inaenda kutoka Kisiwani kwa upande wa Barabara. Sasa naachaje kusifia? Kwa wananchi wa Liwale, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jina lake linakwenda kuandikwa kwa wino wa dhahabu. Liwale ilipata wilaya mwaka 1975, mwaka 2023 Mwezi wa Sita tarehe 16 tunaenda kuandika mkataba wa kujenga barabara ya lami kutoka Nachingwea - Liwale mpaka Masasi. Makofi kwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeisoma hii bajeti. Hii ni bajeti yangu ya nane kwenye Bunge hili. Napenda kukipongeza chama changu cha Mapinduzi, na nina uhakika kitaendelea kudumu. Kwa sababu bajeti yake ukiangalia mwaka hadi mwaka inaenda kujibu changamoto za Watanzania, inaenda kujibu matatizo ya Watanzania. Kwa hiyo, kwa namna hii bajeti inavyokwenda kutekeleza; kwa mfano, kwa upande wa kilimo, tumeona fedha nyingi zimepelekwa pale. Lengo letu ni ku-modernize kilimo chetu kiende zaidi kwenye kilimo cha kisasa kiwe ni kilimo ambacho kinaongeza tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako matatizo ya bei za mazao ya wakulima. Ufumbuzi wa haya matatizo ya bei ya wakulima ni tija. Kama mkulima anaweza kuzalisha korosho kwa Shilingi 1,000/= kwa kilo, hata akiuza kwa Shilingi 1,500/= anapata tija. Kwa hiyo, nai-support hii bajeti kwa sababu inaenda kujibu matakwa ya wananchi wa nchi hii. Nani asiyejua kwamba tulikuwa na matatizo ya majengo ya shule za msingi, sekondari na vyuo? Hayo yote yametekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye jimbo langu, kwa upande wa afya, naingia madarakani tukiwa na kituo kimoja tu afya, na tulikuwa hatuna hospitali ya wilaya. Leo tuna hospitali ya wilaya, leo tuna vituo vitano vya afya. Sasa nani ataweza kusema kwamba hashukuru? Kwanza kwenye dini zote wanasema, usiposhukuru kwa kidogo na usipomshukuru mwenzio, basi hata Mwenyezi Mungu naye huwezi kumshukuru. Sasa sisi tunaendelea kupongeza kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa, mimi nimekabidhiwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye Jimbo langu la Liwale. Leo hii nakwenda kifua mbele, nina miaka miwili mbele tayari asilimia zaidi ya 70 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetekelezwa. Kwa nini Chama cha Mapinduzi kisiendelee kuongoza? Baada ya kuyasema hayo, naomba nitoe ushauri ufuatao:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti tumesema tumefuta ada kwenye vyuo vya ufundi na tumeweka mkopo kwenye vyuo vya kati, lakini turudi nyuma tuulize, zamani mimi nakumbuka waliokuwa wanafanya vizuri shule ya msingi walikuwa wanapelekwa shule za ufundi, nami ni muhanga wa watu hao. Hebu chukua historia, wewe umekwenda shule ya ufundi, umemaliza; umeenda chuo cha ufundi, umemaliza; mchukulie yule uliyemwacha darasa la saba akaenda shule hizi za kawaida, akachukua uhasibu, baada ya miaka 10 mkutane. Wewe una FTC yako, yule ana CPA yake ya uhasibu. Nani ana maisha mazuri? Mzazi gani atampeleka mwanaye akasome ufundi? Utakwenda kuhangaika na vyuma huko miaka nenda rudi wakati yule uliyemwacha darasa la saba, amekwenda amechukua uhasibu, leo ana maisha mazuri. Kwa hiyo, watu wanachotafuta zaidi ni maisha mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ni nzuri. Naomba tunapowahitaji hawa wahitimu wa vyuo vya ufundi, tuangalie wanakwenda kuishi maisha ya aina gani? Mchukulie fundi refrigeration. Amesoma refrigeration, yupo pale Muhimbili. Atahangaika na refrigeration pale miaka nenda rudi, lakini kuna mtu amekwenda pale kama mhasibu, kesho kutwa unasikia ana CPA, ana mshahara mzuri. Kuna mwingine anakwenda pale kama muuguzi, leo ni Mganga Mkuu. Wewe utakaa pale miaka 20 unahangaika na switch za umeme pale kwenye ma-fridge mpaka unastaafu. Kwa hiyo, tatizo kubwa lililowafanya watu waache huko kwenye ufundi, ni kwa sababu ya maisha yao. Kwa hiyo, tunapokwenda kuboresha hili, tuangalie na hilo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu alisema mwenyewe kwamba, kama walipa kodi kwenye nchi hii wakiwa wachache, wanaenda kubeba mzigo mkubwa. Kwa hiyo, kodi inakuwa kubwa. Ili kupunguza hii, ni kuongeza walipakodi. Ushauri wangu katika hili, tuje na mikakati ya kuongeza walipakodi kwenye nchi yetu. Watanzania kwa asilimia kubwa hawalipi kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchangiaji mmoja alisema asubuhi, na hiyo ni kweli kabisa. Leo ukienda Kariakoo kuna bei mbili. Kuna bei ya VAT na kuna bei isiyo na VAT. Maana yake ni kwamba wewe uchague. Ukitoa shilingi 10,000 utalipa VAT, ukitoa shilingi 7,000 hupati risiti. Kwa hiyo, twende na mikakati sahihi. Siyo tu kukabana na hao wachache, tuongeze na idadi ya walipakodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, niingie kwenye vifaa vya ujenzi. Nimeona hapo, Mheshimiwa Waziri amesema ameongeza ushuru kwenye cement. Hili jambo siyo sawa. Hili jambo haliwezi kuwa sawa. Kwa sababu gani? Leo hii yenyewe ni kwamba tayari vifaa vya ujenzi vipo juu. Sasa ukiongeza kodi tu kwenye hiyo cement, mambo yanaenda kuharibika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine wa mwisho kabisa, naiomba Serikali, tumezungumza sana masuala ya wanyamapori. Bahati mbaya sana kwenye Wizara ya Maliasili sikuchangia. Nataka niwaambie, pamoja na ngonjera zote, riwaya zote, sera zote, maelezo yote, hayatoshi, watu wanauawa, watu wanakufa, tembo wanakula mazao. Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yako, Waziri wa Kilimo kwenye bajeti yako, tenga kabisa fedha za kutosha tuletewe chakula sisi wakazi wa Mkoa wa Lindi. Hakuna mazao kule, mazao yote yameisha na tembo. Hakuna neno lolote lile mimi leo nikirudi Liwale kumwambia mwananchi wa Liwale jambo lolote juu ya tembo, akanielewa haiwezekani. Sana sana nitapigapiga chenga tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanyamapori, suala la tembo limetuharibia sana na linaharibu kabisa kabisa sura yote. Unajua mwenye njaa hafundishiki, mwenye njaa haelewi, mwenye njaa siyo mwenzako. Mtu ukitaka kumuadhibu mtu muadhibu na njaa. Sasa sisi Liwale tuna njaa na hii njaa siyo kwamba wavivu na hii njaa siyo kwamba mabadiliko ya tabianchi; ni tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ije na mkakati maalum unaoeleweka. Tunaomba kadhia ya tembo ichukuliwe kwa uzito mkubwa, vinginevyo inaenda kuharibu mazuri yote yanayoendelea kufanywa na Serikali hii na nimesema hapa tunampongeza sana Mama anafanya sana lakini kwenye hili la tembo…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: …linakwenda kumuharibia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)