Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya 2023/2024. Kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya nami nimeweza kusimama na kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nizungumze kwenye hizi barabara. Tumeona wenzetu wa Kusini sasa hivi wanasheherekea, wanashangilia wanasifia lakini yapo maeneo ambayo na sisi tumekuwa tukipiga kelele sana kuhusiana na barabara angalau za kuunganisha Mkoa na Mkoa ama Wilaya na Wilaya ambazo bado ni changamoto kubwa sana. Mimi ningeomba sana kwa Wizara ya Fedha tunayo barabara ambayo inatoka Mpanda inapita Kaliua kwenda Kahama, ningeomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi naye atusikie kwenye barabara hii, tumeshapigia kelele sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Tabora ni moja kati ya Mikoa ambayo kwanza ipo pembezoni lakini pili Mkoa wa Tabora ni moja kati ya Mikoa ambayo ina wakulima wengi, yaani sisi shughuli zetu za kutuingizia kipato ni kilimo. Sasa kama tunalima sana halafu tunakuwa hatuna barabara kwa ajili ya kusafirisha mazao yetu, hili jambo kwa kweli haliwezekani. Kwa hiyo, na sisi tuombe sana, tunaomba barabara inayotoka Mpanda kwenda Kaliua kufika Kahama ijengwe kwa kiwango cha lami ili iweze kurahisisha usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ambayo inatoka Tabora Mjini inakwenda Bukene kupitia Mambali. Hii barabara nimeiongelea sana Mheshimiwa Naibu Waziri hapa aliniahidi mara kadhaa kwamba hii barabara itajengwa kwa kiwango cha lami. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie katika bajeti hii angalau hata kilomita chache ili zingine ziweze kuingia baadae, nakuomba sana tusaidie ili kuweza kusaidia wananchi wetu wanaotoka Tabora, badala ya kuzunguka kwenda mpaka Nzega ili waende wakatokee waende Kahama wapite hapa wapite Mambali-Bukene waingie Kahama na mwisho wa siku wanafika mpaka Mwanza. Kwa hiyo, itatusaidia pia kupunguza safari kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusiana na hili ongezeko la kwenye masuala ya Utalii. Bado tuna safari ndefu sana kama mpaka sasa tunazungumzia ongezeko la kutoka dola 1,310 tumefika 2,527 kwa nchi yetu ya Tanzania yenye vivutio vya kutosha, yenye vivutio vizuri, yenye mambo mengi ya ajabu, mpaka leo tunazungumzia 2,527, bado tuna safari ndefu. Tuna sema tuko kwenye asilimia 93, Tanzania sasa hivi tulitakiwa kuwa tunazungumzia asilimia180 mpaka 200 kwa jinsi tulivyokuwa na vivutio vizuri, tulivyokuwa na vivutio vya kutosha, tulivyokuwa na maajabu mengi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe Wizara ya Fedha huku mnapata fedha na nilishawahi kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha “ukitaka kula sharti uliwe”. Mheshimiwa Waziri wa Fedha anachukua fedha katika hizi taasisi lakini fedha hazirudi kule kwenda kutekeleza majukumu. TANAPA sasa hivi wanazo hifadhi 16, TAWA wana mapori ya akiba ya kutosha, TFS wana misitu chungu nzima, sikuambii na huko Ngorongoro lakini kote huko tunakusanya mapato, katika mapato yale lazima tufike mahali tukubali kutoa ili tuweze kutengeneza tupate zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha huku kuna hela, huku fedha ipo, lakini tuwekeze ilituweze kupata tija kwenye hili suala la utalii. Kama Mheshimiwa Rais aliamua kwa dhati ya moyo wake kutangaza utalii, kazi aliyoifanya ni kubwa sana, kama Wabunge tunaendelea kushauri Wizara iangalie kwa jicho la tatu kwenye hii sekta ya maliasili na utalii ili tuweze kuongeza mapato pia yaweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya maliasili ina changamoto nyingi ikiwemo wafanyakazi wake kulalamikia maslahi yao, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha waangalie namna gani ya kuweza kuwasaidia watumishi hawa kuhusiana na maslahi yao, wanafanya kazi ngumu, wanafanya kazi hatarishi. Kwa kweli, mimi nimewahi kuhudumu kwenye Kamati hii ya Maliasili nimejionea mwenyewe, kuna maeneo unakwenda unasema hivi kuna Askari wako huku wanafanya kazi unaambiwa wapo wanafanya kazi. Sasa kwa nini tusiwaangalie na kuona ni namna gani tunavyoweza kuwasaidia ili kuweza kuongeza maslahi yao. Pia kazi hizi zinafanywa na wote ni za aina moja siyo tofauti lakini maslahi yao wanalipwa tofauti tofauti, sasa hii inavunja moyo wale wengine kufanya kazi kwa sababu wanaona kwa nini wengine wapate zaidi kuliko mimi wakati kazi tunayofanya ni ya aina moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Wizara ya Fedha liangalieni hili jambo, ondoeni matabaka ili kazi ziweze kufanyika kwa ufanisi. Kuna wakati mwingine mnasikia watu wanauawa, wanyama wanakufa, saa zingine watu wanakasirika wanaona ngoja na mimi nilale zangu bwana kwani nini? Lakini mkitengeneza mazingira mazuri kwa wafanyakazi wa sekta hii ya maliasili na utalii mimi naamini kabisa tutaongeza mapato kutoka hizo dola 2,527 tutafika mapa dola elfu tano na kitu, ushauri wangu kwa Wizara ninaomba sana wakichukua fedha wapeleke fedha ili kazi ziweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii ya utalii zipo taasisi za utafiti, hizi taasisi haziguswi kabisa, yaani hata ukifika bajeti yao yenyewe pia inakuwa haieleweki. Kwa hiyo mimi niombe sana kwenye Wizara ya Fedha angalieni hizi taasisi za utafiti ili ziweze kufanya kazi zao vizuri na waweze kuongeza tija katika suala zima la utalii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa mwanasiasa ni lazima uwe unaangalia mambo yote yanayoendelea, unasikiliza unajua kwamba wapi nini kinafanyika. Juzi katika harakati zangu nilimskia Mheshimiwa Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Chongolo akiwa Kondoa, migogoro inapunguza sana kasi ya uchumi katika nchi yetu, kama hatukuwa makini huu uchumi tunaouimba utaishia kwa watu ambao huku Mjini tu, lakini kwenye maeneo yenye migogoro tutausikia kwenye bomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Chongolo alikuwa kule kwenye pori la Mkungunero. Pale Mawaziri Nane wameshakwenda na pori lile wakasema kwamba tayari wameshalishughulikia lakini mpaka hivi tunavyozungumza wananchi wamekwenda kulalamika mbele ya Mheshimiwa Katibu Mkuu wa CCM. Nazungumza hivyo kwa sababu Tabora tuna mgogoro uliopo Kaliua na mgogoro huu hauna sababu hata kidogo, Mawaziri Nane wamekwenda katika Jimbo la Kaliua, Kata ya Ukumbikakoko na Usinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hawa walisema hawa wananchi Mheshimiwa Rais ameruhusu waendelee kukaa hapa hapa na ikiwezekana waongezewe na maeneo mengine pale, kwa sababu Serikali haina mpango wa kuyachukua. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi hawa, lakini cha ajabu Mawaziri Nane wameondoka kinachoendelea huko ni mgogoro ambao mtakuja kusikia mauaji ambayo hayana hata sababu zozote za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi lazima uwaguse Watanzania wote bila kujali watu wanaishi wapi. Sasa hawa wanaoishi na migogoro, ambao hawajui kesho yao itakuwaje leo Mheshimiwa Rais ameruhusu wananchi hawa waendelee kubaki lakini anakuja mwingine ndani ya Serikali hiyohiyo anapinga maoni ya Mawaziri Nane walivyokuja na kauli ya Mheshimiwa Rais. Sasa hivi tuseme hii Serikali iko tofauti ama shida ni nini?

Mheshimiwa Mwenyeekiti, nimeona niliseme hili ili mjue kwamba tunapozungumzia bajeti humu, tunapowasemea Watanzania, tunapomshukuru Mama kwa kuleta bajeti ya Watanzania lakini ajue kuna Watanzania ambao hawanufaiki na haya tunayoyazungumza kwa sababu ya migogoro waliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe sana kama inawezekana watenge fedha ziweze kusaidia hii migogoro iweze kupungua. (Makofi)