Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2023/2024 ambao imewasilishwa na Mheshimiwa Waziri kaka yangu Dkt Mwigulu Lameck Nchemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia uzima na kukutana asubuhi ya leo. Pili, kwa dhati ya moyo wangu na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki nasema hivi wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki walionipigia kura nyingi sana natamka hadharani kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika muda wa miaka miwili. Kazi kubwa aliyoifanya katika uongozi wake kudumisha demokrasia nchini, kuweka uwazi wa Serikali, diplomasia na kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo leo tunajivua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya na vijana siku hizi wanasema Mheshimiwa Rais anastahili kupewa maua yake ya kutosha kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa hakika wale wenye nia njema hawatakuwa na kusita kumpa maua yake, tumpe maua mengi Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea tabia ambayo nataka ienee katika nchi yetu, eti kwamba tusipongezane kwa mambo mazuri yanayofanyika, wengi wamefika mahali wanasema ukimpongeza unakuwa wewe ni chawa. Hata kwenye Biblia imeandikwa kwamba: “moyo usiyo na shukurani hukausha mema yote” Kwa hiyo Watanzania tusijengewe, kwa sababu tu humpendi Fulani, kafanya jambo zuri, mpongeze afanye kazi zaidi. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais anapofanya kazi nzuri, uungwana wa kawaida unatakiwa umpongeze kwa sababu anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo letu la Singida Mashariki, Wilaya ya Ikungi katika muda huu tunaoenda kumaliza bajeti ambayo tumeletewa, fedha tulizoletewa za kutekeleza miradi ni zaidi ya bilioni saba zimeshuka katika wilaya yetu. Kwa hiyo maana yake ni kwamba fedha nyingi zimeshuka kutekeleza miradi, si kwamba tunatarajia fedha zimekuja na hivi tunavyoongea miradi lukuki imetekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajivunia sana uongozi wa Mheshimiwa Rais, tunajivunia kiongozi wetu anavyofanya vizuri. Sisi wananchi kuna maeneo yalikuwa hamna madarasa, leo madarasa yapo, kulikuwa hamna vituo vya afya, kuna vituo vya afya, kulikuwa barabara zimejifunga, barabara zimefunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika Wilaya yetu ya Ikungi tulikuwa hatujawahi kuwa na lami, sasa lami inawekwa, tulikuwa hatuna taa za barabarani, tulikuwa gizani usiku, tunalala mapema, leo taa za barabarani zinawekwa. Tutakuwa watu wa ajabu kabisa bila kumpongeza Mheshimiwa Rais na kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri. Mzee Mkapa alisema kushukuru ni kuomba tena, tunaamini tunaposhukuru tunamwomba tena Mheshimiwa Rais atuletee fedha tuweze kuleta maendeleo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nampongeza sana Mkuu wa Mkoa ndugu yangu Peter Serukamba kwa kazi nzuri ya kusimamia shughuli za maendeleo, nampongeza sana DC wa Ikungi ndugu yangu Thomas Apson kwa kazi nzuri ya kusimamia maendeleo na nampongeza Mkurugenzi wetu Justice Kijazi kwa kazi nzuri ya kusimamia maendeleo. Hivi tunavyoongea tumepata hati safi kwa sababu ya usimamizi mzuri unaoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, naomba nichangie maeneo mawili makubwa ambayo yatasaidia katika kutoa ushauri kwenye bajeti yetu tunayoenda kuipitisha. La kwanza ni sekta ya uzalishaji, lakini pia nitaongelea ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Katika maeneo haya mawili nitaomba niende haraka kwa sababu yamejaa mambo muhimu kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni sekta ya uchumi, ambayo ni sekta ya uzalishaji upande wa kilimo. Kilimo kimeongezewa fedha katika mwaka huu wa fedha. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, tumpongeze Waziri wa Fedha, tuwapongeze kwa kuleta fedha nyingi katika kutupitisha zikatekeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili nitakuwa specific kwenye eneo la kilimo cha alizeti, kwa maana ya mafuta ya kula. Tulikuwa tukilalamika hapa nchi yetu ina upungufu wa mafuta ya kula mpaka tukalazimika kwenda kuagiza nje ya nchi. Tumekuwa tukitumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kununua mafuta nje ya nchi. Ukaja mkakati kupitia Wizara ya Kilimo, tuzalishe alizeti ya kutosha, wakaleta mbegu, wananchi wakawezeshwa, leo tunavyoongea wananchi wamevuna vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoongea bei ya debe la alizeti limeshuka, wananchi wangu wanalalamika. Wanaomba Serikali itusaidie kuhakikisha kwamba ili ile alizeti yao inawapa faida. Kwa hiyo nataka nimwombe sana Waziri ahakikishe kwamba tunasaidia zao hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hapa kwenye eneo na namna ambavyo tunapunguza kodi katika refined mafuta kwa asilimia 25 badala ya 35 ambayo tunadhani ingekuwepo. Niombe sana kwenye semi refined tunayo asilimia 10, lakini kwenye crude oil tunayo asilimia sifuri ili kusaidia viwanda vya ndani. Niombe sana kama tunataka kuendana na mpango mzuri wa Wizara ya Kilimo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha turudishe asilimia 35 kwenye refined hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanya hivi kutasaidia kupunguza mazao yanayotoka nje kwa maana ya bidhaa ya nje isiingie humu ndani ili tuweze kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha na tumsaidie mkulima aliyoko pale kijijini. Hiyo ndiyo itakuwa na maana kubwa kwa uwekezaji wa kilimo cha alizeti ambacho tunasema, pia itaongeza mafuta mazuri ya alizeti katika nchi yetu ambayo nje ya nchi wanayahitaji, maana yake tutauza mpaka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe ili kumkomboa mkulima na kwenda na kauli moja, kwa maana ya lugha ya pamoja, tunaomba sana tupandishe kuwa asilimia 35 badala ya 25 ambayo tunaipendekeza ambayo kiukweli itaenda kuua soko, itaenda kuua kilimo cha mwananchi wetu wa kawaida kitu ambacho siyo lengo la Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana hilo na Wabunge wengi wameshauri, naomba sana hili lichukuliwe na namwomba Waziri anapokuja kuhitimisha aje atuhakikishie hilo, wananchi wanasubiri huko nje, wanatuambia tusaidieni, tuokoeni tuweze kupata faida ya kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni suala la ununuzi wa ndege ya cargo ambayo tumeipokea juzi na Mheshimiwa Rais ametuongeza, tunapongeza sana. Maana yake ni kwamba leo tunakuwa na uwezo wa ku–export moja kwa moja mazao ya mbogamboga mpaka na mazao ya matunda ikiwepo parachichi ambayo inatakiwa sana duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili tumekuwa na mpango mzuri wa mazao ya mbogamboga horticulture katika maeneo yetu. Wizara ya Kilimo ina mpango mzuri kwa upande wa horticulture. Tunaomba sana sana kumekuwa na changamoto ya vifaa vya kuhifadhia mbogamboga pamoja na matunda. Tumekuwa na hizi cold rooms kwa maana ya tracks hizi ambazo zinasafirisha mazao yetu ili yasiharibike, lakini tumekuwa pia na cold rooms equipment’s ambazo zinatakiwa katika maeneo ya mashamba ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali na Mheshimiwa Waziri aje na mpango wa kuondoa angalau ushuru au kodi ili kuingiza vile vifaa ambavyo vinaenda ku–support kilimo cha mbogamboga katika maeneo yetu kwa sababu vile vifaa ni vya gharama kubwa. Wananchi wengi hawawezi wenye mashamba ambao wamejitahidi kuingia kwenye jambo hili na ili wawekezaji ambao wameamua ku–support na ile ndege ili ipate mzigo mkubwa wa kupeleka nje ya nchi, tuweze kuuza na kupata fedha za kigeni ili fedha za kigeni zije zisaidie hapa nchini, niombe sana Mheshimiwa Waziri afanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri akiweza kufanya hivyo atasaidia kilimo cha wananchi wetu ambao wameamua kujiwekeza kwenye eneo hili, lakini hii ndege ambayo tumeinunua itakuwa na maana kubwa ya kuhakikisha tunasafirisha mzigo kwa maana ya mzigo mkubwa kwenda nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni suala la ushirikishwaji wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu na naomba niseme wazi, nimekuwa nikiongea mara tatu hapa katika suala la bandari kwa muda mwingi sana. Niombe sana, eneo hili la bandari, bandari ndiyo kioo chetu. Kumekuwa na kauli mbalimbali na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu jana ametoa kauli nzuri sana kuhusiana na bandari, mawazo tutaendelea kuyachukua, hatutarudi nyuma tunataka tuwekeze ili tuongeze pato la Taifa, kusiwe na upotoshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili kuna makundi manne ambayo yanatukwamisha. Kundi la kwanza ni suala la wapinzani wetu kutaka kutuzuia tusiendelee. La pili, ni wafanyabiashara wasio waaminifu wameingilia mchakato huu ili wao waendelee kufaidika na udhaifu wa bandari yetu. Watu wa tatu ni baadhi ya wafanyakazi wa TPA na wa TRA wanaofaidika na mfumo huu mbaya wa kuendesha bandari yetu na watu wa nne ni bandari shindani zilizoko katika ukanda huu ambazo hazipendi sisi tufanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao DP World ni wana uwezo mkubwa sana. Niombe sana tuendelee kuwaza kwamba nchi hii haitauza bandari, bandari ni ya Watanzania, Mheshimiwa Rais ameshasema tuondelee hofu kwa sababu hatuna sababu ya kuogopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hofu hii ipo niongee hili neno dogo tu. Tulikuwa na stendi yetu pale Mnazi mmoja Kisutu, stendi ya Wananchi wa Dar es salaam waliandamana kwa sababu inapelekwa Ubungo wakasema ni mbali sana, wakaenda, tukaenda kujenga stendi Ubungo, leo Ubungo imeonekana ni mjini katikati, lakini leo tunavyoongea stendi iko wapi? Iko Mbezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi waondoe hofu nia yetu ni njema twende kuiunga mkono Serikali ili iongeze mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja ili iweze kupitisha bajeti hii ikalete maendeleo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)