Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii, lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia leo hotuba ya bajeti ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uendelevu wa kukusanya mapato ya ndani ambayo ni chanya. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa usimamizi mzuri, na Mawaziri wengine wa kisekta. Kumbukumbu zinanionesha hapa mapato yetu ya ndani, ukurasa namba saba, mwaka 2020/2021 yalikuwa trilioni 20.59, lakini 2021/2022 tukapata trilioni 24.4, hii 2023 ambayo ndiyo tunayo sasa mpaka Aprili tulikuwa na trilioni 21.67.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato yetu ya kutoka TRA kwa mwezi sasa yamepanda kuwa trilioni 2.63. kwa hiyo ukiangalia miezi iliyobaki hapa yatavuka trilioni 24 ya mwaka jana; ndiyo sababu nikasema kuna ongezeko chanya. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha kwamba hili limesimamiwa na mapato yetu hayaendi kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hili vilevile niwapongeze wale waliweza ku-introduce teknolojia hapa. Kuna EFD inafanya kazi kubwa ya kutoa risiti kwenye maeneo yetu. Kwa bahati mbaya sana watu wengi hawana uzoevu wa kuomba risiti na mwisho wa wakati ni kwamba kuna mahali mapato ya Serikali yanapotea. Kwa hiyo kwa hili pamoja na kushauriana sisi wenyewe lakini tunashauri vilevile wafanyabiashara wote wajiandae kuhakikisha kwamba wanapouza watoe risiti na sisi tunapoenda kununua tuombe risiti kwa ajili ya kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ETS ambayo nayo imesaidia kwamba bidhaa zetu zimekuwa stamped tuongeze tu wigo wa hiyo stamping kuhakikisha kwamba sasa tunaweza kuzitambua na mapato yetu yanaweza kuendelea kuongezeka yavuke hiki ambacho tunakiona. Maana tukiendelea kuwa na mapato mengi ya ndani kuna wakati tutafikia kama tukifanya vizuri sana tunaweza ku-support bajeti yetu kwa asilimia hata 75. Tukienda huko maana yake ni kwamba sasa tutakuwa tumeanza kusogea mbele zaidi kuliko ambako sasa hivi tuko. Kwa hiyo ushauri wangu kwenye Serikali hapa tuendelee kuangalia vyanzo vingine kuhakikisha kwamba mapato ya ndani yanaongezeka yaweze ku-support bajeti na miradi yetu mingi iwe financed kutoka kwenye mapato yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nitakalochangia ni sekta za uzalishaji, mara nyingi hupenda kuzizungumzia sana. Ili uchumi wetu uchangamke hatuna majibu rahisi, ni lazima sekta za uzalishaji zizalishe sana na mchango wa Pato la Taifa kutoka kwenye kilimo, mifugo na hata uvuvi uwe mkubwa. Ukishakuwa mkubwa, maana yake uchumi wetu utachangamka. Kwa nini nasema utachangamka? Mnajua kabisa dhima yetu ni kuwa na uchumi shindani na shirikishi. Sasa ili uwe shindani na shirikishi lazima tuwashirikishe wananchi wengi zaidi; na hawa wengi wameajiriwa kwenye kilimo, uvuvi na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hapa kwenye ukurasa namba 11 mwaka 2021/2022 tulibajeti kilimo bilioni 294 lakini mwaka 2022/2023 tukabajeti 954.0 billion. Mwaka huu tuna billioni 970.8 kuna ongezeko la kama bilioni 16.8 hivi. Hii nikiangalia mimi naiona kama ni ndogo kwa sababu ya ushirikishi ule wa wananchi wengi. Ningeomba tu twende tuangalie kwenye Malabo Declaration itakayotupeleka kwenye 10 percent kadiri tunavyozidi Kwenda, ili tuendelee kuhakikisha kwamba kilimo sasa kinaweza kuwa ndio uti wa mgongo wa Taifa. Kwa sababu tulitangaza kilimo uti wa mgongo wa Taifa kikiwa kinapewa bajeti ya bilioni 200. Sasa uti wa mgongo unaopewa bilioni 200 nafikiri maneno yalikuwa yamekosewa. Kwa hiyo niwaombe sana niishauri Serikali tuendelee kuongeza pesa eneo hili ili watu wengi waendelee kuajiriwa na kushirikishwa katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukaona kwa bajeti ile ya mwaka jana imesaidia upatikanaji wa pembejeo za kilimo lakini imetupatia kilimo cha mashamba makubwa (broke farms) ambayo yameanza sasa kuratibiwa na Waziri muhusika. Vilevile imepewa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, imeanza kushughulika na ujenzi wa skimu za umwagiliaji, na mwisho inatakiwa iendelee kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo. Ukiyaona haya yote yaliyotajwa kama yametekelezwa na yakitekelezwa vizuri maana yake hapa ndipo palipo na majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kulima sana ni lazima uchumi wetu uwe unaongozwa na soko, kwamba demand ya hiki kitu iko wapi, mahindi yanatakiwa wapi, alizeti inatakiwa wapi. Kama inatakiwa kwa wingi na hicho ambacho kinaonekana kwamba bei yake ikawa nzuri zaidi wakulima wataendelea kulima kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametoa ruzuku, lakini mwaka jana nilishauri Serikali kwamba ruzuku ile ya mbolea iliyotolewa wakulima wengi hawakufaidika nayo kwa sababu vituo vya upatikanaji wa mbolea vilikuwa mbali na wananchi. Mwaka huu viongezwe ili kuhakikisha kwamba vinawakaribia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ruzuku hii wananchi wengi ambao walitakiwa kujiandikisha hawakujiandikisha wengine. Kwa hiyo tuombe sana sasa daftari la kujiandikisha lifanyiwe uhariri upya ili wajiandikishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hii ruzuku ya mbolea iliyotolewa hapa tuhakikishe kwamba huduma za ugani kutoka kwa hawa maafisa ugani zinapatikana ili wananchi wajue ni namna gani ya hiyo ruzuku ya mbolea kuitumia kwa ajili ya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwenye kilimo hapa nizungumzie skimu za umwagiliaji. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwamba niliona hata kule Buzanda kuna skimu sasa hata ya kutengeneza kutoka Ziwa Victoria. Najua na maeneo mengine yanayozunguka Ziwa Victoria yanatengeneza skimu. Kwenye hili upembuzi yakinifu ufanyike mapema kwenye maeneo yetu ili skimu hiyo zianze kufanya kazi; badala ya wananchi kuzalisha mara moja wazalishe mara tatu na uchumi wao utakuwa umepanda, na uchumi ukipanda tutakuwa tayari tumepata uchumi shindani na shirikishi na hivyo uchumi wetu utaonekana sasa ni shindani hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya hifadhi ya chakula. Nimeziona tani 400,000 zinatakiwa kuhifadhiwa, sina uhakika kama maeneo mengine walipata shida kama ya kwangu kwamba debe la mahindi mwaka jana lilifikia shilingi 25,000 mpaka 27,000. Kwa hiyo niombe sana uhifadhi wa chakula ufanyiwe kazi kwa umakini zaidi ili inapotekea crisis kama iliyotokea mwaka jana au mwaka huu wa fedha Serikali iwe na uwezo wa kuwasaidia wananchi wasikutane na bei ambazo sasa hawawezi kununua tena. Ninaamini hili likifanyika mambo yatakuwa mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna sekta nyingine ya uzalishaji ambayo ni ya uvuvi. Nimeona wanasema watanunua boti 160 wameshanunua 118. Kuna kitu cha kufanya hapa. Kwenye uvuvi ndani ya nchi hii jirani yangu tu Mwijage hapa boti 160 zikipelekwa hazitoshi, nchi nzima boti 160? Hapa naomba tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu waangalieni kwa jicho la huruma hawa watu wa uvuvi. Hatuwezi kupeleka boti 160 nchi nzima tukasema tumeenda kuchangamsha sekta ya uvuvi, tutakuwa bado hatujafanya kitu cha maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye mifugo ukiangalia bado tuna hoja kubwa ya malisho. Kwa hiyo mifugo tuliyonayo haina tija, tuna mifugo mingi lakini ukiangalia ng’ombe mmoja anatoa lita moja, bado hakuna tija kwenye sekta hii. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili liangaliwe upya kuona namna gani tunaweza kutengeneza sekta yetu hii hizi za uzalishaji zikaweza kuwa na tija na uchumi wa nchi ukaweza shindani na shirikishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii kitu cha tatu nilitaka kuchangia niwapongeze sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri. Kulikuwa na hoja ya vijana wanaosoma kwenye vyuo vyetu vya DIT, Mbeya University na Arusha Technical Collage. Hawa wanamaliza form four wanakwenda kule kimsingi ni kama wale wanamaliza form four kwenda form five na form six, lakini wao walitakiwa walipie ada. Sasa hii ada hawa ni watoto wa wakulima lakini Serikali kupitia Mheshimiwa Rais, Rais makini Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliona hili kwamba sasa hawa watu wa DIT wameondolewa ada hiyo. Hizi tertiary institutes tunazihitaji sana kwa ajili kutengeneza kupata mafundi wa viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri mimi huko nyuma nilisoma nikiwa tech…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tumaini Magessa.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)