Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mezani ya kuridhia azimio la makubaliano ya nchi mbili Tanzania na wenzetu wa Dubai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kumbukumbu sikumbuki kama kuna makubaliano yamewahi kuhusisha Watanzania wengi kuyajadili kama haya. Watanzania wengi wamejadili kwenye platform mbalimbali, kwenye mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi yetu, kwenye vyombo vya habari, barabara na kwingine kote na hapa inathibitisha namna ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amejenga mazingira bora, mazuri na salama ya Watanzania kutoa maoni yao bila uoga wala hofu. Wengi sana wamechangia kwa uwazi bila hofu, mijadala ilikuwa inakwenda mpaka saa nane usiku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mijadala ya hii Watanzania wana haki ya kujadili kwa sababu hii nchi yao na wala haina shida, wamejadili na wana haki. Wapo walioonesha hofu na kazi nzuri iliyofanywa na Bunge lako sina mashaka kwamba hofu imeondoka kwa mtu aliyetaka kuelewa hofu imeondoka. Kama kuna watu walikuwa na mashaka na uzalendo na uimara na uthabiti wa Bunge hili bila shaka leo tumethibitisha hili Bunge imara sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana upepo ulivyokuwa unapulizwa walidhani watu watayumba hapa. Waheshimiwa Wabunge mmethibitisha ninyi ni wazalendo, ninyi ni imara, ninyi ni thabiti na hampo hapa kwa bahati mbaya, mko kulinda maslahi ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Samia, kama kulikuwa na watu wana mashaka na uzalendo wake na uimara wake na uthabiti wake bila shaka katika jambo hili tumethibitisha na Rais amethibitisha ni mzalendo, ni imara, ni thabiti anayestahili kuendelea kuaminiwa kuliongoza Taifa letu. Ameonesha ujemedari mkubwa, kelele zimepigwa nyingi, kasimama imara akasema tusonge mbele na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiacha watu wengi ambao kwa kweli walikuwa wana maswali ya hapa na pale na yamejibiwa, wako wachache ambao walitaka kutumia hofu hii kujaribu kulikoroga Taifa letu na hawa vizuri tukashughulika nao vizuri. Kwa sababu mbegu hata kama ni ndogo namna gani ikipuuzwa iko siku itaota, itaathiri Taifa letu na kweli vizuri tusiyumbishe maneno, tusimumunye maneno, hawa tuwakabili usoni mchana kweupe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asilimia 90 ya Watanzania tulizaliwa baada ya Muungano, hizo tofauti hizo huko, hatukuzikuta wala hatuzijui, zilishazikwa baada ya Muungano, sasa bahati mbaya sana anatokea mtu mzima, anaaminika, anakwenda, tumempa heshima na katika watu waliompa heshima ni pamoja na Rais Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais huyu kwa uungwana wake ndiye aliyeamua twende kwenye maridhiano, kwa uungwana kabisa. Hatukubadili sheria, hatukubadili Katiba, Katiba ile ile iliyowafungia, muungwana amewafungulia; sheria zilezile zilizowafungia, muungwana amewafungulia; leo kwa kulewa tu mtu mmoja anataka kusimama kuutumia vibaya uungwana wa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lilianza taratibu, taratibu, tunaanza kuona wanyoosha nyoosha vidole, unasema aah hivi haya maridhiano ndio yanataka kutumika hivi. Hapana, sisi Wana-CCM ndio waasisi wa maridhiano, hatukulazimishwa na mtu, tunayaamini lakini maridhiano yasitumike kuligawa Taifa letu, hilo hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi leo Profesa Mbarawa, uzalendo wake, uungwana wake unaenda kutwezwa kijinga, kilevi; hapana, na kwenye hili lazima tulaani kwa nguvu zote na bahati nzuri mwanzoni watu walikuwa wanaongea pembeni, dada yangu kamleta mwenyewe mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili haliwezi kukubalika, tukianza kuhoji maamuzi ya nchi hii kwa vigezo vya wapi nani anatoka, si sawa. Tunaligawa Taifa letu, tunaharibu nchi yetu na hili lazima lilaaniwe na kila Mtanzania anayetaka haki katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna watu wametoa mifano hapa mimi nilikuwa naagalia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika mbili malizia Mheshimiwa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naangalia nimesoma makubaliano ya Tanzania na Uganda imeandikwa Intergovernmental Agreement between Uganda na Tanzania nikaangalia hii hapa na hii imesainiwa tarehe 25 Mei, 2017 ya bomba la mafuta. Huu hapa na wenyewe unasema hivyo hivyo Intergovernmental Agreement between The United Republic of Tanzania na Emirates of Dubai. Hapa kuna mmoja umesainiwa 2017 kati ya Tanzania na Uganda hakuna maneno, hakuna hofu na haukuletwa hapa, tumesaini, hakuna kelele na vifungu vinafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hapa kwa sababu tumekuwa waungwana, tukasema wacha turidhiane ndiyo midomo inapanuka hivi! Hapana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nataka kusisitiza wasituharibie nchi yetu kwa sababu ya uungwana wetu, hili hatutalikubali, hili tutalinda kwa nguvu zote, uungwana wa Rais lazima ulindwe. Hivyo ninawaomba Wabunge, nawaomba Wabunge wenzangu tupeleke salamu, tupitishe kwa kishindo makubaliano haya na Watanzania watuunge mkono tuwaadhibu wote wanaotaka kuligawa Taifa hili wajifunze na wasirudie tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)