Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia kwenye hoja iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Profesa Mbarawa kuhusu azimio hili.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametufikisha hapa tulipo kuanzia pale safari yetu ilipoanzia kwenye jambo hili. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake njema anayoifanya kwenye eneo la uwekezaji. Mheshimiwa Rais yeye ameamua kulifungua Taifa letu na tumeona uwekezaji tunaoupokea na wawekezaji tunaowapokea ndani ya Taifa letu sasa ni zaidi ya asilimia 100 ya miaka ya nyuma ambayo ilikuwepo. Kwa hiyo, kwa kweli Mheshimiwa Rais tunampongeza sana, hata jambo hili lilikoanzia ni kwenye maonesho ya Dubai Expo 2020 ambayo yalifanyika mwaka 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Mheshimiwa Rais alipoamua kwenda kwenye maonesho yale wapo waliosema kwa nini anakwenda. Kwa hiyo, hili ya kuongea huko nje wala Mheshimiwa Rais naamini halimpi shida kwa sababu ameyazoea, cha muhimu ni kuona anatekeleza malengo yale aliyoapa kuyakeleza kwa niaba ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye siku ya kilele cha maonesho ya Expo siku ya Tanzania tarehe 28 Februari, 2022 Mheshimiwa Rais aliona mikataba 37 ikisainiwa yenye thamani ya shilingi za Kitanzania trilioni 20.5 ambayo kwenye mikataba hiyo 37 tunataraji kutengeneza ajira za vijana wa Kitanzania 205,500. Moja ya mikataba ile 37 ni huu ambao umepelekea kuja na azimio hili, ndio maana nimeanza kwa kumpongeza sana, sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi njema anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia Wabunge mmesema vyema kama kuna Mtanzania hajatuelewa basi huyu ameamua mwenyewe kutokuelewa, lakini elimu iliyotolewa hapa kuanzia alipoanza Profesa Kitila Mkumbo mpaka wa mwisho Mheshimiwa Kigwangalla elimu imefika kwa Watanzania, cha muhimu hapa ni kuunga mkono twende tukatekeleze mkataba huu. (Makofi)

Naomba pia kuongeze pale kwenye hizo hofu ambazo zinasemwa huko nje, bandari yetu imeuzwa, bandari yetu imebinafsishwa, naomba niwaambie Watanzania kuwa bandari yetu iko salama, haijauzwa na haijabinafsishwa; kilichofanyika ni kutafuta mwekezaji kati ya wawekezaji wengi tunaowahitaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam, huyu ni mmoja kati ya wawekezaji wengi tunaowahitaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe Watanzania tulipofanya kongamano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya tarehe 3 Februari, 2023, tulisaini hati za makubaliano nyingine sita na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji kwenye Taifa letu. Moja ya mkataba tuliosaini siku ile ni hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania na Bandari ya Antwerp ya nchini Ubelgiji na lengo lake lilikuwa ni kuimarisha ushirikiano katika uboreshaji wa utoaji huduma wa Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, kama bandari imeuzwa Serikali imeingia hati ya makubaliano nyingine na mwekezaji mwingine ni jambo sio kweli.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bandari yetu ni salama, bado ipo mikoni mwa Watanzania na bado tunawahitaji wawekezaji wengine waje wawekeze kwenye Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine zote tulizonazo ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitamani sana hilo niwaambie Watanzania kwamba bandari yetu ni salama na bado tunahitaji wawekezaji wengine. Profesa Mbarawa na timu yako endelea kututafutia wawekezaji na kuwapokea wawekezaji wetu kwa ajili ya bandari zetu zote na tuweze kufanya vizuri ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)