Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia azimio hili muhimu na kipekee kwa mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, niliomba kuchangia kwa sababu wakati wa bajeti hii ambayo tunaendelea nayo tarehe 23 Juni, 2022 nikiwa nachangia hapa niliiomba Serikali ifikirie namna ya kutafuta wabia wa uendeshaji wa bandari hii na kwa bahati nzuri niliwataja hawa hawa ambao wamekuja kubahatika kuwa wabia wetu ambao DP World. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliwajuaje DP World nikawataja kwenye mchango wangu mwaka jana, mwezi wa sita? Mwaka 2006 nilikuwa nafuatilia mwenendo wa mijadala ya Bunge la Marekani. Alipokuwepo Rais George W. Bush alileta muswada kwenye Bunge la Marekani waridhie DP World wachukue management ya bandari zao sita za Marekani (USA). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mjadala ukawa mkali sana na ulienda ukagusa kila eneo na mjadala ulikuja kusimama kwa sababu waliokuwa wanaendesha bandari za Marekani walikuwa ni P&O wa Uingereza, lakini walinunuliwa na DP World ambapo DP World walikuwa na kila kigezo cha kuendesha, isipokuwa mjadala ule ulikwama Bungeni Marekani kwa sababu za kiusalama kwa upande wao.

Mheshimiwa Spika, hawa DP World ambao Serikali yetu imewachagua uwezo wao sio wa kutilia mashaka hata kidogo. Hata hivyo, tunarudi ni nini tufanye kwa upande wetu?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Priscus, amekwenda vizuri ila hakumalizia vizuri. Baada ya pale kilichotokea; baada ya DP World kukataliwa na Congress ya Marekani, kilichoendelea pale ilichukua kampuni nyingine ambayo sio ya Marekani na ilikuwa ni kampuni ya Uingereza ambayo ndiyo inaendesha zile bandari sita mpaka sasa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Priscus Tarimo.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naendela kusema jambo moja, kuna kipindi katika nchi yetu tulikwama kwenye mambo ya msingi kwa sababu ya baadhi ya viongozi kushindwa kufanya maamuzi. Leo hatuwezi kuacha Mheshimiwa Rais ametuongoza kwenye kufanya maamuzi ya busara, sisi tuikwamishe Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uamuzi ambao tumekwishaanza kuufanyia kazi, azimio lililopo mbele yetu ni azimio la ukombozi kwa kila namna unavyolitazama. Mikutano ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea mambo wanayotuhoji juu ya maamuzi yetu ya ndani ni kwa sababu ya uwezo wetu wa kibajeti, ni kwa sababu tunaendelea kuwa tegemezi.

Mheshimiwa Spika, huu mpango kwa kila angle unayoiangalia unakwenda kutukwamua kwenye bajeti tegemezi. Kama tunakwenda kuitoa bandari kwenye mchango wa trilioni saba kwenda kwenye mchango wa trilioni 26 mpaka 30 kwenye pato letu, tunakwenda kupata uhuru wa kiuchumi na tunakwenda kuyasimamia mambo yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni lazima kwa pamoja tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha azimio hili linapita. Tunapokwenda kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ni lazima pia tuwasikilize hao wanaotukosoa, ni wananchi wetu, wana hoja, lakini ningeomba sana Kitengo cha Mawasiliano cha Serikali kiwe kimetangulia mbele, kwa sababu kwenye hoja hizo, kuna hoja za kuzifanyia kazi, lakini kuna hoja zinahitaji ufafanuzi tu. Kwa nini tuache upotofu utangulie, baadae tuje tufanye kazi ya kusafisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri sisi tuwatangulie katika kutoa ufafanuzi kwenye zile hoja ambazo zimpotoshwa. Hata hivyo, kwenye hoja ambazo ni za msingi zipo ambazo tumezichukua tutazifanyia kazi kwenye hatua zinazofuata, kwenye HGA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye hadithi za Biblia katika busara za Mzee Suleiman, tunakumbuka hoja za wanawake wawili waliokuwa wanagombania mtoto. Busara za Mfalme Suleiman ilikuja pale ili kujua ni yupi mzazi kweli wa yule mtoto aliposema mtoto huyu akatwe nusu wagawanywe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaopinga hili azimio hawaongelei hizi ajira 72,000 watazipata wapi kama tusipopitia hili suala? Hawaongelei haya mapato tutakayoenda kuyapata tutayapata wapi kwa ajili ya Watanzania na maendeleo ya yetu? Hawaongelei kabisa kukua kwa uchumi wetu kutokana na haya. Maana yake wanataka kulizuia na hawana mbadala wa kututoa hapa tulipo kutupeleka mbele. Tukiangalia kiuhalisia namna halisi ni sisi ambao tunaona ni namna gani tunakwenda kusimamia hili azimio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ushauri wa Kamati katika kila angle wamepita mle mle ambapo wananchi ndipo wanapolilia. Ni kwa nini watu wengine waendelee kupotosha wakati uhalisia uko mbele? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba niwashawishi Wabunge wenzangu tuliunge mkono kama ambavyo tumkwishaonesha ili tuweze kupata manufaa haya yanayokuja na hili na mimi siku zote nilikuwa ninasema tunajenga reli ya kisasa hivi reli hiyo itabeba abiria tu? Hiyo hela ambayo tumewekeza au huo mkopo utarudi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuja hawa DP World, wakaweza kuongeza mizigo kwenye bandari yetu kama inavyoonekana hapa kutoka tani milioni 18 mpaka tani milioni 48 maana yake bandari zetu, reli yetu na bandari za kwenye maziwa zitafanya kazi na tutarudisha mikopo na hela tutapata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ahsante sana nimesema nigusie maeneo hayo na ninaunga hoja mkono. (Makofi)