Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, washindwe kabisa kwa jina la Yesu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, haya ni majaribu katika dunia, tunamwomba Mwenyezi Mungu atupitishe salama.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kupata nafasi hii, lakini pili kabla sijapongeza kiongozi wetu wa nchi, nianze kwa kueleza kwamba uchumi duniani unaendeshwa kwa misingi mliyokubaliana kama Taifa na uchumi unazingatia maandiko na sera mlizokubaliana wenyewe, na nchi yetu imekubali sekta binafsi kufanya kazi na Serikali, kwa hiyo sekta binafsi kama tulivyosikia wengine inabeba shughuli za uchumi kwa asilimia 90 na ndio Serikali inawaalika sekta binafsi, lakini Ilani ya Chama cha Mapinduzi na hili lieleweke Ilani ya CCM sio kadi ya CCM, ieleweke ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, sera na ndio ahadi tulizoahidi mwaka 2020, kwa hiyo tunaponukuu kitabu hiki tunaenda kwenye reli tuliyokubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ilani hii kwenye Ibara ya 9(b) pamoja na Ibara ya 14 zinaeleza wazi na kwa sababu ya msingi wa maelezo yangu, nisome maneno machache tu, inasema; “kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani, kwa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukuwa na kustawi pamoja na kuvutia wawekezaji ili kuleta mchango stahiki katika maendeleo ya nchi yetu; lakini pili yake inasema CCM inatambua na kuthamini nafasi ya sekta binafsi hivyo itaendelea kusimamia Serikali katika kuhakikisha kuwa inalinda sekta binafsi pamoja na kuweka mazingira ya kiuchumi na kibiashara yanayo vutia wawekezaji nje na ndani ya nchi yetu.”

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(3)(e) inaeleza wazi mikataba yote itakayokuwa inakutana kati ya nchi na nchi italetwa Bungeni. Ninapoenda kumpongeza Mheshimiwa Rais ni kwa mara ya kwanza ninaweza kusema tunapata mkataba wa nchi na nchi unaletwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jambo hili ni jambo tunatakiwa tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya dhati ya kuweka mambo hadharani katika mambo makubwa yenye maslahi ya Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Watanzania kwamba, maslahi mapana ya Tanzania yanalindwa kwa sababu sisi tunawawakilisha Watanzania wote ambao ni zaidi ya milioni 61. Kwa hiyo nikisema hivyo nielekee sasa kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, nimeusoma huu mkataba, nimeusoma mkataba kwa maana ya makubaliano hayo, lakini sina haja ya kwenda details za huko nyuma, naomba nieleze tu kwamba pale nyuma..., naomba hiyo, kwa sababu nimehama kiti.

Mheshimiwa Spika, mimi sio mwanasheria nimesoma engineering, kwa hiyo nintaka tu niseme kwamba ile appendix I imejibu hofu ya watanzania. Imeeleza kwamba areas of cooperation, imeeleza kwa maana ya phase one na imeeleza phase two tutakazoenda kushirikiana katika jambo hili. Kwa hiyo, nataka niwaombe Watanzania kwamba wanasheria wetu wamesimamiwa na Serikali na kwa sababu na namna ambavyo tumejiandaa vizuri kwenye uwekezaji na kwa historia mbalimbali za huko nyuma ninaamini kabisa makubaliano haya yatakuwa na maslahi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema hapa katika msingi ule ule wa kufungamanisha biashara za wananchi na katika biashara na wananchi wetu ni kwamba sisi tunayo Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Dar es Salaam wanakwmbia inaendeshwa chini ya kiwango kwa maana ya jiografia tuliyonayo, lakini tumekuwa tukishauri hapa Bungeni kwamba tumekuwa tunaendesha chini ya kiwango, tumekuwa na malalamiko mengi ya bandari yetu, tumekuwa hatuwapati wateja wote ambao tunatakiwa kuwapata, lakini meli nyingi zimekuwa zikichelewa hata kushushwa maana yake ni kwamba kuna mambo hatufanyi vizuri ndio maana Serikali ilipofanya tathmini ikajiridhisha kwamba inapaswa iingie sasa utaratibu wa uwekezaji wa ubia ili kuhakikisha kwamba bandari yetu inafanya kazi kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini leo tunavyoongea tumeweza kujenga reli yetu ya SGR. Reli hii ni reli ambayo tumewekeza fedha zaidi ya trilioni 17; ni fedha nyingi sana. Tusipoangalia reli hii au treni hii itakuwa kama toroli kama matoroli mengine, haitakuwa na faida yoyote katika nchi yetu kwa sababu reli inataka mzigo, reli inataka mzigo, kama hatuna mzigo mzuri kutoka Congo na maeneo mengine, reli hii haitarudisha fedha tuliyowekeza pale. Kwa hiyo, ndio maana tukasema kwamba lazima bandari yetu ambayo ni hab iweze kuwa na mzigo wa kutosha na mzigo wa kutosha hauwezi kuja bila kuboresha huduma za kibandari.

Mheshimiwa Spika, tukiboresha huduma za kibandari itasaidia kuchachua uchumi wa nchi yetu wamesema wengine hapa. Kwa hiyo, hoja ni kwamba tunachoangalia hapa ni matokeo yatakayotokea pale mbele yetu, lakini SGR hii itakwenda kuwa na tija kama tutakuwa na mzigo kama nilivyoeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niendelee zaidi niseme mapato yetu ya nchi yetu yanategemea sana pale kwenye bandari yetu. Leo hii soko lile la pale Kariakoo linategemea kwa asilimia kubwa namna mzigo unavyoingia katika bandari yetu. Maana yake ni kwamba leo bandari isipofanya vizuri automatic Kariakoo haitafanya vizuri. Kwa hiyo, nilitaka niseme huu uwekezaji unapokwenda kuwekwa utaenda kuwa na tija kwenye maslahi ya Taifa letu, lakini kama haitoshi tumeambiwa mapato yataongezeka kutoka trilioni saba mpaka trilioni 26 maana yake nini? Sisi bajeti yetu ya mwaka ni trilioni 42 tukiweza kukusanya kwenye bandari peke yake trilioni 26 maana yake tutakuwa na asilimia 62 ya mapato yetu yote yataenda ku-cover kwenye Bajeti Kuu ya Serikali, maana yake tutaondoka kwenye utegemezi wa misaada kutoka nje kwa wale washirika wa maendeleo, maana yake sasa hivi tunategemea asilimia 20 kutoka nje. Maana yake tukiweza kupata trilioni 26 hizi zitaenda kuondoa lile gap tulilokuwa nalo kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hoja yangu nilitaka niseme azimio hili tunapoenda kulipitisha, linaenda kuanzisha safari nzuri ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Wale ambao wanapotosha wanaweza wakawa wana nia mbaya kwa sababu wengine hawapendi tuendelee kupiga hatua, lakini kama haitoshi Mheshimiwa Rais anataka aone nchi yake inakwenda. Tumekuwa hapa na kelele kwenye Mradi wa Mwalimu Nyerere, tumekuwa tunataka kuwa na umeme wetu wa uhakika, tunaenda kuzalisha zaidi ya megawatts 2115, tutaenda kujibu kiu ya Watanzania ya kupata umeme vijijini lakini mradi ule tungekuwa tumesikiliza kelele leo tumefikia asilimia 87. Mheshimiwa Rais ameusimamia vizuri, tungesikiliza watu hawa leo tungerudi tunaendelea kuwa na matatizo ya umeme nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana mradi huu twende mbele matokeo watayaona Tanzania tunayo itamani inakuja kupitia uboreshaji wa bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini maneno mawili ya kuzingatia maombi yangu makubwa ni kuomba sana tutakapomaliza hii IGA kupitisha leo niwaombe kwenye HGAs wataalam wetu na Serikali wasimamie mikataba ya miradi itakayoenda iweze kuwa na maslahi kwa ajili ya Watanzania, ile hofu ya watanzania ambayo ipo iondolewe kupitia mikataba midogo midogo itakayoenda kuwekezwa, lakini kama haitoshi tumeambiwa TPA ndio watakaoendelea kuwa msimamizi wa bandari yetu kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naamini kabisa tutasimamia vizuri mambo ya kiusalama, tutasimamia vizuri sana mambo yote yanayoelekea huko.

Mheshimiwa Spika, nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: La mwisho ni kulinda ajira za Watanzania ili waweze kuwa na faida na mradi huu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo ninaunga mkono na ninaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuunge mkono azimio hili ili Serikali iweze kufanya kazi. (Makofi)