Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mada iliyopo mezani. Kwanza, niunge mkono wasilisho la Mheshimiwa Waziri, lakini niungane kabisa na mapendekezo ya Kamati mbili zilizotuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya makabrasha na mikataba nimeyasoma sana, na nimshukuru sana consultant wangu Mheshimiwa Advocate Lujwahuka aliyeniongoza kipengele kwa kipengele. Kwa hiyo mambo ya mikataba sitayazungumza ila nitaunga mkono kwa kupitia transport and transportation economics, mambo ambayo mimi nina uzoefu nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la bandari au usafiri na usafirishaji kuna wadau wawili wana maslahi, mmoja ni mwenye mzigo. Maslahi ya mwenye mzigo ni mzigo wake ufike haraka sana na ufike salama. Mdau wa pili ni mwenye rasilimali au mwendeshaji, yeye ni kupata chumo alilowekeza return on investment na faida, na apate faida justifiable, siyo awanyonye wale wanaomtegemea. Kwa hiyo, utendaji wa bandari unakwenda namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumze suala lingine kuhusu ushindani wa bandari (the competitiveness of a port); hii inategemea namna gani bandari inaweza kupokea meli, inaitwa vessel turn around, ikaipokea haraka na kuiondoa ikaondoka haraka, yaani kama mtu anakuja, captain anaingia maji ya Dar es Salaam, anaiita Dar es Salaam, Dar es Salaam mnakuja, wanamwambia karibu. Aingie aende bandarini, ashushe, apakie aondoke; hicho no kipimo moja wapo cha competitiveness of a port. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine linaloleta ushindani wa bandari ni muunganiko wa sekta au miundombinu inayofanya hiyo bandari ifanye vizuri, hapo tuna barabara na reli au mfumo mzima wa logistics.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja, Bandari ya Dar es Salaam tumekuwa tukishindwa kuuza matunda na chai itokayo mikoa ya Kusini kwa sababu ya udhaifu wa logistics, yaani matunda wanayapeleka Mombasa na chai wanapeleka Mombasa kwa sababu ya competitiveness hiyo.

Mheshimiwa Spika, sasa competitiveness, indicators nilizozungumza ni vessel turn around, lakini kitu kingine ni ukubwa wa mzigo. Bandari inashika mzigo kiasi gani. Kama mzigo ukipakiliwa China au Singapore meli ikajaa, isisimame popote, ina maana mzigo wetu utakuja haraka, kwa hiyo bandari yetu itakuwa competitive.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama walivyozungumza Wabunge, unakusanya mzigo mzigo kwa sababu huwezi kuwa na mzigo mkubwa na hapo ndipo inapokuja utafute mshirika mwenye uwezo. Siyo siri, DP World anakuja; kwa nini? DP World ameshashika mzigo ulipo, ameshashika Rwanda, ameshashika DR Congo, lakini yeye ni mkusanyaji mzuri wa mizigo huko inakotoka.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tunamchukua? Ni ili tupate mzigo mkubwa meli ije moja kwa moja Dar es Salaam, na Dar es Salaam iwe trans-shipment center ndogo. Kama mizigo inafika hapa basi ipakuliwe hapa na kwenda kwenye nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, competitiveness namba tatu ni speed. Basi kama meli imepakia kutoka itokako moja kwa moja Dar es Salaam itakuja kwa speed kubwa, hakutakuwa na trans-shipment ya suala hilo, ilibidi niliseme hivyo.

Mheshimiwa Spika, ninapozungumza hapa, limezungumzwa suala la TEHAMA. Nadhani Mheshimiwa Mwakyembe atakuwa anasikia, katika watu ambao wamehangaika kuweka mifumo katika Bandari ya Dar es Salaam alikuwa ni Mheshimiwa Mwakyembe. Hata kulazimisha watu walipe kuingiza benki watu walipe kwenye benki watu walikuwa wanakataa. Lakini kwa kuweka TEHAMA, mwekezaji anayekuja anakuja kuweka TEHAMA. Maana yake ni nini? Maana yake anapokuja, kontena likifika mteja ataweza kujua kontena lake limefika, lakini na wenye interests zao wataweza kujua kwamba kontena limefika.

Mheshimiwa Spika, sasa niichambue kwa misingi ya kiuwekezaji. Katika uwekezaji tunaangalia suala la kwanza ni ajira, niwatoe hofu na wote walionipigia simu na walionitumia messages. Ukisoma kifungu namba 13 uwekezaji huu utaongeza shughuli, lakini kifungu namba 13 kinasema ajira za Watanzania waliopo kazini zitalindwa, lakini na Watanzania zaidi watafundishwa ili waweze kupata kazi pale. Kwa hiyo, kiuwekezaji mimi sina tatizo.

Mheshimiwa Spika, suala la pili katika uwekezaji, tunakwenda kuzaa bidhaa. Kimsingi katika hii sekta ya uwezeshaji ni service, huduma zitaongezeka kwa sababu meli zitakuwa zinakuja kwa haraka zinachukua muda kidogo, kutakuwepo big volume, the service will improve kwa sababu una-order mzigo wako, mzigo unafika, unaondoa mzigo wako, unakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuchangamsha uchumi. Hakuna haja ya kuzunguka, tumezungumza kutengeneza industrial zone, tumezungumza kutengeneza logistics center. Zikitengenezwa watakazi-manage ni wananchi, kwa hiyo uchumi utachangamka.

Mheshimiwa Spika, kipengele namba 18 kimezungumza wazi, uwekezaji lazima utupeleke kwenye kulipa kodi. Kutakuwepo na kukusanya kodi. Sasa makusanyo ya kodi yale tunakusanya kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mengine wamezungumza, haya ya disputes. Lakini niwaeleze wasafiri na wasafirishaji kwamba ukisafirisha mzigo kutoka Dar es Salaam, transporter, ukifika kwenye mpaka wa Congo utakwama. Lakini magari yanayotoka Durban hayakwami kwa sababu gani? Ni kwa sababu anayesimamia mizigo kutoka Durban anawasiiana na yule anayekusanya mzingo ndani ya Lubumbashi, mzigo unakusanywa moja kwa moja unaweza kupita. Sisi madereva wetu wanakaa siku 30, hata siku 40 kwenye mpaka wa Tanzania na DRC.

Mheshimiwa Spika, lakini niwambejambo moja, na hili nakuomba Mheshimiwa Waziri unisikilize; mimi katika Ziwa Victoria nina bandari 13, huyo mtu kwenye phase two, usisubiri phase two, mlete kwenye bandari 13 za kwangu, aende Goziba, aende Rwangamile, aende Kyamkwikwi atengeneze bandari ili marine seaport aweze kusafiri na kusafirisha watu. Songoro Marine anashindwa kusafiri kwa sababu hana port nzuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nilisema mwanzoni naunga mkono hoja, lakini Mheshimiwa Waziri umenisikia, mlete huyo mtu atengeneze bandari kwetu, atengeneze bandari Goziba tusafiri. (Makofi)