Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, na mimi kama Wabunge wengine wote tuliopata nafasi ya kuchangia leo kwanza nikushukuru sana, lakini jambo la pili, kama ambavyo unetuongoza kwamba tuna wajibu sasa wa sisi jambo la kwanza kabisa kuisaidia Serikali yetu kutoa tafsiri sahihi kwa watu wanaofuatilia jambo hili ambalo liko mbele yetu kwa sababu kwa bahati mbaya kabisa lilianza kwenda mitaani ama duniani pasipo sisi Wabunge kupata tafsiri sahihi ama kuelewesha kinachoendelea, na kwa bahati mbaya mikataba hii na hasa zaidi huu mkataba wa makubaliano ulioko mbele yetu kati ya nchi ya Dubai na Tanzania wa kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi ulipata kwenda mtaani kabla sisi wengine hatujauona.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kidogo kwanza kuhusu mimi mwenyewe binafsi. Mimi nilipata nafasi ya kuwa opposition kabla sijarudi tena kwenye chama chetu, chama tawala, Chama cha Mapinduzi na bado niko kwenye ma-group ambayo kuna mchanganyiko wa watu, kuna watu wa Chama cha Mapinduzi, lakini pia kuna watu wa opposition.

Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza na mimi nilipopata kusikia ama kuona kwenye ma-group haya watu wakivutana kuhusiana na masuala haya ya makubaliano kati ya nchi ya Tanzania na Dubai hata mimi nilishtuka kwa sababu nilikuwa sijui nini kinaendelea. Nikajipa nafasi ya kusoma na kujifunza, tukakutana na wataalam wakatuelewesha.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana watu wachache waliamua kuchukua vipengele vinavyowafurahisha wao au vile wanavyoamini kwamba vina controversy na kuvipeleka kwenye public badala ya kusoma tafsiri sahihi ya kila jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajaribu kusema tu kwenye mambo machache na nitajikita kwenye article 21 ya mkataba huu pamoja na article ya 22; na niwaombe Watanzania wenzangu, hasa tuliopo kwenye yale ma-group tuliyobishania haya mambo na wenyewe wakaangalie halafu baadae tupate tafsiri ya pamoja.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo nataka niliweke sawa ni hili ambalo limekuwa likipotoshwa mitaani kwamba mkataba huu utatekelezwa kwa kutumia Sheria za Uingereza. Mimi sio mwanasheria, lakini walau Kiingereza ninakifahamu, ukisoma article ya 21 ambayo iko kwenye ukurasa wa 28 kwa Kiingereza na wewe ni mwanasheria, utaniongoza. Inasema hivi;“The governing law of this agreement shall be English Law whereas the governing law of each HGA kwa maana ya Host Government Agreement and the relevant project agreement shall be in the laws of Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo sahihi sana ni kwamba makubaliano haya kati ya nchi ya Tanzania…

SPIKA: Mheshimiwa Mwambe ngoja. Sasa hapo usiseme kwa tafsiri isiyo sahihi, sema kwa tafsiri isiyo rasmi.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi, nashukuru kwa kunirejebisha.

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi sana kipengele hiki kinataka kusema kwamba makubaliano haya yaliyofanywa kati ya nchi ya Dubai na Tanzania yatakuwa kwa kutumia English Law, lakini wanachokisema hapa ni common law kwa sababu Dubai wana sheria zao na Tanzania tuna sheria zetu, kwa hiyo, itatumika common law itakayoweza kuziongoza nchi zote mbili kwenda kutekeleza majukumu waliyokubaliana hapa. Hiyo ni sehemu ya kwanza, kwa hiyo, ule upotishaji, yale maneno kwamba mikataba hii itafanywa kwa kutumia lugha ya Kiingereza, sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele hicho hicho tafsiri yake ni kwamba sasa ndio maana pale wanasema kuna Host Government Agreement, tutakapofanya utekelezaji wa vile vipengele vidogovidogo kati ya Bandari ya Tanzania na Bandari ya Dubai au wale waendeshaji kutoka Dubai itatumika Sheria ya Tanzania kwa sababu mwekezaji atakapokuja Tanzania hatua ya kwanza atakayoifanya ni kusajili kampuni yake BRELA. BRELA inatumia sheria za Tanzania kwa hiyo, hili nalo lazima likae sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo halikuwekwa vizuri sana lilikuwa…

SPIKA: Sasa kwa sababu umesema pia, nikusaidie…

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ndio, naomba unisaidie.

SPIKA: Hicho kifungu chako kiunganishe na kifungu cha tano, ukurasa wa 16. Kifungu cha 5(2) na chenyewe soma.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, Ukurasa wa 16. Kama ulivyoniongoza, article 5 inayosema kuhusu Rights to Develop, Manage or Operate.

Mheshimiwa Spika, kwenye ukurasa wa 16, kifungu kidogo cha pili, kama ulivyoniongoza kinasema hivi, “The State Parties agree the implementation of plans for development of the projects by DPW is subject to the conclusion of definitive Project Agreements, Land Rights and HGAs for each relevant project.” (Makofi)

SPIKA: Sasa mikataba hii ndio inaendana na kile kifungu, itakayoingiwa hapa. Sheria zitakazotumika ni za Tanzania. Haya ahsante. (Makofi)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kuniongoza.

Mheshimiwa Spika, na jambo la pili ambalo limekuwa linaleta sintofahamu ni kuhusu suala la exclusivity. Kuna wanaodai kwamba DPW wamepewa haki ya kutokuingiliwa milele, yaani kwamba pasitokee mtu mwingine yeyote katikati atakayetaka kufanya kitu chochote.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye mkataba huu kwa uelewa wangu, na ilivyo huku ndani ni kwamba kipindi hiki cha majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusiana na uwekezaji unaotakiwa ukafanyike bandarini, kipindi cha miezi 12 pasitokee nchi nyingine hapa katikati kutaka kuonesha interest au kutangaza kwamba anaweza akaja na yeye kutaka kuwekeza kwenye eneo hili ambalo ni eneo la phase one. Hii nayo naomba ikae hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na baada ya hapo sasa naomba nitoe ushauri wangu kwa Serikali; kama ambavyo umetuongoza, lakini pia nilisema nitasoma kifungu cha 22, hiki ni cha subsequent amendment, na yenyewe imekuwa inapotoshwa na utaniongoza kwenye mambo ya kisheria, mimi nakwenda tu kwenye mambo ya Kiingereza, kinasema hivi; This agreement may be amended at any time in writing, by the mutual agreement of the State Parties. No amendment to this agreement will have effect without agreement by the signature and the ratification and/or adoption of the appropriate documentation by the State Parties. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hakuna sehemu inayosema mkataba huu ukiingiwa hakutafanyika makubaliano yoyote, makubaliano haya. Kwa hiyo wajibu wetu Bunge kama ulivyosema kutokana na Kanuni zilizopo, tuna wajibu sasa wa kutaka kuishauri Serikali mambo ambayo yakaingiwe kwenye mkataba.

Mheshimiwa Spika, la kwanza kabisa ambalo napenda kushauri ni kuhusiana na suala la muda. Tutakapoletewa mikataba hiyo midogo midogo laizma ku-define muda ili tuweze kupata uhakika wa tunachokifanya, na ninapendekeza kipindi cha mkataba kiwe ni miaka 25, renewable kila baada ya miaka mitano ili kuona sasa kama performance inayopatikana ni nzuri, basi tuendelee kwa vipindi hivyo vitano mfululizo kwa miaka mitano mitano. Isiwe ni open goal.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei.

TAARIFA

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, huyu mtu anakuja kuwekeza fedha nyingi sana, na fedha zile nazo ziwe recouped kwa muda fulani, payback period itakuwepo, kwa hiyo huwezi kusema ni miaka 25, inaweza ikawa hata miaka 30 kutegemea na aina ya mradi na kutegemea kwamba tija ya uzalishaji faida itakuaje.

SPIKA: Hapo hiyo taarifa inabidi nimlinde. Yeye kwa mawazo yake kasema tunaweza kuanza na miaka 25, ni mawazo yake. Kwa maana ya kwamba Serikali inavyokwenda kuzungumza na huyu mtu hoja ya muda ni muhimu na yeye anapendekeza miaka 25, wewe umetaja 30, labda ni 50, labda ni 10. Kwa hiyo, wote hatujui, tuniambia tu Serikali ikatazame hoja ya muda.

Mheshimiwa Cecil Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na ninaamini muda wangu unalindwa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ninapenda kupendekeza tunapoelekea kwenye hiyo mikataba midogo midogo ya utekelezaji, suala hili la eneo la bandari, ukisoma kwenye haya makubaliano imetaja eneo kubwa sana, na hata ukienda kwenye appendix I na yenyewe imetaja maeneo yaliyopo pale. Sasa wasiwasi uliopo ni kuhusu bandari ambazo zitakwenda kusimamiwa. Kwa hiyo, mimi napendekeza, kwa kuanzia…

SPIKA: Ngoja, eneo kubwa sana ukimaamisha nini?

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kwenye cover ya huu mkataba hapa inasema concerning, naangalia tu kile kipengele cha mwisho; economic and social partnership to the development…

SPIKA: Unasoma wapi, twende pamoja.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kwenye cover ya makubaliano (agreement).

SPIKA: Yaani unasoma jina hapa juu?

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ndiyo, chini kabisa sasa, hizo lines mbili za chini.

SPIKA: Sawa, enhe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, improving performance of sea and lake ports in Tanzania. Sasa unaposema sea and lake ports in Tanzania, linaweza likawa eneo kubwa sana kwa maana…

SPIKA: Hapana, sasa ngoja, ndiyo twende vizuri.

Hili ni jina la mkataba, huku mbele umewekewa hizo appendix I, kama ulivyosema na ukaenda kwenye phase one, ukaenda kwenye phase two; maana yake huu mkataba humu ndani umetaja mambo ambayo yanahusika. Kwa hiyo, hatuwezi kuweka ile namna ambavyo wale watu wameiweka kule nje. Kwa nini, nimesema Bunge la leo lina kazi mbili, hii hapa na kuuelimisha umma kuhusu mkataba huu.

Sasa mkataba huu pamoja na hilo jina la mkataba huku ndani kumetajwa ni mambo gani yanayohusika, na kichwa cha habari cha hiyo appendix I kinaeleza nini hapo Mheshimiwa Mwambe? Kichwa cha habari cha appendix I kinasemaje? Kichwa cha habari tu pale juu. Ukurasa wa 35 hapo juu kabisa, appendix I.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kwenye ukurasa wa 35 appendix I inasema; Areas of Cooperation.

SPIKA: Ambayo ndiyo maana nikakupeleka kule.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Haya yote lazima moja moja wakae mezani wakubaliane, ambalo hawakubaliani linakaa pembeni. Ahsante sana.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Kwa hiyo, na mimi nataka kusisitiza kwenye hili, sasa tutakapotoka nje maana yake lazima tuwe specific kwa haya mambo, kwamba kuna areas of cooperation ambazo zipo na zitakubaliwa kutokana na appendix I badala ya ile tunayoambiwa kwamba iko very general, tutakwenda kila bandari ya Tanzania, tutakwenda mitoni, kwenye maziwa na maeneo mengine. Jambo hili siyo sahihi, lakini lilikuwa likitembea huko mitaani, kwa hiyo tukasome hii appendix I tunaweza tukapata uelewa wa pamoja kwa maana ya sasa bandari zitakazokusudiwa, lakini pamoja na area tutakayo-cover.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninapenda pia kuliweka sawa ni faida zitakazopatikana kwenye utekelezaji wa makubaliano haya kwa maana ya mikataba. Ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Mbarawa kwa maana ya Mheshimiwa Waziri kwenye mikataba hii wakati wa utekelezaji kuna mambo mengi tunakwenda kunufaika na sisi kama nchi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza kabisa ni kupunguza muda wa meli kukaa bandarini ambayo itakwenda kuongeza efficiency; lakini suala la pili ni la kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania kutoka ajira 1,500 lakini tutakwenda mpaka ajira 2,950. Jambo lingine inategemea kuongeza mapato ya Serikali kutoka pesa inayokusanywa sasa hivi bandarini ambayo ni trilioni 7.76 mpaka mwaka 2031 kufikia trilioni 26.70.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya ndiyo mambo ambayo sisi kama Watanzania tuna haja ya kuyaweka sawa na ndugu zetu waliopo nje wanaotusikiliza waamini, na Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wamekuwa wakielezea kuhusu sisi sasa, wananchi watuamini kwamba hatutaweza kwenda kuwaingiza kwenye kitu ambacho siyo kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna Mkataba wa TICTS ulikuwa unatekelezwa, sasa hivi tunakwenda na wengine kama watakuwa DP World au mtu mwingine atakuwa na interest ya kutaka kuja pale, lakini kimsingi hatuwezi kurudia makosa yaliyofanyika huku nyuma.

Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)