Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niungane na wenzangu, lakini kabla nataka na mimi niweke msingi kama ambavyo makubaliano haya yanaweka msingi na msingi wangu nitauweka kutoka kwenye vitabu vya Mwenyezi Mungu, nita-refer Biblia.

Mheshimiwa Spika, Hosea 4:6 inasema; “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa, kwa kuwa wameyakataa maarifa.” Mathayo 22:29 inasema; “Yesu akajibu akawaambia mwapotea kwa kuwa hamyajui maandiko.” Yohana 8:32 inasema; “Tena mtaifahamu kweli na hiyo kweli itawaweka huru.” Methali 11:9 inasema; “Asiyemcha Mungu, humpoteza jirani yake kwa kinywa chake, bali wenye haki watapona kwa maarifa.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanzia hapo, hofu zetu zote ni kutokuwa na maarifa na Serikali inachokifanya sasa hapa leo imetupa maarifa ya kutosha, tuondoe sasa ile dhana yetu tuliyokuwa nayo kwenye vichwa, tukubali kuingiza vitu vipya, ili tusiendelee kudanganywa na kuangamia. Mimi kwa kuwa somo la sheria na mimi pia nilipata kidogo ukakasi, lakini sikutaka kuangamia kwa kukosa maarifa. Nilijipa muda wa kusema nitafute maarifa. Kwenye huu mkataba kwanza kitu cha kwanza unachotakiwa kujua unakwenda kwanza malengo yake ni nini.

Mheshimiwa Spika, kwa sisi tusio wanasheria, watu wa biashara tunapoandika research huwa kuna general objectives na kuna specific objectives. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la jumla la mkataba huu ni kati ya nchi na nchi na hawa nchi na nchi wanaingia makubaliano ya kushirikiana kwenye masuala ya biashara kwenye maeneo ya bandari, automatic bandari zinakuwa kwenye maziwa, kwenye bahari, kwenye mito, hiyo ni ya ujumla na hii utaipata kwenye ibara ya pili; malengo ya mkataba.

Mheshimiwa Spika, ukija Ibara ya nne ya mkataba ambayo inaeleza mawanda au upana ndiyo hiyo tulikuwa tunasema scope, hii imejaribu kuelezea mawanda ya huu mkataba lakini imekwenda specific kwamba hawa nchi wameshaingia makubaliano na wenzetu wale wanafikiri kwamba kampuni ambayo labda inaweza tukaanza nayo ni ya kwao ya uwekezaji kwenye bandari ambayo ni DP World.

Mheshimiwa Spika, wakai-bind kabisa kwa specific objective kwamba ninyi mkienda Tanzania mtaingia mkataba baada ya kuwa hatua zote zimefikiwa pamoja na Bunge kuridhia, mkataba wenu mtakwenda kuingia kwenye maeneo haya. Ndio hiyo appendix moja tuliyoisema imeeleza kwa undani, lakini kilichonifurahisha katika kujua malengo, siyo kwamba bandari zote au maziwa yote au Tanga sijui huko Mtwara wapi zimeingia, hapana. Kwenye hiyo hiyo article four namba mbili inasema; Tanzania will inform Dubai of any other opportunities relating to ports, freezones and logistics sectors in Tanzania to allow Dubai or Dubai entities to express interest and submit proposals for consideration in respect of such other opportunities.

Mheshimiwa Spika, kwamba sisi Tanzanaia ndiyo tutakuwa na mamlaka ya kuwaambia wale Dubai tuna fursa nyingine huku labda kuna Bandari ya Mtwara tunaomba kwa sababu hapa mmefanya vizuri, tunaomba basi na Mtwara mkafanye kitu kama hiki. Wao watakuwa na responsibility ya kutafuta mtaji na kwenda kuendeleza, kusiamia na kuhakikisha wanaboresha. Hivyo ndivyo mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wanasheria wakisoma wanatudanganya kwamba maziwa yote yamechukuliwa, bahari zote zimechukuliwa, mbona namba mbili hamuiangalii kwamba consideration ni sisi ndio tutakao-inform hawa kwamba tuna opportunities nyingine katika hizi water bodies za uwekezaji wa bandari, hapo mimi nikajiridhisha, nikaondoka na kuangamizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mwanasiasa kuna hoja nyingine utaifikiria kwamba je, ardhi ya Watanzania inachukiliwa? Maana ardhi ikishachukuliwa Tanzania maana mimi watu wangu watakaa wapi? Wapiga kura wangu Iringa watakaa wapi au wataenda wapi? Nikaenda Ibara ya nane inaeleza ukurasa wa 18 haki ya ardhi, lakini hapa Ibara hii inaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha hatua muhimu zinachukuliwa ili kuwezesha DP World kupata haki ya matumizi ya ardhi. Yes, lazima sisi kama Watanzania tuwa-guarantee wale matumizi ya ardhi yetu. Wanaleta mitambo, sawa, watawekeza pale. Sasa kama hatutawalinda kwa sheria zetu tukaendelea kuwa na urasimu, tukaendelea kuwa-disturb, unategemea wawekezaji wataendelea kuwepo?

Mheshimiwa Spika, sisi tumepewa jukumu la kuwalinda hawa wawekezaji na ni jukumu la msingi, sio kumiliki ardhi. Katika hii ukurasa wa tisa inaeleza tafsiri, hakuna mtu anakuja kumiliki na kuchukua ardhi ya Watanzania. Ukurasa wa tisa, Land Rights inavyoeleza interpretation inasema; “Land Rights shall mean all those rights (excluding rights of ownership of the land in Tanzania.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imeondoa hilo suala la umiliki wa ardhi, kwa hiyo wao watakuwepo kwenye matumizi ya ardhi. Sisi tunasoma hivi, ili tusiangamie hata kama sio wanasiasa. (Makofi)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, manufaa kwa Watanzania...

SPIKA: Mheshimiwa Jesca Msambatavangu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei.

TAARIFA

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nataka kusema kwamba huu mkataba na anavyozungumza vizuri sana Mheshimiwa wetu, jina lake gumu sana, Mheshimiwa Jesca, ni kwamba wanaangalia logistic ya from Dar es Salaam na kufikisha mzigo Burundi, Rwanda kote na Uganda. Kwa hiyo, lazima wafikirie kwamba ili iwe ni efficient lazima waweze kuboresha bandari za Ziwa Victoria, kama itakuwa hivyo na pia waweze kuweka maeneo ya bandari kavu sawasawa na kadhalika na pia kuwezesha hizi export… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nashukuru sana kwa Taarifa; fahari ya wazee ni mvi kichwani, hiyo ndio hekima ya mzee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwamba wewe huwezi kumpa mtu atoe makontena pale usimpe sehemu ya kuweka makontena. Huyu DP World ana bandari kavu Rwanda, usimpe access ya treni kwenda Rwanda kupeleka makontena yake; ana-supply na South Africa, sijui na wapi huko na Djibouti huko ana mikataba inaendelea, usimpe access kwamba atakwenda hadi huko kupeleka makontena, haiwezekani. Kwa hiyo, ndio maana kuna appendix II kwamba, badae tutakuja kuendelea kuongea sisi tutakapokubali tutamshirikisha yeye.

Mheshimiwa Spika, kama mwanasiasa manufaa hayo mengine ya ushirikishaji, tatizo kubwa tulilonalo saa hizi ni ajira. Mimi nikaangalia changamoto, hivi mimi watu wangu wa Iringa wanaosoma pale Chuo cha Bandari, Dar es Salaam watapata kazi au ndio zinakwisha au wanafukuzwa?

Mheshimiwa Spika, nikaangalia Ibara ya 13 - ushirikishwaji wa wazawa, ajira na majukumu kwa jamii. Tunahangaika hapa kutoa ajira, tunaleta wawekezaji ili tupate ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anasema ibara hii, inaelekeza kuwa mikataba itakayosainiwa ya utekelezaji wa mradi lazima iainishe mpango wa ushirikishwaji wa wazawa katika utekelezaji wa mradi husika, unaona? Na maeneo yafuatayo yatapewa kipaumbele kwenye hii article. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo inasema kutoa kipaumbele kwa kampuni za ndani katika zabuni na ushauri pale ambapo makampuni hayo yatakidhi vigezo. Baadhi ya miradi inayokwenda kutekelezwa iwe imetolewa kwa kampuni za ndani na raia wa Tanzania; kutekeleza mpango wa mafunzo ya uendelezaji wa raia wa Tanzania; kusaidia kujenga uwezo wa vyuo/mafunzo katika tasnia ya usafiri majini na usafirishaji; na kuwezesha tafiti na uhamasishaji wa teknolojia kwa wazawa.

Mheshimiwa Spika, hii tayari msingi umewekwa wazawa wetu sisi…

SPIKA: Sekunde 30 malizia.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, wazawa watapata ajira, lakini na wale waliokuwepo wataboreshwa kwa kupewa mafunzo. Maana asije akasema nimeweka kitu cha kisasa hapa Mtanzania hawezi, tunataka ampe mafunzo aweze kuki-operate kile kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka nini?

SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, mimi naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)