Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante na nichukue fursa hii kwanza kabisa kumpongeza Kiongozi wetu Mkuu na Jemedari Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuifanya Tanzania isonge mbele na ipate maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nimshukuru Waziri Mkuu na kumpongeza kulifanya jambo hili kama msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali kuweza kulifikisha hapa lilipo, namna ambavyo amelisimamia na kuweza kushauri wataalamu wote kwa ujumla pamoja na Rais wetu ametutendea haki kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii ya kipekee kuishukuru timu nzima iliyoweza kuishauri Serikali hususan wanasheria wetu kutoka Wizara na kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Kwa mara ya kwanza nikiwa ndani ya Bunge lako tukufu nikishuhudia mkataba huu ukija kwa uwazi zaidi. Ifikie wakati kama Watanzania tutambue wapi tunatoka na tunakwenda wapi. Namna ambavyo mkataba huu umeletwa ndani ya Bunge ni makubaliano ya wazi yasiyojificha na kuna muda tuchukue kuwapongeza watu ambao wanafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Waziri umefanya kazi vizuri, umeweka uzalendo mbele, umelitendea haki Taifa la Tanzania, timu yako tumefanya nayo kazi kwa kuuliza swali moja moja. Mimi binafsi nimemtafuta kati ya timu, mtu mmoja ambaye alikuwemo kuhusika na hili nikajiridhisha menyewe na hichi kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamefanya kazi kwa uchambuzi wa kina, hoja zote za Watanzania wamezizingatia hata zilizokuwa zikipita ndani ya mitandao. Hata na mimi kama Mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi nadni ya Bunge hili kuna maeneo na vipengele nilikuwa navihisi kwamba haviko sawa, lakini nichukue fursa hii kuwaambia wananchi wa Tanzania waondoshe hofu, Serikali yao iko makini, viongozi wao wako makini, Bunge liko makini, Waziri Mkuu yuko makini, Spika yuko makini. Imefanywa kazi hii kwa umahiri mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi ripoti zote zimepitiwa kupitia Kamati zako za Bunge. Kamati zimejiridhisha na sisi tuliokuwa hatupo ndani ya Kamati tumeyatafuta na tumejiridhisha kuona makubaliano haya hayana chembe ya shaka. Kuna maneno yanayozungumza kwamba huu ni mkataba, Watanzania ifike wakati tuamke, tujue hizi kelele zinatoka wapi. Hakuna vita vikubwa duniani kama vita vya uchumi, hakuna kitu kikubwa duniani kama kitu cha kupiga hatua ya maendeleo. Siku zote hata maendeleo ya mtu binafsi yeye mwenyewe lazima apate vita, atapata vita kwa marafiki zake, atapata vita kwa majirani zake, atapata vita kwa watu waliomzunguka. Hii vita tuliyokuwa nayo ni Tanzania ya kusonga mbele ifike wakati Watanzania mjue kwamba maamuzi yanayotolewa ni maamuzi ambayo ni kwa maslahi ya nchi na si kwa maslahi ya mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani zaidi ya Wabunge 300 na tuko ndani ya Bunge tuone kwamba kitu hiki kinachoenda kufanyika kama ni cha hovyo tukakiridhia, hicho kitu hakiwezekani abadani, na mimi niliesimama hapa ni Mbunge wa CCM nitasema kweli daima kwenye hili wamefanya haki, wametutendea haki wanasheria wametutendea haki katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna vipengele zaidi ya vipengele nane ndani ya makubaliano haya, Watanzania wanavizungumza. Hofu yao ni jambo ambalo linatufanya sisi tufanye utekelezaji wa kina, Watanzania tunawapongeza, hofu yenu imetufanya tuwe na bidii na kufanya kazi hii kwa kina na uaminifu. Hofu yenu imetujengea uimara wa kufanya kazi hii kwa uangalifu mkubwa, tuwaahidi kama mlivyotupa ridhaa ya kuwawakilisheni ndani ya nyumba hii tunahakikisha tutawatendea haki. Ondoeni hofu kazi hii inaenda kufanyika kwa uweledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la ubaguzi; wakati huu tuliokuwa nao ukimuona Mtanzania hususan mwenye uongozi anayeongoza watu, anatamka kauli ya ubaguzi tunamshangaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilyesimama hapa naitwa Tauhida Gallos Nyimbo; Nyimbo ni mtu wa Songea baba yangu ni mtu wa Songea, mama yangu ni Mzaramu. Mimi nimezaliwa Zanzibar na Mbunge kutoka Zanzibar, leo tukisimama Watanzania tunaanza kubaguana hatutofika na dhambi ya ubaguzi ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitegemea kiongozi ndani ya Tanzania utakuja na hoja za msingi, Serikali yetu haikatai kukosolewa, makosa ambayo tunayakosoa inafanya uboreshaji zaidi. Nilitegemea kumuona kiongozi anayeongoza watu anahubiri amani, umoja na mshikamo pale ambapo anapoona kuna makosa anapaswa kurekebisha hayo makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ninajishangaa, kiongozi wa siasa anapoleta ubaguzi ndani ya chama chake, Naibu Katibu Mkuu anatoka Zanzibar, ninajiuliza anajifikiria vipi? Ana sehemu hata ya kuchangia kapata maamuzi ndani ya hivyo vikao vyao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Zanzibar katika sehemu ambayo ilikuwa kwa muda mrefu inakusanya mapato ZRB msimamizi wake anatoka Bara, hakuna kelele, hakuna zogo na mapato yanakusanywa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya utawala wa ZBC Zanzibar Mkurugenzi mmoja anatoka Bara, alishawahi kuwa NEC katika nafasi ya Chama cha Mapinduzi, sasa hivi ni Mkurugenzi ZBC, tunataka Tanzania hiyo ya kutoka Songea mpaka Makunduchi, hii ni Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka Wabunge tufike wakati tutamani kumuona mtu anayetoka hapa ndani ya jengo hili anakuwa pia ni Rais wa Zanzibar kutoka Bara. Tuipelekeni Tanzania huko, tuionesheni Katiba yetu na kuiboresha, tuhakikishe Tanzania inakuwa moja watu wa Tanzania wanakuwa wamoja, itikadi za kisiasa tusiivunje Tanzania, itakadi ya kisiasa isimvunje mama Tanzania, upendo wetu ndio umoja wetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja azimio hili asilimia mia moja, ahsante. (Makofi/ Vigelegele)