Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza na mimi niungane na wengine kukupongeza Mheshimiwa Waziri na msaidizi wako kwa hotuba nzuri lakini kipekee kama Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo nisimame hapa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tukio kubwa na la kihistoria linaloendelea Mkoa wa Njombe. Kwa ulipwaji wa fidia uliozinduliwa leo kwenye miradi ya Liganga na Mchuchuma, kama kamati tunafarijika na hasa mimi ambaye nimekuwa kinara wa jambo hili ninapoona hatua hii kubwa ya ku-inject shilingi bilioni 15 kwa ajili ya wananchi maana yake tunaona mradi mkubwa wa kimkakati wa kulinyanyua Taifa hili wa uchimbaji wa chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma sasa unaenda kufanya kazi. Tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia upande wangu mimi wa kuchangia, kama nilivyosema mimi ni Mjumbe wa Kamati na kwenye kamati yetu tangu tumefika kumekuwa na habari ya zile risiti za electronic au ambazo zimekuwa zinafanywa na Kampuni ya SICPA. Sasa nilikuwa naomba nijielekeze hapa kwenye habari ya risiti za ETS ili walau na mimi niweze kupata nafasi ya kuchangia jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wametufuata sana kwenye Kamati nadhani tangu miaka hii miwili yote iliyopita na hata juzi walikuwa hapa wanaendelea na jambo hili. Hili Bunge ni la wananchi, wafanyabiashara kila wanapohisi kwamba wanahitaji msaada wamekuwa wanakimbilia katika Bunge. Sasa mimi kama mjumbe tumekaa miaka yote hii lakini bado hatujapata majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikawa nimekuja leo, naomba nitoe ushauri tu kwa Waziri wa Fedha, nadhani anakumbuka vikao tulishafanya mpaka Kamati ya Uongozi wa Bunge na wewe mwenyewe ukiwemo, maofisa wa TRA; wafanyabiashara wanayo hoja na hoja ambayo lazima isikilizwe. Hii ni kwa sababu hawa ndiyo wanaolipa kodi, ni wazalishaji wakubwa wameajiri Watanzania. Kwa hiyo hatuwezi kuendelea kufanya nao bisahara huku wakiwa wana sononeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, point yao kubwa ni kwamba gharama ziko juu sana ukilinganisha na nchi nyingine; na wao wanasema mwanzo walivyoanza zilikuwa kampuni karibu tisa na huyu muwekezaji akasema amewekeza mtaji. Kwa hiyo angetakiwa ku-recuperate ile capital yake ambayo ameweka na akawa anawachaji juu akitegemea kwamba baada ya muda ingeshuka. Sasa kutoka kampuni tisa zilizoanza sasa tuna kampuni zaidi ya 200 sasa. Kwa hiyo wafanyabiashara wanahisi zile gharama inabidi zishuke ili na wao waweze kuji-tune na wafanye biashara katika unafuu zaidi waweze kuajiri Watanzania wengi na kupanua wigo wa biashara zao; nadhani ameongelea Mheshimiwa Vuma hapo

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu jambo moja Mheshimiwa Waziri. Tumeliongea sana kwenye kamati hili lione. Ongea na mwekezaji huyo aliyepo ambaye anafanya kazi hii ili ashushe gharama hizi ili kwa pamoja wafanyabiashara pia waweze kuridhika. Na kwa sababu wao wamekuwa wanakuja kwenye Kamati na wewe hujawahi kukaa nao, sasa, andaa kikao awepo mzabuni, wawepo wafanyabiashara na wewe mwenyewe ikiwezekana na Kamati tukae hili jambo tujadili kwa pamoja. Kwa sababu haiwezekani tukawa tunafanya biashara na watu ambao wana lalamika. Mwwekezaji kawekeza mtaji wake na hivyo ni lazima tujue amewekeza fedha lakini aone pia jinsi ya kupunguza ili iwe justifiable kwa sababu hiki kitu watu wanaona. Dunia ni kijiji, wewe mwenyewe katika bajeti hii ulituhubiria kwamba tutaenda kufanya biashara yaani tutaendesha Serikali kidijitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo leo kila kitu kiko wazi. Kila kinachofanyika sehemu yoyote kiko wazi watu wanaona. Kwa hiyo tuombe hili ulichukue wafanyabiashara wakapatiwe unafuu ili waweze kufaidika na kile kidogo wanachokizalisha na Watanzania waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikitoka kwenye habari ya SICPA au kwenye stempu hizi za ETS, mimi ni mjumbe kama nilivyosema, kilimo kiko kwetu. Mheshimiwa Waziri mme-inject fedha nyingi sana kwenye Mradi wa BBT, nyote ni mashahidi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa project hiyo ambayo inaenda kuinua vijana na wakina mama; lakini iko habari ya Benki yetu ya Kilimo (Tanzania Agricultural Development Bank). Hii benki kwenye Azimio la Bunge la mwaka jana mwezi Novemba kwenye Ripoti ya PAC walisema kabisa kwamba benki ilipewa mtaji wa bilioni 208 na kukawa na ahadi ya Serikali kuiongezea mtaji mpaka ifike shilingi bilioni 760 lakini hatujapata ripoti kujua kazi hii ilifanywa vipi na so far mmeongeza nini na mwaka wa fedha unaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunachoomba ahadi ilikuwa kufikisha mtaji wa benki hii iwe shilingi bilioni 760. Mheshimiwa Waziri hatuwezi…

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji Serikali ingeipa Benki ya TADB bilioni 100 ingelikuwa na mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 760, ingewakopesha wakulima wengi, ingekopesha vyama vya ushirika vingi na ingeleta mapinduzi makubwa kwenye hii sekta ya kilimo nchini. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ezra taarifa?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa naipokea na ndipo hapo nilikuwa naendelea; kwamba maelekezo au Azimio la Bunge tuwe tunatoa shilingi bilioni 100 kila mwaka. Kwahiyo tunachoomba azimio lile ambalo Bunge lako lilipitisha mwaka jana Novemba hebu liweze kufanyiwa kazi. Kwa sababu kwa sisi tunaotoka vijijini siyo kila mtu yuko kwenye BBT, wala siyo kila mtu anaweza kukopesheka benki, wengine hawana dhamana kwenye benki za biashara. Benki yetu hii riba ni ndogo, asilimia tisa hadi asilimia kumi na mbili, si kila benki inaweza kutoa hivyo. Kwa hiyo tunachoomba mtaji uongezwe ili wakulima wetu huko vijijini waweze kupata nafasi ya kuweza kushiriki uchumi na hasa fedha hizi ambazo Mama Samia anazitoa sehemu nyingi na anavyozidi kuifungua nchi kiuchumi hata sisi huko vijijini waweze kushiriki kufanya uchumi wa nchi hii hatimaye waweze kupata maendeleo; niliombe hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha najua mikopo ile ya asilimia 10 imesitishwa. Niombe kwenye hili, kipindi mnajaribu kuangalia kanuni na ukopeshaji mpya, kundi la vijana ni kundi linalokua. Unapoweka kijana wa miaka 35, these guys are still teenagers. Walio wengi hawajajua hata thamani ya ile fedha, mnawapa hii fedha baadaye wanaanza kusumbuana na halmashauri. Ongezeni umri at least miaka 45 na wenyewe bado ni vijana. Waende huko wapewe watu ambao kidogo wako matured hizi fedha watazipata watafanyia biashara, watawaajiri wale vijana wenye miaka 18, 20 waweze kufanya nao kazi huku fedha iki-rotate na kurudi; kuliko leo ambavyo unampa fedha mtu kijana wa miaka 18 au 25 haendi, hajui aitumiaje. Lakini kwa sababu ameambiwa fedha ipo anachukua na hatimaye anashindwa kuirejesha na thamani ya ile fedha inashindwa kuonekana…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru. (Makofi)